Wagalatia Mlango 5 Galatians

Wagalatia 5:1 Galatians 5:1

Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa.

Wagalatia 5:2 Galatians 5:2

Tazama, mimi Paulo nawaambia ninyi ya kwamba, mkitahiriwa, Kristo hatawafaidia neno.

Wagalatia 5:3 Galatians 5:3

Tena namshuhudia kila mtu atahiriwaye, kwamba ni wajibu wake kuitimiza torati yote.

Wagalatia 5:4 Galatians 5:4

Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema.

Wagalatia 5:5 Galatians 5:5

Maana sisi kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani.

Wagalatia 5:6 Galatians 5:6

Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo.

Wagalatia 5:7 Galatians 5:7

Mlikuwa mkipiga mbio vizuri; ni nani aliyewazuia msiitii kweli?

Wagalatia 5:8 Galatians 5:8

Kushawishi huku hakukutoka kwake yeye anayewaita ninyi.

Wagalatia 5:9 Galatians 5:9

Chachu kidogo huchachua donge zima.

Wagalatia 5:10 Galatians 5:10

Nina matumaini kwenu katika Bwana, ya kwamba hamtakuwa na nia ya namna nyingine. Lakini yeye anayewafadhaisha atachukua hukumu yake, awaye yote.

Wagalatia 5:11 Galatians 5:11

Nami, ndugu zangu ikiwa ninahubiri habari ya kutahiriwa, kwa nini ningali ninaudhiwa? Hapo kwazo la msalaba limebatilika!

Wagalatia 5:12 Galatians 5:12

Laiti hao wanaowatia mashaka wangejikata nafsi zao!

Wagalatia 5:13 Galatians 5:13

Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo.

Wagalatia 5:14 Galatians 5:14

Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako.

Wagalatia 5:15 Galatians 5:15

Lakini mkiumana na kulana, angalieni msije mkaangamizana.

Wagalatia 5:16 Galatians 5:16

Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.

Wagalatia 5:17 Galatians 5:17

Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.

Wagalatia 5:18 Galatians 5:18

Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria.

Wagalatia 5:19 Galatians 5:19

Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,

Wagalatia 5:20 Galatians 5:20

ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,

Wagalatia 5:21 Galatians 5:21

husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.

Wagalatia 5:22 Galatians 5:22

Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,

Wagalatia 5:23 Galatians 5:23

upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.

Wagalatia 5:24 Galatians 5:24

Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.

Wagalatia 5:25 Galatians 5:25

Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.

Wagalatia 5:26 Galatians 5:26

Tusijisifu bure, tukichokozana na kuhusudiana.