Yoshua Mlango 24 Joshua

Yoshua 24:1 Joshua 24:1

Yoshua akawakusanya kabila zote za Israeli huko Shekemu, akawaita wazee wa Israeli, na wakuu wao, na waamuzi wao, na maakida wao nao wakahudhuria mbele za Mungu.

Yoshua 24:2 Joshua 24:2

Yoshua akawaambia watu wote, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Baba zenu hapo zamani walikaa ng'ambo ya Mto, maana Tera, baba yake Ibrahimu, naye ni baba yake Nahori; wakaitumikia miungu mingine.

Yoshua 24:3 Joshua 24:3

Nami nikamtwaa Ibrahimu baba yenu toka ng'ambo ya Mto, nikamwongoza katika nchi yote ya Kanaani; nikaongeza uzao wake, nikampa Isaka.

Yoshua 24:4 Joshua 24:4

Kisha nikampa huyo Isaka, Yakobo na Esau; nami nikampa Esau mlima Seiri aumiliki; Yakobo na watoto wake wakashuka Misri.

Yoshua 24:5 Joshua 24:5

Kisha nikawatuma Musa na Haruni nikaipiga nchi ya Misri, kwa hayo yote niliyoyatenda kati yake; hatimaye nikawatoa ninyi.

Yoshua 24:6 Joshua 24:6

Nikawatoa baba zenu watoke Misri; nanyi mkaifikilia bahari; Wamisri wakawafuatia baba zenu kwa magari na wapanda farasi mpaka bahari ya Shamu.

Yoshua 24:7 Joshua 24:7

Nao walipomlilia Bwana, akaweka giza kati ya ninyi na Wamisri, akaileta bahari juu yao, akawafunikiza; nayo macho yenu yaliyaona mambo niliyoyatenda huko Misri; kisha mkakaa jangwani siku nyingi.

Yoshua 24:8 Joshua 24:8

Kisha nikawaleta na kuwaingiza katika nchi ya Waamori waliokaa ng'ambo ya pili ya Yordani; nao wakapigana nanyi; nikawatia mikononi mwenu, mkaimiliki nchi yao; nami nikawaangamiza mbele yenu.

Yoshua 24:9 Joshua 24:9

Ndipo Balaki, mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, akainuka, akapigana na Israeli; tena akatuma watu akamwita Balaamu, mwana wa Beori, aje awalaani;

Yoshua 24:10 Joshua 24:10

lakini sikukubali kumsikiliza Balaamu; kwa hiyo akafuliza kuwabarikia ninyi; basi nikawatoa katika mkono wake.

Yoshua 24:11 Joshua 24:11

Nanyi mliuvuka Yordani, mkafika Yeriko; nao watu wa Yeriko wakapigana nanyi, Mwamori, na Mperizi, na Mkanaani, na Mhiti, na Mgirgashi, na Mhivi, na Myebusi; nami nikawatia mikononi mwenu.

Yoshua 24:12 Joshua 24:12

Nikatuma mavu mbele yenu, waliowafukuza mbele yenu hao wafalme wawili wa Waamori, si kwa upanga wako, wala kwa upinde wako.

Yoshua 24:13 Joshua 24:13

Nami nimewapa ninyi nchi msiyoitendea kazi, na miji msiyoijenga, nanyi mmekaa humo; mnakula matunda ya mashamba ya mizabibu na mizeituni msiyoipanda.

Yoshua 24:14 Joshua 24:14

Basi sasa mcheni Bwana, mkamtumikie kwa unyofu wa moyo na kwa kweli; na kuiweka mbali miungu ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, na huko Misri; mkamtumikie yeye Bwana.

Yoshua 24:15 Joshua 24:15

Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana.

Yoshua 24:16 Joshua 24:16

Hao watu wakajibu wakasema, Hasha! Tusimwache Bwana, ili kuitumikia miungu mingine;

Yoshua 24:17 Joshua 24:17

kwa maana Bwana, Mungu wetu, yeye ndiye aliyetupandisha sisi na baba zetu kutoka nchi ya Misri; kutoka nyumba ya utumwa; naye ndiye aliyezifanya ishara zile kubwa mbele ya macho yetu, na kutulinda katika njia ile yote tuliyoiendea, na kati ya watu wa mataifa yote tuliopita katikati yao.

