2 Timotheo Mlango 2 2nd Timothy

2 Timotheo 2:1 2ndTimothy 2:1

Basi wewe, mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo katika Kristo Yesu.

2 Timotheo 2:2 2ndTimothy 2:2

Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.

2 Timotheo 2:3 2ndTimothy 2:3

Ushiriki taabu pamoja nami, kama askari mwema wa Kristo Yesu.

2 Timotheo 2:4 2ndTimothy 2:4

Hakuna apigaye vita ajitiaye katika shughuli za dunia, ili ampendeze yeye aliyemwandika awe askari.

2 Timotheo 2:5 2ndTimothy 2:5

Hata mtu akishindana katika machezo hapewi taji, asiposhindana kwa halali.

2 Timotheo 2:6 2ndTimothy 2:6

Yampasa mkulima mwenye taabu ya kazi kuwa wa kwanza wa kupata fungu la matunda.

2 Timotheo 2:7 2ndTimothy 2:7

Yafahamu sana hayo nisemayo, kwa maana Bwana atakupa akili katika mambo yote.

2 Timotheo 2:8 2ndTimothy 2:8

Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu.

2 Timotheo 2:9 2ndTimothy 2:9

Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi.

2 Timotheo 2:10 2ndTimothy 2:10

Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.

2 Timotheo 2:11 2ndTimothy 2:11

Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia;

2 Timotheo 2:12 2ndTimothy 2:12

Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi;

2 Timotheo 2:13 2ndTimothy 2:13

Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.

2 Timotheo 2:14 2ndTimothy 2:14

Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao.

2 Timotheo 2:15 2ndTimothy 2:15

Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.

2 Timotheo 2:16 2ndTimothy 2:16

Jiepushe na maneno yasiyo na maana, ambayo si ya dini; kwa kuwa wataendelea zaidi katika maovu,

2 Timotheo 2:17 2ndTimothy 2:17

na neno lao litaenea kama donda-ndugu. Miongoni mwa hao wamo Himenayo na Fileto,

2 Timotheo 2:18 2ndTimothy 2:18

walioikosa ile kweli, wakisema ya kwamba kiyama imekwisha kuwapo, hata kuipindua imani ya watu kadha wa kadha.

2 Timotheo 2:19 2ndTimothy 2:19

Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu.

2 Timotheo 2:20 2ndTimothy 2:20

Basi katika nyumba kubwa havimo vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali na vya mti, na vya udongo; vingine vina heshima, vingine havina.

2 Timotheo 2:21 2ndTimothy 2:21

Basi ikiwa mtu amejitakasa kwa kujitenga na hao, atakuwa chombo cha kupata heshima, kilichosafishwa, kimfaacho Bwana, kimetengenezwa kwa kila kazi iliyo njema.

2 Timotheo 2:22 2ndTimothy 2:22

Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi.

2 Timotheo 2:23 2ndTimothy 2:23

Walakini uyakatae maswali ya upumbavu yasiyo na elimu, ukijua ya kuwa huzaa magomvi.

2 Timotheo 2:24 2ndTimothy 2:24

Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu;

2 Timotheo 2:25 2ndTimothy 2:25

akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli;

2 Timotheo 2:26 2ndTimothy 2:26

wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.