Sefania Mlango 3 Zephaniah

Sefania 3:1 Zephaniah 3:1

Ole wake yeye aliyeasi na kutiwa unajisi, mji wa udhalimu!

Sefania 3:2 Zephaniah 3:2

Hakuitii sauti; hakukubali kurudiwa; hakumwamini Bwana; hakumkaribia Mungu wake.

Sefania 3:3 Zephaniah 3:3

Wakuu wake walio ndani yake ni simba wangurumao; makadhi wake ni mbwa-mwitu wa jioni; hawasazi kitu cho chote hata siku ya pili.

Sefania 3:4 Zephaniah 3:4

Manabii wake ni watu hafifu, wadanganyifu; makuhani wake wamepatia unajisi patakatifu, wameifanyia sheria udhalimu.

Sefania 3:5 Zephaniah 3:5

Bwana kati yake ni mwenye haki; hatatenda uovu; kila asubuhi hudhihirisha hukumu yake, wala hakomi; bali mtu asiye haki hajui kuona haya.

Sefania 3:6 Zephaniah 3:6

Nimekatilia mbali mataifa, buruji zao zina ukiwa; nimeziharibu njia kuu zao, hata hapana mmoja apitaye; miji yao imeangamizwa; hamna mtu hata mmoja, wala hapana akaaye huko.

Sefania 3:7 Zephaniah 3:7

Nalisema, Hakika utaniogopa, utakubali kurudiwa; ili yasikatiliwe mbali makao yake, sawasawa ya yote niliyoagiza katika habari zake; lakini waliondoka mapema na kuyaharibu matendo yao yote.

Sefania 3:8 Zephaniah 3:8

Basi ningojeni, asema Bwana, hata siku ile nitakapoondoka kuteka mateka; maana nimeazimia kuwakusanya mataifa, ili nizikutanishe falme, nipate kuwamwagia ghadhabu yangu; naam, ukali wote wa hasira yangu; kwa maana dunia yote itateketezwa kwa moto wa wivu wangu.

Sefania 3:9 Zephaniah 3:9

Maana hapo ndipo nitakapowarudishia mataifa lugha iliyo safi, wapate kuliitia jina la Bwana, wamtumikie kwa nia moja.

Sefania 3:10 Zephaniah 3:10

Maana toka nchi iliyo mbali na mito ya Kushi, waniombao dua, yaani, binti za watu wangu waliotawanyika, wataleta matoleo yangu.

Sefania 3:11 Zephaniah 3:11

Siku ile hutatahayarikia matendo yako yote uliyoniasi; maana hapo nitawaondoa watu wako wanaotakabari na kujivuna, wasiwe kati yako, wala hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu.

Sefania 3:12 Zephaniah 3:12

Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao watalitumainia jina la Bwana.

Sefania 3:13 Zephaniah 3:13

Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewaogofya.

Sefania 3:14 Zephaniah 3:14

Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele, Ee Israeli; Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu.

Sefania 3:15 Zephaniah 3:15

Bwana ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; Hutaogopa uovu tena.

Sefania 3:16 Zephaniah 3:16

Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, Usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee.

Sefania 3:17 Zephaniah 3:17

Bwana, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa; Atakushangilia kwa furaha kuu, Atakutuliza katika upendo wake, Atakufurahia kwa kuimba.

Sefania 3:18 Zephaniah 3:18

Nitawakusanya wanaousikitikia mkutano wa ibada, hao waliokuwa wa kwako; ambao mzigo uliokuwa juu yake ulikuwa fedheha kwao.

Sefania 3:19 Zephaniah 3:19

Tazama, wakati huo nitawapatiliza watu wote wanaokutesa; nami nitamponya yeye achechemeaye, nami nitamkusanya yeye aliyefukuzwa; nami nitawafanya kuwa sifa na jina, hao ambao fedheha yao ilikuwa katika dunia yote.

Sefania 3:20 Zephaniah 3:20

Wakati huo nitawaingizeni, na wakati huo nitawakusanya; kwa maana nitawafanya ninyi kuwa sifa na jina, miongoni mwa watu wote wa dunia, nitakapowarudisha wafungwa wenu mbele ya macho yenu, asema Bwana.