Yona Mlango 3 Jonah

Yona 3:1 Jonah 3:1

Neno la Bwana likamjia Yona mara ya pili, kusema,

Yona 3:2 Jonah 3:2

Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa; ukaihubiri habari nitakayokuamuru.

Yona 3:3 Jonah 3:3

Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama Bwana alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu.

Yona 3:4 Jonah 3:4

Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa.

Yona 3:5 Jonah 3:5

Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo.

Yona 3:6 Jonah 3:6

Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu.

Yona 3:7 Jonah 3:7

Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji;

Yona 3:8 Jonah 3:8

bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake.

Yona 3:9 Jonah 3:9

Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe?

Yona 3:10 Jonah 3:10

Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.