Danieli Mlango 12 Daniel

Danieli 12:1 Daniel 12:1

Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo; na wakati huo watu wako wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile.

Danieli 12:2 Daniel 12:2

Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele.

Danieli 12:3 Daniel 12:3

Na walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele.

Danieli 12:4 Daniel 12:4

Lakini wewe, Ee Danielii, yafunge maneno haya, ukakitie muhuri kitabu, hata wakati wa mwisho; wengi wataenda mbio huko na huko, na maarifa yataongezeka.

Danieli 12:5 Daniel 12:5

Ndipo mimi, Danielii, nikatazama, na kumbe, wamesimama wengine wawili, mmoja ukingoni mwa mto upande huu, na mmoja ukingoni mwa mto upande wa pili.

Danieli 12:6 Daniel 12:6

Na mmoja akamwuliza yule mtu aliyevikwa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, Je! Itakuwa muda wa miaka mingapi hata mwisho wa mambo haya ya ajabu?

Danieli 12:7 Daniel 12:7

Nami nikamsikia yule mtu aliyevikwa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, hapo alipoinua mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto kuelekea mbinguni; akaapa kwa yeye aliye hai milele na milele, ya kwamba itakuwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati; tena watakapokuwa wamekwisha kuvunja nguvu za hao watu watakatifu, ndipo mambo hayo yote yatakapotimizwa.

Danieli 12:8 Daniel 12:8

Nami nikasikia, lakini sikuelewa; ndipo nikasema, Ee Bwana wangu, mwisho wa mambo haya utakuwaje?

Danieli 12:9 Daniel 12:9

Akasema, Enenda zako, Danielii; maana maneno haya yamefungwa, na kutiwa muhuri, hata wakati wa mwisho.

Danieli 12:10 Daniel 12:10

Wengi watajitakasa, na kujifanya weupe, na kusafika; bali wabaya watatenda mabaya; wala hataelewa mtu mbaya awaye yote; bali wao walio na hekima ndio watakaoelewa.

Danieli 12:11 Daniel 12:11

Na tangu wakati ule ambapo sadaka ya kuteketezwa ya daima itaondolewa, na hilo chukizo la uharibifu litakaposimamishwa, itapata siku elfu na mia mbili na tisini.

Danieli 12:12 Daniel 12:12

Heri angojaye, na kuzifikilia siku hizo elfu na mia tatu na thelathini na tano.

Danieli 12:13 Daniel 12:13

Lakini enenda zako hata utakapokuwa mwisho ule; maana wewe utastarehe, nawe utasimama katika kura yako mwisho wa siku hizo.