1 Yohana Mlango 2 1st John

1 Yohana 2:1 1stJohn 2:1

Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki,

1 Yohana 2:2 1stJohn 2:2

naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.

1 Yohana 2:3 1stJohn 2:3

Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake.

1 Yohana 2:4 1stJohn 2:4

Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake.

1 Yohana 2:5 1stJohn 2:5

Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake.

1 Yohana 2:6 1stJohn 2:6

Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda.

1 Yohana 2:7 1stJohn 2:7

Wapenzi, siwaandikii amri mpya, ila amri ya zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Na hiyo amri ya zamani ni neno lile mlilolisikia.

1 Yohana 2:8 1stJohn 2:8

Tena nawaandikia amri mpya, neno lililo kweli ndani yake na ndani yenu; kwa kuwa giza linapita na ile nuru ya kweli imekwisha kung'aa.

1 Yohana 2:9 1stJohn 2:9

Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa.

1 Yohana 2:10 1stJohn 2:10

Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo.

1 Yohana 2:11 1stJohn 2:11

Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.

1 Yohana 2:12 1stJohn 2:12

Nawaandikia ninyi, watoto wadogo, kwa sababu mmesamehewa dhambi zenu, kwa ajili ya jina lake.

1 Yohana 2:13 1stJohn 2:13

Nawaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nawaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mmemshinda yule mwovu. Nimewaandikia ninyi, watoto, kwa sababu mmemjua Baba.

1 Yohana 2:14 1stJohn 2:14

Nimewaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu.

1 Yohana 2:15 1stJohn 2:15

Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.

1 Yohana 2:16 1stJohn 2:16

Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.

1 Yohana 2:17 1stJohn 2:17

Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.

1 Yohana 2:18 1stJohn 2:18

Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho.

1 Yohana 2:19 1stJohn 2:19

Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu.

1 Yohana 2:20 1stJohn 2:20

Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote.

1 Yohana 2:21 1stJohn 2:21

Sikuwaandikia ninyi kwa sababu hamwijui iliyo kweli, bali kwa sababu mwaijua, tena kwamba hapana uongo wo wote utokao katika hiyo kweli.

1 Yohana 2:22 1stJohn 2:22

Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa Yesu ni Kristo? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye Baba na Mwana.

1 Yohana 2:23 1stJohn 2:23

Kila amkanaye Mwana, hanaye Baba; amkiriye Mwana anaye Baba pia.

1 Yohana 2:24 1stJohn 2:24

Ninyi basi, hilo mlilolisikia tangu mwanzo na likae ndani yenu. Ikiwa hilo mlilolisikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana, na ndani ya Baba.

1 Yohana 2:25 1stJohn 2:25

Na hii ndiyo ahadi aliyotuahidia, yaani, uzima wa milele.

1 Yohana 2:26 1stJohn 2:26

Nimewaandikia haya katika habari za watu wale wanaotaka kuwapoteza.

1 Yohana 2:27 1stJohn 2:27

Nanyi, mafuta yale mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha; lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake.

1 Yohana 2:28 1stJohn 2:28

Na sasa, watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili kusudi, atakapofunuliwa, mwe na ujasiri, wala msiaibike mbele zake katika kuja kwake.

1 Yohana 2:29 1stJohn 2:29

Kama mkijua ya kuwa yeye ni mwenye haki, jueni ya kuwa kila atendaye haki amezaliwa na yeye.