Yona Mlango 1 Jonah

Yona 1:1 Jonah 1:1

Basi neno la Bwana lilimjia Yona, mwana wa Amitai, kusema,

Yona 1:2 Jonah 1:2

Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu.

Yona 1:3 Jonah 1:3

Lakini Yona akaondoka akimbilie Tarshishi, apate kujiepusha na uso wa Bwana; akatelemka hata Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi, akatoa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa Bwana.

Yona 1:4 Jonah 1:4

Lakini Bwana alituma upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu na kuvunjika.

Yona 1:5 Jonah 1:5

Basi wale mabaharia wakaogopa, kila mtu akamwomba mungu wake; nao wakatupa baharini shehena iliyokuwa merikebuni, ili kuupunguza uzito wake. Lakini Yona alikuwa ameshuka hata pande za ndani za merikebu; akajilaza, akapata usingizi.

Yona 1:6 Jonah 1:6

Basi nahodha akamwendea, akamwambia, Una nini, Ewe ulalaye usingizi? Amka, ukamwombe Mungu wako; labda Mungu huyo atatukumbuka, tusipotee.

Yona 1:7 Jonah 1:7

Wakasemezana kila mtu na mwenzake, Haya, na mpige kura, mpate kujua mabaya haya yametupata kwa sababu ya nani. Basi wakapiga kura, nayo kura ikamwangukia Yona.

Yona 1:8 Jonah 1:8

Ndipo wakamwambia, Tafadhali utuambie, wewe ambaye mabaya haya yametupata kwa sababu yako; kazi yako ni kazi gani? Nawe umetoka wapi? Nchi yako ni nchi ipi? Nawe u mtu wa kabila gani?

Yona 1:9 Jonah 1:9

Akawaambia, Mimi ni Mwebrania; nami namcha Bwana, Mungu wa mbingu, aliyeziumba bahari na nchi kavu.

Yona 1:10 Jonah 1:10

Ndipo watu wale wakaogopa mno, wakamwambia, Ni jambo gani hili ulilolitenda! Kwa maana watu wale walijua ya kuwa amekimbia, ajiepushe na uso wa Bwana, kwa sababu alikuwa amewajulisha.

Yona 1:11 Jonah 1:11

Basi wakamwambia, Tukutende nini, ili bahari itulie? Kwa maana bahari ilikuwa inazidi kuchafuka.

Yona 1:12 Jonah 1:12

Naye akawaambia, Nikamateni, mnitupe baharini; basi bahari itatulia; kwa maana najua ya kuwa ni kwa ajili yangu tufani hii imewapata.

Yona 1:13 Jonah 1:13

Lakini wale watu wakavuta makasia kwa nguvu, ili wapate kurudi pwani, wasiweze; kwa maana bahari ilizidi kuwachafukia sana.

Yona 1:14 Jonah 1:14

Basi wakamlilia Bwana, wakasema, Twakuomba, Ee Bwana, twakuomba, tusiangamie kwa ajili ya uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa ajili ya damu isiyo na hatia; kwa maana wewe, Bwana, umefanya kama ulivyopenda.

Yona 1:15 Jonah 1:15

Basi wakamkamata Yona, wakamtupa baharini, nayo bahari ikaacha kuchafuka.

Yona 1:16 Jonah 1:16

Ndipo wale watu wakamwogopa Bwana mno, wakamtolea Bwana sadaka, na kuweka nadhiri.

Yona 1:17 Jonah 1:17

Bwana akaweka tayari samaki mkubwa ili ammeze Yona, naye Yona akawa ndani ya tumbo la samaki yule muda wa siku tatu, mchana na usiku.