Yoeli Mlango 1 Joel

Yoeli 1:1 Joel 1:1

Neno la Bwana lililomjia Yoeli, mwana wa Pethueli.

Yoeli 1:2 Joel 1:2

Sikieni haya, enyi wazee; Sikilizeni, enyi wenyeji wote wa nchi. Je! Mambo haya yamekuwako katika siku zenu, Au katika siku za baba zenu?

Yoeli 1:3 Joel 1:3

Waarifuni watoto wenu habari yake, Watoto wenu wakawaambie watoto wao, Na watoto wao wakakiambie kizazi kingine.

Yoeli 1:4 Joel 1:4

Yaliyosazwa na tunutu yameliwa na nzige; na yaliyosazwa na nzige yameliwa na parare; na yaliyosazwa na parare yameliwa na madumadu.

Yoeli 1:5 Joel 1:5

Levukeni, enyi walevi, mkalie; Pigeni yowe, ninyi nyote mnywao divai; Kwa sababu ya divai mpya; Maana umekatiliwa mbali na vinywa vyenu.

Yoeli 1:6 Joel 1:6

Maana taifa limepanda juu ya nchi yangu, Lenye nguvu, tena halina hesabu; Meno yake ni kama meno ya simba, Naye ana magego ya simba mkubwa.

Yoeli 1:7 Joel 1:7

Ameuharibu mzabibu wangu; ameuvunja mtini wangu; ameyaambua magamba yake kabisa; ameuangusha chini; matawi yake yamefanywa kuwa meupe.

Yoeli 1:8 Joel 1:8

Ombolea kama mwanamwali avaaye magunia Kwa ajili ya mume wa ujana wake.

Yoeli 1:9 Joel 1:9

Sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji Zimekatiliwa mbali na nyumba ya Bwana; Hao makuhani, wahudumu wa Bwana, wanaomboleza.

Yoeli 1:10 Joel 1:10

Shamba limeharibika, nchi inaomboleza; maana nafaka imeharibika, divai mpya imekauka, mafuta yamepunguka.

Yoeli 1:11 Joel 1:11

Tahayarini, enyi wakulima; Pigeni yowe, enyi watunzaji wa mizabibu; Kwa ajili ya ngano na shayiri, Maana mavuno ya mashamba yamepotea.

Yoeli 1:12 Joel 1:12

Mzabibu umesinyaa, mtini nao umevia; Nao mkomamanga na mtende na mtofaa; Naam, miti yote ya mashamba imekauka; Maana furaha imekauka katika wanadamu.

Yoeli 1:13 Joel 1:13

Jikazeni mkaomboleze, enyi makuhani; Pigeni yowe, enyi wahudumu wa madhabahu; Njoni mlale usiku kucha katika magunia, Enyi wahudumu wa Mungu wangu; Kwa kuwa sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji Zimezuiwa katika nyumba ya Mungu wenu.

Yoeli 1:14 Joel 1:14

Takaseni saumu, iteni kusanyiko la dini, Wazee na wakusanye wenyeji wote wa nchi; Waende nyumbani kwa Bwana, Mungu wenu, Na kumlilia Bwana,

Yoeli 1:15 Joel 1:15

Ole wake siku hii! Kwa maana siku ya Bwana inakaribia, nayo itakuja kama uangamivu utokao kwake aliye Mwenyezi.

Yoeli 1:16 Joel 1:16

Je! Chakula hakikukatiliwa mbali mbele ya macho yetu? Naam, furaha na kicheko mbali na nyumba ya Mungu wetu?

Yoeli 1:17 Joel 1:17

Mbegu zinaoza chini ya udongo wake; ghala zimeachwa ukiwa; mabanda yamevunjika; kwa maana nafaka imekauka.

Yoeli 1:18 Joel 1:18

Jinsi wanyama wanavyougua! Makundi ya ng'ombe yamefadhaika, kwa sababu hawana malisho; naam, makundi ya kondoo yamepata mateso.

Yoeli 1:19 Joel 1:19

Ee Bwana, nakulilia wewe; Kwa maana moto umeyala malisho ya nyikani, Na miali ya moto imeteketeza miti yote ya mashamba.

Yoeli 1:20 Joel 1:20

Naam, wanyama wa mashamba wanakutwetea wewe; Kwa maana vijito vya maji vimekauka, Na moto umeyateketeza malisho ya nyikani.