Zekaria Mlango 9 Zechariah

Zekaria 9:1 Zechariah 9:1

Ufunuo wa neno la Bwana, lililosemwa juu ya nchi ya Hadraki, na Dameski itakuwa mahali pake pa kustarehe; kwa maana jicho la mwanadamu na la kabila zote za Israeli linamwelekea Bwana;

Zekaria 9:2 Zechariah 9:2

na Hamathi pia iliyo mpakani mwake; na Tiro, na Sidoni, kwa maana ana akili nyingi.

Zekaria 9:3 Zechariah 9:3

Na Tiro alijijengea ngome, akakusanya fedha kama mchanga, dhahabu safi kama matope ya njia kuu.

Zekaria 9:4 Zechariah 9:4

Tazama, Bwana atamwondolea mali zake, naye ataupiga uwezo wake alio nao baharini, naye mwenyewe atateketezwa kwa moto.

Zekaria 9:5 Zechariah 9:5

Ashkeloni ataona haya na kuogopa; Gaza pia, naye atafadhaika sana; na Ekroni, kwa maana taraja lake litatahayarika; na mfalme ataangamia toka Gaza, na Ashkeloni atakuwa hana watu.

Zekaria 9:6 Zechariah 9:6

Na mwana wa haramu atatawala huko Ashdodi, nami nitakatilia mbali kiburi cha Wafilisti.

Zekaria 9:7 Zechariah 9:7

Nami nitaondoa damu yake kinywani mwake, na machukizo yake nitayatoa katika meno yake; yeye naye atakuwa ni mabaki kwa Mungu wetu; naye atakuwa kama mtu mkuu katika Yuda, na Ekroni kama Myebusi.

Zekaria 9:8 Zechariah 9:8

Nami nitapiga kambi yangu pande zote za nyumba yangu ili kuwapinga adui, mtu awaye yote asipite ndani yake wala kurudi; wala mtu aoneaye hatapita tena kati yao; kwa maana sasa nimeona kwa macho yangu.

Zekaria 9:9 Zechariah 9:9

Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda.

Zekaria 9:10 Zechariah 9:10

Na gari la vita nitaliondoa liwe mbali na Efraimu, na farasi awe mbali na Yerusalemu, na upinde wa vita utaondolewa mbali; naye atawahubiri mataifa yote habari za amani; na mamlaka yake yatakuwa toka bahari hata bahari, na toka Mto hata miisho ya dunia.

Zekaria 9:11 Zechariah 9:11

Na kwa habari zako wewe, kwa sababu ya damu ya agano lako, nimewatoa wafungwa wako katika shimo lile lisilo na maji.

Zekaria 9:12 Zechariah 9:12

Irudieni ngome, enyi wafungwa wa tumaini; hata hivi leo nasema ya kwamba nitakurudishia maradufu.

Zekaria 9:13 Zechariah 9:13

Maana nimejipindia Yuda, nimeujaza upinde wangu Efraimu; nami nitawaondokesha wana wako, Ee Sayuni, wapigane na wana wako, Ee Uyunani, nami nitakufanya wewe kuwa kama upanga wa shujaa.

Zekaria 9:14 Zechariah 9:14

Naye Bwana ataonekana juu yao, Na mshale wake utatoka kama umeme; Na Bwana MUNGU ataipiga tarumbeta, Naye atakwenda kwa pepo za kisulisuli za kusini.

Zekaria 9:15 Zechariah 9:15

Bwana wa majeshi atawalinda; Nao watakula na kuyakanyaga mawe ya teo; Nao watakunywa na kufanya kelele kama kwa divai; Nao watajazwa kama mabakuli, kama pembe za madhabahu.

Zekaria 9:16 Zechariah 9:16

Na Bwana, Mungu wao, atawaokoa siku hiyo, Kama kundi la watu wake; Kwa maana watakuwa kama vito vya taji, Vikimeta-meta juu ya nchi yake.

Zekaria 9:17 Zechariah 9:17

Maana wema wake, jinsi ulivyo mwingi! Na uzuri wake, jinsi ulivyo mwingi! Nafaka itawasitawisha vijana wanaume, Na divai mpya vijana wanawake.