Zekaria Mlango 10 Zechariah

Zekaria 10:1 Zechariah 10:1

Mwombeni Bwana mvua wakati wa masika, naam, Bwana afanyaye umeme, naye atawapa manyunyu ya mvua, kila mtu atapewa nyasi kondeni.

Zekaria 10:2 Zechariah 10:2

Kwa maana vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo; nao wameleta habari za ndoto za uongo, wafariji bure; kwa sababu hiyo waenda zao kama kondoo, wateswa, kwa sababu hapana mchungaji.

Zekaria 10:3 Zechariah 10:3

Hasira yangu imewaka juu ya wachungaji, nami nitawaadhibu mbuzi waume; kwa maana Bwana wa majeshi ameliangalia kundi lake, yaani, nyumba ya Yuda, naye atawafanya kuwa kama farasi wake mzuri vitani.

Zekaria 10:4 Zechariah 10:4

Kwake yeye litatoka lile jiwe la pembeni, kwake yeye utatoka msumari, kwake yeye utatoka upinde wa vita, kwake yeye atatoka kila mtawala pamoja.

Zekaria 10:5 Zechariah 10:5

Nao watakuwa kama mashujaa, wakanyagao adui zao katika matope ya njia vitani; nao watapiga vita, kwa sababu Bwana yu pamoja nao; na hao wapandao farasi watafadhaishwa.

Zekaria 10:6 Zechariah 10:6

Nami nitaitia nguvu nyumba ya Yuda, nami nitaiokoa nyumba ya Yusufu, nami nitawarudisha, kwa maana nawaonea rehema; nao watakuwa kana kwamba sikuwatupa; kwa maana mimi ni Bwana, Mungu wao, nami nitawasikia.

Zekaria 10:7 Zechariah 10:7

Na watu wa Efraimu watakuwa kama shujaa, na moyo wao utafurahi kana kwamba ni kwa divai; naam, watoto wao wataona mambo haya, na kufurahi; mioyo yao itamfurahia Bwana.

Zekaria 10:8 Zechariah 10:8

Nitawapigia kelele, na kuwakusanya pamoja; kwa maana nimewakomboa; nao wataongezeka kama walivyoongezeka.

Zekaria 10:9 Zechariah 10:9

Nami nitawapanda kama mbegu kati ya mataifa; nao watanikumbuka katika nchi zilizo mbali; nao watakaa pamoja na watoto wao; tena watarudi.

Zekaria 10:10 Zechariah 10:10

Tena nitawarudisha toka nchi ya Misri, nitawakusanya na kuwatoa katika Ashuru; nami nitawaingiza katika nchi ya Gileadi na Lebanoni; ila nafasi ya kuwatosha haitaonekana.

Zekaria 10:11 Zechariah 10:11

Naye atapita kati ya bahari ya mateso, na kuyapiga mawimbi ya bahari, na vilindi vyote vya mto wa Nile vitakauka; na kiburi cha Ashuru kitashushwa; na fimbo ya enzi ya Misri itatoweka.

Zekaria 10:12 Zechariah 10:12

Nami nitawatia nguvu katika Bwana; nao watatembea huko na huko katika jina lake, asema Bwana.