Danieli Mlango 11 Daniel

Danieli 11:1 Daniel 11:1

Tena mimi, katika mwaka wa kwanza wa Dario, Mmedi, mimi nalisimama nimthibitishe na kumtia nguvu.

Danieli 11:2 Daniel 11:2

Nami sasa nitakuonyesha yaliyo kweli. Tazama, watasimama wafalme watatu katika Uajemi; naye mfalme wa nne atakuwa tajiri kuliko hao wote; naye atakapopata nguvu kwa utajiri wake, atawachochea wote juu ya ufalme wa Uyunani.

Danieli 11:3 Daniel 11:3

Na mfalme hodari atasimama, atakayetawala kwa mamlaka kubwa, na kutenda apendavyo.

Danieli 11:4 Daniel 11:4

Naye atakaposimama, ufalme wake utavunjika, na kugawanyika katika pepo nne za mbinguni; lakini hautakuwa wa uzao wake, wala hautakuwa kama mamlaka yake ambayo alitawala kwayo; kwa maana ufalme wake utang'olewa, hata kwa ajili ya wengine zaidi ya hao.

Danieli 11:5 Daniel 11:5

Na mfalme wa kusini atakuwa hodari; na mmoja wa wakuu wake atakuwa hodari kuliko yeye, naye atakuwa na mamlaka; mamlaka yake itakuwa mamlaka kubwa.

Danieli 11:6 Daniel 11:6

Na baada ya miaka kadha wa kadha watashirikiana; kwa kuwa binti wa mfalme wa kusini atakuja kwa mfalme wa kaskazini, ili kufanya mapatano naye; lakini hatakuwa na nguvu za mkono wake sikuzote; wala mfalme yule hatasimama, wala mkono wake; lakini yule binti atatolewa, na hao waliomleta, na yeye aliyemzaa, na yeye aliyemtia nguvu, zamani zile.

Danieli 11:7 Daniel 11:7

Lakini katika chipukizi la mizizi yake atasimama mmoja mahali pake atakayeliendesha jeshi la askari, naye ataingia katika ngome ya mfalme wa kaskazini, na kuwatenda mambo, na kuwashinda;

Danieli 11:8 Daniel 11:8

na miungu yao, pamoja na sanamu zao, na vyombo vyao vizuri vya fedha na dhahabu atavichukua mpaka Misri; kisha atajizuia miaka kadha wa kadha asimwendee mfalme wa kaskazini.

Danieli 11:9 Daniel 11:9

Naye huyo ataingia katika ufalme wa mfalme wa kusini, lakini atarudi mpaka nchi yake mwenyewe.

Danieli 11:10 Daniel 11:10

Na wanawe watafanya vita, na kukusanya mkutano wa majeshi makuu; watakaokuja na kufurika na kupita katikati; nao watarudi na kufanya vita mpaka penye ngome yake.

Danieli 11:11 Daniel 11:11

Na mfalme wa kusini ataingiliwa na ghadhabu, naye atatoka na kupigana naye, yaani, na mfalme wa kaskazini; naye atapanga jeshi kubwa; na jeshi hilo litawekwa mikononi mwake.

Danieli 11:12 Daniel 11:12

Atakapokwisha kuchukua lile jeshi, moyo wake utatukuzwa; naye atawaangusha makumi elfu; lakini hataongezewa nguvu.

Danieli 11:13 Daniel 11:13

Kwa maana mfalme wa kaskazini atarudi, naye atapanga jeshi kubwa kuliko lile la kwanza; naye hakika atakuja mwisho wa zamani zile, yaani, baada ya miaka kadha wa kadha, pamoja na jeshi kubwa na mali nyingi.

Danieli 11:14 Daniel 11:14

Na zamani zile watu wengi watasimama ili kumpinga mfalme wa kusini; pia, wenye jeuri miongoni mwa watu wako watajiinua ili kuyathibitisha maono; lakini wataanguka.

