Nehemia Mlango 13 Nehemiah

Nehemia 13:1 Nehemiah 13:1

Siku hiyo walisoma katika kitabu cha Musa masikioni mwa watu; na ndani yake yalionekana maneno haya yameandikwa, ya kwamba Mwamoni na Mmoabi wasiingie katika kusanyiko la Mungu milele;

Nehemia 13:2 Nehemiah 13:2

kwa sababu hawakuwalaki wana wa Israeli kwa chakula na maji, bali walimwajiri Balaamu juu yao ili awalaani; lakini Mungu aliigeuza ile laana kuwa baraka.

Nehemia 13:3 Nehemiah 13:3

Ikawa walipoisikia torati, wakawatenga Israeli na umati wa watu waliochanganyika nao.

Nehemia 13:4 Nehemiah 13:4

Na kabla ya hayo, Eliashibu, kuhani, aliyewekwa avisimamie vyumba vya nyumba ya Mungu wetu, kwa kuwa alikuwa karibu yake Tobia,

Nehemia 13:5 Nehemiah 13:5

alikuwa amemtengenezea chumba kikubwa, hapo walipoweka zamani sadaka za unga, na ubani, na vyombo, na zaka za nafaka, na divai, na mafuta, walivyoamriwa kuwapa Walawi, na waimbaji, na mabawabu; tena sadaka za kuinuliwa zilizokuwa za makuhani.

Nehemia 13:6 Nehemiah 13:6

Lakini wakati huo wote mimi sikuwako huko Yerusalemu; maana katika mwaka wa thelathini na mbili wa Artashasta, mfalme wa Babeli, nalimrudia mfalme; na baada ya siku kadha wa kadha nikaomba ruhusa tena kwa mfalme.

Nehemia 13:7 Nehemiah 13:7

Nami nikaja Yerusalemu, nikafahamu yale mabaya, ambayo Eliashibu ameyatenda kwa ajili ya Tobia, kwa kumtengenezea chumba katika nyua za nyumba ya Mungu.

Nehemia 13:8 Nehemiah 13:8

Nami nikasikitika sana; basi nikavitupa nje vyombo vyote vya Tobia vitoke humo chumbani.

Nehemia 13:9 Nehemiah 13:9

Kisha nikatoa amri, nao wakavisafisha vyumba; nami nikavirudisha humo vyombo vya nyumba ya Mungu, pamoja na sadaka za unga na ubani.

Nehemia 13:10 Nehemiah 13:10

Tena nikaona ya kwamba Walawi hawakupewa sehemu zao; basi wamekimbia Walawi na waimbaji, waliofanya kazi, kila mtu shambani kwake.

Nehemia 13:11 Nehemiah 13:11

Ndipo nikagombana na mashehe, nikasema, Mbona nyumba ya Mungu imeachwa? Kisha nikawakusanya, nikawaweka mahali pao.

Nehemia 13:12 Nehemiah 13:12

Ndipo Yuda wote walipoleta zaka za nafaka, na mvinyo, na mafuta, kwenye hazina.

Nehemia 13:13 Nehemiah 13:13

Nami nikawaweka watunza hazina juu ya hazina, yaani, Shelemia kuhani, na Sadoki mwandishi, na wa Walawi, Pedaya; na wa pili wao alikuwa Hanani, mwana wa Zakuri, mwana wa Matania; kwani walihesabiwa kuwa waaminifu, na ilikuwa juu yao kuwagawia ndugu zao.

Nehemia 13:14 Nehemiah 13:14

Unikumbukie hayo, Ee Mungu wangu, wala usifute fadhili zangu nilizozitenda kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu, na kwa taratibu zake.

Nehemia 13:15 Nehemiah 13:15

Siku hizo naliona katika Yuda watu wengine waliokanyaga mashinikizo ya mvinyo siku ya sabato, na wengine waliochukua miganda, na kuwapakia punda zao; tena na mvinyo, na zabibu, na tini, na namna zote za mizigo, waliyoileta Yerusalemu, siku ya sabato; nami nikashuhudia juu yao siku ile waliyouza vyakula.

