Waamuzi Mlango 13 Judges

Waamuzi 13:1 Judges 13:1

Wana wa Israeli wakafanya tena yaliyo mabaya mbele za macho ya Bwana, Bwana akawatia katika mikono ya Wafilisti, muda wa miaka arobaini.

Waamuzi 13:2 Judges 13:2

Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto.

Waamuzi 13:3 Judges 13:3

Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume.

Waamuzi 13:4 Judges 13:4

Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi;

Waamuzi 13:5 Judges 13:5

kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.

Waamuzi 13:6 Judges 13:6

Ndipo yule mwanamke akaenda akamwambia mume wake, akisema, Mtu wa Mungu alinijia, na uso wake ulikuwa kama uso wa malaika wa Mungu, wa kutisha sana; nami sikumwuliza, Umetoka wapi? Wala hakuniambia jina lake;

Waamuzi 13:7 Judges 13:7

lakini aliniambia, Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; basi sasa, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi. Maana mtoto huyo atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni, hata siku ya kufa kwake.

Waamuzi 13:8 Judges 13:8

Ndipo huyo Manoa akamwomba Bwana, akisema, Ee Bwana, nakuomba, yule mtu wa Mungu uliyemtuma na aje kwetu mara ya pili, atufundishe hayo yatupasayo kumfanyia huyo mtoto atakayezaliwa.

Waamuzi 13:9 Judges 13:9

Mungu akasikiza sauti ya Manoa; naye malaika wa Mungu akamwendea yule mwanamke tena alipokuwa anaketi shambani; lakini mumewe, Manoa, hakuwapo pamoja naye.

Waamuzi 13:10 Judges 13:10

Basi huyo mwanamke akaenda haraka, akapiga mbio, na kumwambia mumewe, akisema, Tazama, huyo mtu amenitokea, huyo aliyenijilia siku ile.

Waamuzi 13:11 Judges 13:11

Basi Manoa akainuka, akamwandama mkewe, na kumfikilia mtu huyo, akamwuliza, Je! Wewe ndiwe mtu yule aliyenena na huyu mwanamke? Akasema, Naam, ni mimi.

Waamuzi 13:12 Judges 13:12

Manoa akasema, Basi sasa hayo maneno yako yatakapotimia, je! Huyo mtoto atakuwa wa namna gani, na kazi yake itakuwa ni nini?

Waamuzi 13:13 Judges 13:13

Malaika wa Mungu akamwambia Manoa, Katika hayo yote niliyomwambia huyo mwanamke na ajihadhari.

Waamuzi 13:14 Judges 13:14

Asile kitu cho chote kitokacho katika mzabibu, wala asinywe divai, wala mvinyo, wala asile kitu cho chote kilicho najisi; hayo yote niliyomwamuru na ayatunze.

Waamuzi 13:15 Judges 13:15

Kisha Manoa akamwambia huyo malaika wa Bwana, Nakuomba, tukuzuie, ili tupate kuandaa mwana-mbuzi kwa ajili yako.

Waamuzi 13:16 Judges 13:16

Lakini malaika wa Bwana akamwambia Manoa, Ujapokuwa wanizuia, sitakula katika mkate wako; na kwamba wataka kufanya tayari sadaka ya kuteketezwa, inakupasa kumsongezea Bwana. Kwa kuwa Manoa hakujua ya kwamba yeye ni malaika wa Bwana.

Waamuzi 13:17 Judges 13:17

Manoa akamwambia huyo malaika wa Bwana, Jina lako ni nani, ili kwamba hapo hayo maneno yako yatakapotimia nipate kukutukuza?

Waamuzi 13:18 Judges 13:18

Huyo malaika wa Bwana akamwambia, Kwani wewe kuniuliza jina langu, kwa kuwa jina hilo ni la ajabu?

Waamuzi 13:19 Judges 13:19

Basi Manoa akamtwaa yule mwana-mbuzi, pamoja na sadaka ya unga, akamtolea Bwana hapo juu ya mwamba; huyo malaika akatenda la ajabu; Manoa na mkewe wakaangalia.

Waamuzi 13:20 Judges 13:20

Kwa maana, ikawa, mara huo mwali wa moto ulipopaa juu mbinguni kutoka pale madhabahuni, huyo malaika wa Bwana akapaa katika mwali wa moto wa madhabahu; nao Manoa na mkewe wakaangalia; wakainama kifudifudi.

Waamuzi 13:21 Judges 13:21

Lakini malaika wa Bwana hakumtokea Manoa tena, wala mkewe. Ndipo Manoa alipojua ya kwamba ndiye malaika wa Bwana.

Waamuzi 13:22 Judges 13:22

Manoa akamwambia mkewe, Hakika yetu tutakufa sisi, kwa sababu tumemwona Mungu.

Waamuzi 13:23 Judges 13:23

Lakini mkewe akamwambia, Kama Bwana angetaka kutuua hangepokea sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya unga, mikononi mwetu, wala hangetuonyesha mambo hayo yote, wala hangetuambia mambo kama hayo wakati huu.

Waamuzi 13:24 Judges 13:24

Basi yule mwanamke akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, Bwana akambarikia.

Waamuzi 13:25 Judges 13:25

Roho ya Bwana ikaanza kumtaharakisha katika Mahane-dani, katikati ya Sora na Eshtaoli.