Tito Mlango 3 Titus

Tito 3:1 Titus 3:1

Uwakumbushe watu kunyenyekea kwa wenye uwezo na mamlaka, na kutii, na kuwa tayari kwa kila kazi njema;

Tito 3:2 Titus 3:2

wasimtukane mtu ye yote, wasiwe wagomvi, wawe wema, wakionyesha upole wote kwa watu wote.

Tito 3:3 Titus 3:3

Maana hapo zamani sisi nasi tulikuwa hatuna akili, tulikuwa waasi, tumedanganywa, huku tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi, tukiishi katika uovu na husuda, tukichukiza na kuchukiana.

Tito 3:4 Titus 3:4

Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa;

Tito 3:5 Titus 3:5

si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu;

Tito 3:6 Titus 3:6

ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu;

Tito 3:7 Titus 3:7

ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu.

Tito 3:8 Titus 3:8

Ni neno la kuaminiwa; na mambo hayo nataka uyanene kwa nguvu, ili wale waliomwamini Mungu wakumbuke kudumu katika matendo mema. Hayo ni mazuri, tena yana faida kwa wanadamu.

Tito 3:9 Titus 3:9

Lakini maswali ya upuzi ujiepushe nayo, na nasaba, na magomvi, na mashindano ya sheria. Kwa kuwa hayana faida, tena hayana maana.

Tito 3:10 Titus 3:10

Mtu aliye mzushi, baada ya kumwonya mara ya kwanza na mara ya pili, mkatae;

Tito 3:11 Titus 3:11

ukijua ya kuwa mtu kama huyo amepotoka, tena atenda dhambi, maana amejihukumu hatia yeye mwenyewe.

Tito 3:12 Titus 3:12

Wakati nitakapomtuma Artema kwako au Tikiko, jitahidi kuja kwangu huku Nikopoli; kwa maana huku nimekusudia kukaa wakati wa baridi.

Tito 3:13 Titus 3:13

Zena, yule mwana-sheria, na Apolo, uwasafirishe kwa bidii, wasipungukiwe na cho chote.

Tito 3:14 Titus 3:14

Watu wetu nao wajifunze kudumu katika matendo mema, kwa matumizi yaliyo lazima, ili wasiwe hawana matunda.

Tito 3:15 Titus 3:15

Watu wote walio pamoja nami wakusalimu. Tusalimie wale watupendao katika imani. Neema na iwe pamoja nanyi nyote.