Sefania Mlango 1 Zephaniah

Sefania 1:1 Zephaniah 1:1

Neno la Bwana lililomjia Sefania, mwana wa Kushi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amaria, mwana wa Hezekia; katika siku za Yosia, mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda.

Sefania 1:2 Zephaniah 1:2

Nitavikomesha kabisa vitu vyote, visionekane juu ya uso wa nchi, asema Bwana.

Sefania 1:3 Zephaniah 1:3

Nitamkomesha mwanadamu na mnyama; nitakomesha ndege wa angani, na samaki wa baharini, na hayo makwazo pamoja na wabaya; nami nitamkatilia mbali mwanadamu, asionekane juu ya uso wa nchi, asema Bwana.

Sefania 1:4 Zephaniah 1:4

Nami nitaunyosha mkono wangu juu ya Yuda, na juu ya watu wote wakaao Yerusalemu; nami nitayakatilia mbali mabaki ya Baali, yasionekane mahali hapa, na hilo jina la Wakemari pamoja na makuhani;

Sefania 1:5 Zephaniah 1:5

na wale walisujudiao jeshi la mbinguni juu ya dari za nyumba; na hao waabuduo, waapao kwa Bwana na kuapa pia kwa Malkamu;

Sefania 1:6 Zephaniah 1:6

na hao waliorudi nyuma, na kuacha kumfuata Bwana; na hao wasiomtafuta Bwana, wala kumwulizia.

Sefania 1:7 Zephaniah 1:7

Nyamaza kimya mbele za Bwana MUNGU; Kwa maana siku ya Bwana i karibu; Kwa kuwa Bwana ameweka tayari dhabihu, Amewatakasa wageni wake.

Sefania 1:8 Zephaniah 1:8

Na itakuwa, katika siku ile ya dhabihu ya Bwana, nitawaadhibu wakuu, na wana wa mfalme, na watu wote waliovaa mavazi ya kigeni.

Sefania 1:9 Zephaniah 1:9

Na katika siku ile nitawaadhibu hao wote warukao juu ya kizingiti, waijazao nyumba ya bwana wao udhalimu na udanganyifu.

Sefania 1:10 Zephaniah 1:10

Na katika siku ile, asema Bwana kutakuwako sauti ya kilio kutoka lango la samaki, na mlio mkuu katika mtaa wa pili, na mshindo mkuu kutoka milimani.

Sefania 1:11 Zephaniah 1:11

Haya! Lieni, ninyi mkaao katika Makteshi, maana wafanya biashara wote wameangamia; hao wote waliokuwa na mizigo ya fedha wamekatiliwa mbali.

Sefania 1:12 Zephaniah 1:12

Kisha itakuwa wakati ule, nitauchunguza Yerusalemu kwa taa; nami nitawaadhibu watu walioganda juu ya sira zao; wasemao katika mioyo yao, Bwana hatatenda mema, wala hatatenda mabaya.

Sefania 1:13 Zephaniah 1:13

Na huko utajiri wao utakuwa mateka, na nyumba zao zitakuwa ukiwa; naam, watajenga nyumba, lakini hawatakaa ndani yake; nao watapanda mizabibu, lakini hawatakunywa divai yake.

Sefania 1:14 Zephaniah 1:14

Hiyo siku ya Bwana iliyo kuu i karibu; I karibu, nayo inafanya haraka sana; Naam, sauti ya siku ya Bwana; Shujaa hulia kwa uchungu mwingi huko!

Sefania 1:15 Zephaniah 1:15

Siku ile ni siku ya ghadhabu, Siku ya fadhaa na dhiki, Siku ya uharibifu na ukiwa, Siku ya giza na utusitusi, Siku ya mawingu na giza kuu,

Sefania 1:16 Zephaniah 1:16

Siku ya tarumbeta na ya kamsa, Juu ya miji yenye maboma, Juu ya buruji zilizo ndefu sana.

Sefania 1:17 Zephaniah 1:17

Nami nitawaletea wanadamu dhiki, hata watakwenda kama vipofu, kwa sababu wamemtenda Bwana dhambi; na damu yao itamwagwa kama mavumbi, na nyama yao kama mavi.

Sefania 1:18 Zephaniah 1:18

Fedha yao wala dhahabu yao havitaweza kuwaokoa katika siku ile ya ghadhabu ya Bwana; bali nchi yote pia itateketezwa kwa moto wa wivu wake; maana atawakomesha watu wote wakaao katika nchi hii, naam, ukomo wa kutisha.