Danieli 11:15 Daniel 11:15

Basi mfalme wa kaskazini atakuja, na kufanya kilima, na kuupiga mji wenye maboma; na silaha za kusini hazitaweza kumpinga, wala watu wake wateule, wala hapatakuwa na nguvu za kumpinga.

Danieli 11:16 Daniel 11:16

Maana ajaye kupigana naye atatenda kadiri apendavyo, wala hapana mtu atakayesimama mbele yake; naye atasimama katika nchi ya uzuri, na uharibifu utakuwa mkononi mwake.

Danieli 11:17 Daniel 11:17

Naye atakaza uso wake ili aje pamoja na nguvu zote za ufalme wake, naye atafanya mapatano naye; naye atatenda kadiri apendavyo; naye atampa binti wa watu ili amharibu; lakini hilo halitasimama wala kumfaa.

Danieli 11:18 Daniel 11:18

Baada ya hayo atauelekeza uso wake kwenye visiwa, naye atavipiga visiwa vingi; lakini mkuu mmoja ataikomesha aibu iliyoletwa na yeye; naam, aibu yake hiyo atamrudishia mwenyewe.

Danieli 11:19 Daniel 11:19

Ndipo atauelekeza uso wake kwenye ngome za nchi yake mwenyewe; lakini atajikwaa na kuanguka, wala hataonekana tena.

Danieli 11:20 Daniel 11:20

Ndipo badala yake atasimama mmoja, atakayepitisha mwenye kutoza ushuru kati ya utukufu wa ufalme wake; lakini katika muda wa siku chache ataangamizwa, si kwa hasira, wala si katika vita.

Danieli 11:21 Daniel 11:21

Kisha badala yake atasimama mmoja, mtu astahiliye kudharauliwa, ambaye hawakumpa heshima ya ufalme; naye atakuja wakati wa amani, naye ataupata ufalme kwa kujipendekeza.

Danieli 11:22 Daniel 11:22

Na wale wenye silaha mfano wa gharika watagharikishwa mbele yake, na kuvunjika, naam, mkuu wa maagano pia.

Danieli 11:23 Daniel 11:23

Na baada ya maagano atatenda kwa hila; maana atapanda, naye atakuwa hodari pamoja na watu wadogo.

Danieli 11:24 Daniel 11:24

Wakati wa amani atapaingia mahali palipofanikiwa sana pa wilaya hiyo; naye atatenda mambo ambayo baba zake hawakuyatenda, wala babu zake; atatawanya kati yao mawindo, na mateka, na mali; naam, atatunga hila zake juu ya ngome, hata wakati ulioamriwa.

Danieli 11:25 Daniel 11:25

Naye atachochea nguvu zake na ushujaa wake juu ya huyo mfalme wa kusini kwa jeshi kubwa; na mfalme wa kusini atafanya vita kwa jeshi kubwa mno lenye nguvu nyingi; lakini hatasimama; maana watatunga hila juu yake.

Danieli 11:26 Daniel 11:26

Naam, walao sehemu ya chakula chake watamwangamiza, na jeshi lake litagharikishwa; na wengi wataanguka wameuawa.

Danieli 11:27 Daniel 11:27

Na katika habari za wafalme hao wawili, mioyo yao watanuia kutenda madhara, nao watasema uongo walipo pamoja mezani; lakini hilo halitafanikiwa; maana mwisho utatokea wakati ulioamriwa.

Danieli 11:28 Daniel 11:28

Ndipo atakaporudi mpaka nchi yake mwenye utajiri mwingi; na moyo wake utakuwa kinyume cha hilo agano takatifu; naye atafanya kama apendavyo, na kurudi mpaka nchi yake.

Danieli 11:29 Daniel 11:29

Kwa wakati ulioamriwa atarudi, na kuingia upande wa kusini; lakini wakati wa mwisho mambo hayatakuwa kama yalivyokuwa wakati wa kwanza.

