Hesabu Mlango 25 Numbers

Hesabu 25:1 Numbers 25:1

Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu;

Hesabu 25:2 Numbers 25:2

kwa kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu yao.

Hesabu 25:3 Numbers 25:3

Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori; hasira za Bwana zikawaka juu ya Israeli.

Hesabu 25:4 Numbers 25:4

Kisha Bwana akamwambia Musa, Watwae wakuu wote wa hao watu, ukamtungikie Bwana watu hao mbele ya jua, ili kwamba hizo hasira kali za Bwana ziwaondokee Israeli.

Hesabu 25:5 Numbers 25:5

Basi Musa akawaambia waamuzi wa Israeli, Waueni kila mtu watu wake waliojiungamanisha na Baal-peori.

Hesabu 25:6 Numbers 25:6

Na tazama, mtu mmoja miongoni mwa wana wa Israeli akaja na kuwaletea nduguze mwanamke Mmidiani mbele ya macho ya Musa, na mbele ya macho ya mkutano wote wa wana wa Israeli, hapo walipokuwa walia mbele ya mlango wa hema ya kukutania.

Hesabu 25:7 Numbers 25:7

Naye Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, alipoona jambo hilo, akaondoka hapo katikati ya mkutano, akashika fumo mkononi mwake;

Hesabu 25:8 Numbers 25:8

akamwandama huyo mtu wa Israeli na kuingia ndani ya hema nyuma yake, naye akawachoma wote wawili kwa fumo lake, yule mume wa Israeli na huyo mwanamke kati ya tumbo lake. Basi pigo likazuiwa kwao wana wa Israeli.

Hesabu 25:9 Numbers 25:9

Nao waliokufa kwa hilo pigo walikuwa watu elfu ishirini na nne hesabu yao.

Hesabu 25:10 Numbers 25:10

Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia,

Hesabu 25:11 Numbers 25:11

Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, amezigeuza hasira zangu zisiwe juu ya wana Wa Israeli, kwa kuwa alikuwa na wivu kati yao kwa wivu wangu mimi, hata nisiwaangamize wana wa Israeli katika wivu wangu.

Hesabu 25:12 Numbers 25:12

Basi kwa hiyo, sema, Tazama, nampa yeye agano langu la amani;

Hesabu 25:13 Numbers 25:13

tena kwake yeye, na kizazi chake baada yake, litakuwa agano la ukuhani wa milele; kwa sababu alikuwa na wivu kwa ajili ya Mungu wake, na kuwafanyia upatanisho wana wa Israeli.

Hesabu 25:14 Numbers 25:14

Basi jina la Mwisraeli huyo aliyeuawa pamoja na yule mwanamke Mmidiani, aliitwa Zimri, mwana wa Salu, mkuu wa nyumba ya baba zake, katika kabila la Simeoni.

Hesabu 25:15 Numbers 25:15

Na jina la huyo mwanamke Mmidiani aliyeuawa, aliitwa Kozbi, binti Suri; naye alikuwa kichwa cha watu wa nyumba ya baba zake huko Midiani

Hesabu 25:16 Numbers 25:16

Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,

Hesabu 25:17 Numbers 25:17

Wasumbue Wamidiani, na kuwapiga;

Hesabu 25:18 Numbers 25:18

kwa sababu wao wawasumbua ninyi kwa hila zao, ambazo kwa hizo wamewadanganya ninyi katika jambo la Peori, na katika jambo la huyo Kozbi, binti wa mkuu wa Midiani, umbu lao, huyo aliyeuawa siku hiyo ya pigo katika jambo la Peori.