1 Yohana Mlango 3 1st John

1 Yohana 3:1 1stJohn 3:1

Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.

1 Yohana 3:2 1stJohn 3:2

Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.

1 Yohana 3:3 1stJohn 3:3

Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu.

1 Yohana 3:4 1stJohn 3:4

Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.

1 Yohana 3:5 1stJohn 3:5

Nanyi mnajua ya kuwa yeye alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake.

1 Yohana 3:6 1stJohn 3:6

Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua.

1 Yohana 3:7 1stJohn 3:7

Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki;

1 Yohana 3:8 1stJohn 3:8

atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.

1 Yohana 3:9 1stJohn 3:9

Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu.

1 Yohana 3:10 1stJohn 3:10

Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.

1 Yohana 3:11 1stJohn 3:11

Maana, hii ndiyo habari mliyoisikia tangu mwanzo, kwamba tupendane sisi kwa sisi;

1 Yohana 3:12 1stJohn 3:12

si kama Kaini alivyokuwa wa yule mwovu, akamwua ndugu yake. Naye alimwua kwa sababu gani? Kwa sababu matendo yake yalikuwa mabaya, na ya ndugu yake yalikuwa ya haki.

1 Yohana 3:13 1stJohn 3:13

Ndugu zangu, msistaajabu, ulimwengu ukiwachukia.

1 Yohana 3:14 1stJohn 3:14

Sisi tunajua ya kuwa tumepita toka mautini kuingia uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti.

1 Yohana 3:15 1stJohn 3:15

Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake.

1 Yohana 3:16 1stJohn 3:16

Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu.

1 Yohana 3:17 1stJohn 3:17

Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?

1 Yohana 3:18 1stJohn 3:18

Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli.

1 Yohana 3:19 1stJohn 3:19

Katika hili tutafahamu ya kwamba tu wa kweli, nasi tutaituliza mioyo yetu mbele zake,

1 Yohana 3:20 1stJohn 3:20

ikiwa mioyo yetu inatuhukumu; kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu naye anajua yote.

1 Yohana 3:21 1stJohn 3:21

Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu;

1 Yohana 3:22 1stJohn 3:22

na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake.

1 Yohana 3:23 1stJohn 3:23

Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri.

1 Yohana 3:24 1stJohn 3:24

Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye naye ndani yake. Na katika hili tunajua ya kuwa anakaa ndani yetu, kwa huyo Roho aliyetupa.