Danieli 11:30 Daniel 11:30

Maana merikebu za Kitimu zitakuja kupigana naye; basi atavunjika moyo, naye atarudi na kulighadhibikia hilo agano takatifu; na kutenda kadiri apendavyo; naam, atarudi, na kuwasikiliza walioacha hilo agano takatifu.

Danieli 11:31 Daniel 11:31

Na wenye silaha watasimama upande wake, nao watapatia unajisi mahali patakatifu, ndiyo ngome, nao wataondoa sadaka ya kuteketezwa ya kila siku, nao watalisimamisha chukizo la uharibifu.

Danieli 11:32 Daniel 11:32

Na wao wafanyao maovu juu ya hilo agano atawapotosha kwa maneno ya kujipendekeza; lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari, na kutenda mambo makuu.

Danieli 11:33 Daniel 11:33

Na hao walio wenye hekima katika watu watafundisha wengi; hata hivyo wataanguka kwa upanga, na kwa moto, na kwa kufungwa, na kwa kutekwa nyara, siku nyingi.

Danieli 11:34 Daniel 11:34

Basi watakapoanguka, watasaidiwa kwa msaada kidogo; lakini wengi wataambatana nao kwa maneno ya kujipendekeza.

Danieli 11:35 Daniel 11:35

Na baadhi yao wenye hekima wataanguka, ili kuwatakasa, na kuwasafisha, na kuwafanya weupe, hata wakati wa mwisho; kwa maana ni kwa wakati ulioamriwa, ambao haujaja.

Danieli 11:36 Daniel 11:36

Naye mfalme atafanya kama apendavyo; naye atajitukuza na kujiadhimisha juu ya kila mungu, naye atanena maneno ya ajabu juu ya Mungu wa miungu, naye atafanikiwa mpaka ghadhabu itakapotimia; maana yaliyokusudiwa yatafanyika.

Danieli 11:37 Daniel 11:37

Wala hataijali miungu ya baba zake; wala yeye aliyetamaniwa na wanawake; wala hatamjali mungu awaye yote; maana atajitukuza mwenyewe juu ya wote.

Danieli 11:38 Daniel 11:38

Lakini katika mahali pake atamheshimu mungu wa ngome; na mungu ambaye baba zake hawakumjua atamheshimu, kwa dhahabu, na fedha, na vito vya thamani, na vitu vipendezavyo.

Danieli 11:39 Daniel 11:39

Naye ataziteka nyara ngome zenye nguvu kwa msaada wa mungu mgeni; na yeye atakayemkubali atamwongeza kwa utukufu; naye atawapa kumiliki wengi; naye ataigawa nchi kwa rushwa,

Danieli 11:40 Daniel 11:40

na wakati wa mwisho mfalme wa kusini atashindana naye; na mfalme wa kaskazini atamshambulia kama upepo wa kisulisuli, pamoja na magari ya vita, na wapanda farasi, na merikebu nyingi; naye ataingia katika nchi hizo, na kufurika na kupita katikati.

Danieli 11:41 Daniel 11:41

Tena ataingia katika hiyo nchi ya uzuri, na nchi nyingi zitapinduliwa; lakini nchi hizi zitaokolewa na mkono wake, Edomu, na Moabu, na wakuu wa watu wa Amoni.

Danieli 11:42 Daniel 11:42

Naye ataunyosha mkono wake juu ya nchi hizo, hata na nchi ya Misri haitaokoka.

Danieli 11:43 Daniel 11:43

Lakini atakuwa na nguvu juu ya hazina za dhahabu na fedha, na juu ya vitu vyote vya Misri vyenye thamani; na Walibia na Wakushi watafuata nyayo zake.

Danieli 11:44 Daniel 11:44

Lakini habari zitokazo mashariki na kaskazini zitamfadhaisha; naye atatoka kwa ghadhabu nyingi, ili kuharibu, na kuwaondolea mbali watu wengi.

Danieli 11:45 Daniel 11:45

Naye ataweka hema zake za kifalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa uzuri; lakini ataifikilia ajali yake, wala hakuna atakayemsaidia.