Waamuzi Mlango 11 Judges

Waamuzi 11:1 Judges 11:1

Basi huyo Yeftha, Mgileadi, alikuwa mtu shujaa sana, naye alikuwa ni mwana wa mwanamke kahaba; Gileadi akamzaa Yeftha.

Waamuzi 11:2 Judges 11:2

Mkewe huyo Gileadi akamzalia wana; na hao wana wa mkewe hapo walipokuwa wamekua wakubwa wakamtoa Yeftha, na kumwambia, Wewe hutarithi katika nyumba ya babaetu; kwa sababu wewe u mwana wa mwanamke mwingine.

Waamuzi 11:3 Judges 11:3

Ndipo Yeftha akawakimbia hao nduguze, akakaa katika nchi ya Tobu; na watu mabaradhuli walikwenda na kutangamana na Yeftha, wakatoka kwenda pamoja naye.

Waamuzi 11:4 Judges 11:4

Ikawa baadaye, wana wa Amoni wakapigana na Israeli.

Waamuzi 11:5 Judges 11:5

Ikatukia, hapo wana wa Amoni walipopigana na Israeli, wazee wa Gileadi wakaenda kumtwaa huyo Yeftha katika ile nchi ya Tobu;

Waamuzi 11:6 Judges 11:6

wakamwambia Yeftha, Njoo wewe uwe kichwa chetu, ili tupate kupigana na wana wa Amoni.

Waamuzi 11:7 Judges 11:7

Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi, Je! Ninyi hamkunichukia mimi na kunifukuza nitoke katika nyumba ya baba yangu? Basi kwani kunijilia hivi sasa wakati mlio katika taabu?

Waamuzi 11:8 Judges 11:8

Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Kwa ajili ya hayo sasa tumegeuka kukuelekea wewe tena, ili uende pamoja nasi na kupigana na wana wa Amoni, nawe utakuwa kichwa chetu juu ya wenyeji wote wa Gileadi.

Waamuzi 11:9 Judges 11:9

Basi Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi Kwamba mwanirejeza kwetu tena ili kupigana na wana wa Amoni, naye Bwana akiwatoa mbele yangu, je! Mimi nitakuwa kichwa chenu?

Waamuzi 11:10 Judges 11:10

Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Yeye Bwana atakuwa shahidi kati yetu; hakika yetu tutafanya sawasawa na neno lako.

Waamuzi 11:11 Judges 11:11

Ndipo Yeftha akaenda pamoja na wazee wa Gileadi, na hao watu wakamfanya awe kichwa, tena mkuu, juu yao; naye Yeftha akanena maneno yake yote mbele ya Bwana huko Mispa.

Waamuzi 11:12 Judges 11:12

Basi Yeftha akatuma wajumbe waende kwa mfalme wa wana wa Amoni akasema, Je! Wewe una nini nami, hata umenijilia kupigana juu ya nchi yangu?

Waamuzi 11:13 Judges 11:13

Mfalme wa wana wa Amoni akawajibu hao wajumbe wa Yeftha Kwa sababu Israeli waliitwaa nchi yangu, hapo walipokwea kutoka katika nchi ya Misri, tokea Arnoni mpaka Yaboki, na hata Yordani; basi sasa rudisha hizo nchi tena pasipo matata.

Waamuzi 11:14 Judges 11:14

Yeftha akatuma wajumbe mara ya pili waende kwa huyo mfalme wa wana wa Amoni;

Waamuzi 11:15 Judges 11:15

akamwambia, Yeftha akuambia hivi; Israeli hakuitwaa nchi ya Moabu, wala nchi ya wana wa Amoni;

Waamuzi 11:16 Judges 11:16

lakini hapo walipokwea kutoka Misri, na Israeli walienenda katika bara hata kuifikilia Bahari ya Shamu, na kufikilia Kadeshi;

Waamuzi 11:17 Judges 11:17

ndipo Israeli wakatuma wajumbe waende kwa mfalme wa Edomu, wakisema, Nakuomba sana unipe ruhusa nipite katika nchi yako; lakini mfalme wa Edomu hakusikia. Ni vivyo wakampelekea wajumbe mfalme wa Moabu; wala yeye hakukubali; basi Israeli wakakaa katika Kadeshi.

Waamuzi 11:18 Judges 11:18

Kisha akaenda nyikani na kuizunguka hiyo nchi ya Edomu, na nchi ya Moabu, nao wakapita upande wa mashariki wa nchi ya Moabu, wakapanga marago upande wa pili wa Arnoni; wala hawakuingia ndani ya mpaka wa Moabu, kwa maana Arnoni ilikuwa ni mpaka wa Moabu.

Waamuzi 11:19 Judges 11:19

Kisha Israeli wakatuma wajumbe waende kwa Sihoni mfalme wa Waamori, mfalme wa Heshboni: Israeli wakamwambia, Twakuomba utupe ruhusa tupite katika nchi yako, mpaka mahali pangu.

Waamuzi 11:20 Judges 11:20

Lakini huyo Sihoni hakuwaamini Israeli ili wapite ndani ya mpaka wake; bali Sihoni akawakutanisha watu wake wote, nao wakapanga kambi katika Yahasa, wakapigana na Israeli.