Nehemia 13:16 Nehemiah 13:16

Tena wakakaa humo watu wa Tiro, walioleta samaki, na biashara za kila namna, wakawauzia wana wa Yuda siku ya sabato, na mumo humo Yerusalemu.

Nehemia 13:17 Nehemiah 13:17

Ndipo nikagombana na wakuu wa Yuda, nikawaambia, Ni neno baya gani hili mnalofanya ninyi, na kuinajisi siku ya sabato?

Nehemia 13:18 Nehemiah 13:18

Je! Sivyo hivyo walivyofanya baba zenu; na Mungu wetu, je! Hakuyaleta mabaya haya yote juu yetu, na juu ya mji huu? Nanyi hata hivyo mwazidi kuleta ghadhabu juu ya Israeli kwa kuinajisi sabato!

Nehemia 13:19 Nehemiah 13:19

Ikawa malango ya Yerusalemu yalipoanza kuwa na giza kabla ya sabato, naliamuru milango ifungwe, nikaamuru isifunguliwe hata sabato iishe; na baadhi ya watumishi wangu nikawaweka juu ya malango, ili usiingizwe mzigo wo wote siku ya sabato.

Nehemia 13:20 Nehemiah 13:20

Basi wenye biashara na wachuuzi wa bidhaa za kila namna wakalala nje ya Yerusalemu mara mbili tatu.

Nehemia 13:21 Nehemiah 13:21

Ndipo nikawashuhudia, nikawaambia, Mbona mwalala mbele ya ukuta? Mkitenda hivi tena, nitawakamata. Tangu wakati ule hawakuja tena siku ya sabato.

Nehemia 13:22 Nehemiah 13:22

Kisha nikawaamuru Walawi wajitakase, nao waje kuyalinda malango, ili kuitakasa siku ya sabato. Unikumbukie hayo nayo, Ee Mungu wangu, ukaniachilie sawasawa na wingi wa rehema zako.

Nehemia 13:23 Nehemiah 13:23

Tena siku zizo hizo nikawaona wale Wayahudi waliokuwa wameoa wanawake wa Ashdodi, na Amoni, na Moabu;

Nehemia 13:24 Nehemiah 13:24

na watoto wao wakanena nusu kwa lugha ya Ashdodi, wala hawakuweza kunena kwa Kiyahudi, bali kwa lugha ya watu hao mojawapo.

Nehemia 13:25 Nehemiah 13:25

Nikagombana nao, nikawalaani, nikawapiga baadhi yao, na kuwang'oa nywele zao; nikawaapisha kwa Mungu, nikasema, Msiwaoze wana wao binti zenu, wala msiwatwae binti zao ili waolewe na wana wenu, wala na ninyi wenyewe.

Nehemia 13:26 Nehemiah 13:26

Je! Sulemani, mwana wa Daudi, hakufanya dhambi kwa kutenda hayo? Lakini katika mataifa mengi hapakuwa na mfalme mwingine mfano wake. Tena alipendwa na Mungu wake, naye Mungu akamfanya mfalme juu ya Israeli; walakini wanawake wageni walimkosesha hata yeye.

Nehemia 13:27 Nehemiah 13:27

Basi, na sisi, je! Tuwasikilize ninyi kutenda neno hili baya, hata kumhalifu Mungu wetu kwa kuwaoa wanawake wageni?

Nehemia 13:28 Nehemiah 13:28

Na mwana mmoja wa Yoyada, mwana wa Eliashibu, kuhani mkuu, alikuwa mkwewe Sanbalati, Mhoroni, basi nikamfukuza kwangu.

Nehemia 13:29 Nehemiah 13:29

Uwakumbuke, Ee Mungu wangu, jinsi walivyounajisi ukuhani, na agano la ukuhani na la Walawi.

Nehemia 13:30 Nehemiah 13:30

Hivyo nikawatakasa na kila kitu kigeni, nami nikawaagizia zamu makuhani na Walawi, kila mtu kazini mwake;

Nehemia 13:31 Nehemiah 13:31

na matoleo ya kuni nyakati zilizoamriwa, na malimbuko. Nikumbuke, Ee Mungu wangu, ili unitendee mema.