Yoshua 24:18 Joshua 24:18

Bwana ndiye aliyewafukuza watu wa mataifa yote watoke mbele yetu, naam, Waamori waliokaa katika nchi hii; basi, kwa sababu hiyo sisi nasi tutamtumikia Bwana, maana yeye ndiye Mungu wetu.

Yoshua 24:19 Joshua 24:19

Yoshua akawaambia watu, Hamwezi kumtumikia Bwana; kwa kuwa yeye ni Mungu mtakatifu; yeye ni Mungu mwenye wivu; hatawasamehe makosa yenu, wala dhambi zenu.

Yoshua 24:20 Joshua 24:20

Kama mkimwacha Bwana na kuitumikia miungu migeni, ndipo atageuka na kuwatenda mabaya na kuwaangamiza, baada ya kuwatendea mema.

Yoshua 24:21 Joshua 24:21

Lakini hao watu wakamwambia Yoshua, La! Lakini tutamtumikia Bwana.

Yoshua 24:22 Joshua 24:22

Yoshua akawaambia watu, Ninyi mmekuwa mashahidi juu ya nafsi zenu, ya kuwa mmemchagua Bwana, ili kumtumikia yeye. Wakasema, Sisi tu mashahidi.

Yoshua 24:23 Joshua 24:23

Akasema, Basi sasa, iondoeni miungu migeni iliyo kati yenu, mkaielekeze mioyo yenu kwa Bwana, Mungu wa Israeli.

Yoshua 24:24 Joshua 24:24

Ndipo hao watu wakamwambia Yoshua, Bwana, Mungu wetu, ndiye tutakayemtumikia; na sauti yake ndiyo tutakayoitii.

Yoshua 24:25 Joshua 24:25

Basi Yoshua akafanya agano na wale watu siku ile, akawapa amri na agizo huko Shekemu.

Yoshua 24:26 Joshua 24:26

Yoshua akayaandika maneno haya katika kitabu cha torati ya Mungu; kisha akatwaa jiwe kubwa, akalisimamisha huko, chini ya ule mwaloni uliokuwa karibu na patakatifu pa Bwana.

Yoshua 24:27 Joshua 24:27

Yoshua akawaambia watu wote, Tazama, jiwe hili litakuwa shahidi juu yetu; kwa maana limesikia maneno yote ya Bwana aliyotuambia, basi litakuwa shahidi juu yenu, msije mkamkana Mungu wenu.

Yoshua 24:28 Joshua 24:28

Basi Yoshua akawaruhusu watu, wakaenda zao, kila mtu kwenye urithi wake.

Yoshua 24:29 Joshua 24:29

Ikawa, baada ya hayo, Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana, akafa, mwenye umri wa miaka mia na kumi.

Yoshua 24:30 Joshua 24:30

Wakamzika katika mpaka wa urithi wake, huko Timnath-sera; ulio katika nchi ya vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi.

Yoshua 24:31 Joshua 24:31

Nao Israeli wakamtumikia Bwana siku zote za Yoshua, na siku zote za hao wazee walioishi baada ya kufa kwake Yoshua, hao walioijua kazi yote ya Bwana, aliyowatendea Israeli.

Yoshua 24:32 Joshua 24:32

Na hiyo mifupa ya Yusufu, ambayo wana wa Israeli walikuwa wameileta kutoka Misri, wakaizika huko Shekemu katika ile sehemu ya nchi, Yakobo aliyoinunua kwa wana wa Hamori, babaye Shekemu, kwa vipande mia vya fedha; nayo ikawa ni urithi wa wana wa Yusufu.

Yoshua 24:33 Joshua 24:33

Huyo Eleazari mwana wa Haruni naye akafa; wakamzika katika kilima cha Finehasi mwanawe, ambacho alipewa yeye katika nchi ya vilima ya Efraimu.