Waamuzi 11:21 Judges 11:21

Bwana, Mungu wa Israeli, akamtia Sihoni na watu wake wote mikononi mwa Israeli, nao wakawapiga; basi Israeli wakaimiliki hiyo nchi ya Waamori, wenye kukaa nchi hiyo.

Waamuzi 11:22 Judges 11:22

Nao wakaumiliki mpaka wote wa Waamori, tokea Arnoni hata Yaboki, tokea hiyo bara hata Yordani.

Waamuzi 11:23 Judges 11:23

Basi sasa yeye Bwana, Mungu wa Israeli, amewapokonya Waamori watoke mbele ya watu wake Israeli, na wewe wataka kuwatamalaki?

Waamuzi 11:24 Judges 11:24

Je! Wewe hutakitamalaki hicho ambacho huyo Kemoshi mungu wako akupa kukitamalaki? Kadhalika, awaye yote ambaye Bwana, Mungu wetu, amemfukuza atoke mbele yetu hao ndio tutakaowatamalaki.

Waamuzi 11:25 Judges 11:25

Na wewe sasa, je! U mwema kuliko Balaki mwana wa Sipori, huyo mfalme wa Moabu, kwa lo lote? Je! Yeye alishindana na Israeli, au kupigana nao?

Waamuzi 11:26 Judges 11:26

Wakati Israeli waliokuwa wakikaa Heshboni na miji yake, na katika Aroeri na miji yake, na katika miji hiyo yote iliyo huko kando ya Arnoni, muda wa miaka mia tatu; mbona ninyi hamkuipata tena katika majira hayo?

Waamuzi 11:27 Judges 11:27

Basi mimi sikukufanyia wewe dhambi, lakini wewe unanitenda uovu kwa kupigana nami; yeye Bwana, yeye Mwamuzi, na awe mwamuzi hivi leo kati ya wana wa Israeli na wana wa Amoni.

Waamuzi 11:28 Judges 11:28

Lakini mfalme wa wana wa Amoni hakuyasikiza hayo maneno ya Yeftha aliompelekea.

Waamuzi 11:29 Judges 11:29

Ndipo roho ya Bwana ikamjilia juu yake Yeftha, naye akapita katika Gileadi na Manase, akapita na katika Mispa ya Gileadi, na kutoka hapo Mispa ya Gileadi akapita kuwaendea wana wa Amoni.

Waamuzi 11:30 Judges 11:30

Naye Yeftha akamwekea Bwana nadhiri, akasema, Kwamba wewe utawatia wana wa Amoni mkononi mwangu kweli,

Waamuzi 11:31 Judges 11:31

ndipo itakuwa ya kwamba, kile kitakachotoka katika milango ya nyumba yangu kunilaki, hapo nitakaporudi na amani kutoka kwa hao wana wa Amoni, kitu hicho kitakuwa ni cha Bwana, nami nitakisongeza kiwe sadaka ya kuteketezwa.

Waamuzi 11:32 Judges 11:32

Basi Yeftha akavuka kuwaendea wana wa Amoni ili kupigana nao; naye Bwana akawaua mkononi mwake.

Waamuzi 11:33 Judges 11:33

Akawapiga kutoka Aroeri hata kufikilia Minithi, miji ishirini, na mpaka Abel-keramimu, akawapiga kwa machinjo makuu mno. Basi hivyo wana wa Amoni walishindwa mbele ya wana wa Israeli.

Waamuzi 11:34 Judges 11:34

Kisha Yeftha akafika Mispa nyumbani kwake, na tazama, binti yake akamtokea kumlaki, na matari na machezo; naye alikuwa ni mwanawe pekee; hakuwa na mwingine, mwana wala binti, ila yeye.

Waamuzi 11:35 Judges 11:35

Ikawa alipomwona akayararua mavazi yake, akasema, Ole wangu! Mwanangu, umenitweza sana, nawe u mmoja miongoni mwa hao wanisumbuao; kwa kuwa mimi nimemfunulia Bwana kinywa changu, nami siwezi kurejea nyuma.

Waamuzi 11:36 Judges 11:36

Binti yake akamwambia, Baba yangu, wewe umemfunulia Bwana kinywa chako; basi unifanyie sawasawa na hayo yaliyotoka kinywani mwako; kwa kuwa yeye Bwana amekulipia kisasi juu ya adui zako, hao wana wa Amoni.

Waamuzi 11:37 Judges 11:37

Kisha akamwambia baba yake, Basi na nifanyiwe neno hili; niache peke yangu muda wa miezi miwili, ili nipate kwenenda milimani, na kuombolea uanawali wangu, mimi na wenzangu.

Waamuzi 11:38 Judges 11:38

Akamwambia, Haya, enda. Akampeleka mbali muda wa miezi miwili; naye akaenda zake, yeye na wenziwe, akauombolea uanawali wake huko milimani.

Waamuzi 11:39 Judges 11:39

Basi ikawa mwisho wa hiyo miezi miwili, akarudi kwa babaye, aliyemtenda sawasawa na ile nadhiri yake aliyokuwa ameiweka; naye alikuwa hajamjua mtu mume. Kisha ikawa desturi katika Israeli,

Waamuzi 11:40 Judges 11:40

kwamba binti za Israeli waende mwaka baada ya mwaka ili kumkumbuka huyo mwana wa Yeftha, Mgileadi, siku nne katika mwaka.