2 Wafalme Mlango 14 2nd Kings

2 Wafalme 14:1 2ndKings 14:1

Katika mwaka wa pili wa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala.

2 Wafalme 14:2 2ndKings 14:2

Naye alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na kenda katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu.

2 Wafalme 14:3 2ndKings 14:3

Akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana, ila si kama babaye Daudi; akafanya kama yote aliyoyafanya baba yake Yoashi.

2 Wafalme 14:4 2ndKings 14:4

Walakini mahali pa juu hapakuondolewa; watu wakaendelea kutoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu.

2 Wafalme 14:5 2ndKings 14:5

Ikawa, mara ufalme ulipokuwa imara mkononi mwake, aliwaua watumishi wale waliomwua mfalme baba yake;

2 Wafalme 14:6 2ndKings 14:6

ila hakuwaua watoto wa hao wauaji; kama ilivyoandikwa katika kitabu cha torati ya Musa, kama alivyoamuru Bwana, akisema, Mababa wasife kwa makosa ya wana, wala wana wasife kwa makosa ya mababa; lakini kila mtu atakufa kwa kosa lake mwenyewe.

2 Wafalme 14:7 2ndKings 14:7

Akawaua Waedomi katika Bonde la Chumvi watu elfu kumi; akautwaa Sela vitani, akauita jina lake Yoktheeli hata leo.

2 Wafalme 14:8 2ndKings 14:8

Ndipo Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, akisema, Njoo, tutazamane uso kwa uso.

2 Wafalme 14:9 2ndKings 14:9

Naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatuma kwa Amazia mfalme wa Yuda, akisema, Mbaruti uliokuwako Lebanoni ulituma kwa mwerezi uliokuwako Lebanoni, kusema, Umwoze mwanangu binti yako; kukapita hayawani aliyekuwako Lebanoni, akaukanyaga ule mbaruti.

2 Wafalme 14:10 2ndKings 14:10

Kweli umepiga Edomu, na moyo wako umekutukuza; ujisifu basi, ukae nyumbani mwako. Mbona unataka kujitia bure katika madhara, hata uanguke, wewe na Yuda pamoja nawe?

2 Wafalme 14:11 2ndKings 14:11

Lakini Amazia hakutaka kusikia. Basi Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea; wakatazamana uso kwa uso, yeye na Amazia mfalme wa Yuda, huko Beth-shemeshi ulio wa Yuda.

2 Wafalme 14:12 2ndKings 14:12

Yuda wakashindwa mbele ya Israeli; wakakimbia kila mtu hemani kwake.

2 Wafalme 14:13 2ndKings 14:13

Yehoashi mfalme wa Israeli akamtwaa Amazia mfalme wa Yuda, mwanawe Yoashi mwana wa Ahazia, huko Beth-shemeshi, akaja Yerusalemu, akauvunja ukuta wa Yerusalemu toka lango la Efraimu hata lango la pembeni, mikono mia nne.

2 Wafalme 14:14 2ndKings 14:14

Akaitwaa dhahabu yote na fedha, na vyombo vyote vilivyoonekana katika nyumba ya Bwana, na katika hazina za nyumba ya mfalme, tena watu, kuwa amana; akarudi Samaria.

2 Wafalme 14:15 2ndKings 14:15

Basi mambo yote ya Yehoashi yaliyosalia, aliyoyafanya, na ushujaa wake, na jinsi alivyopigana na Amazia mfalme wa Yuda, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?

2 Wafalme 14:16 2ndKings 14:16

Yehoashi akalala na baba zake, akazikwa katika Samaria pamoja na wafalme wa Israeli; na Yeroboamu mwanawe akatawala mahali pake.

2 Wafalme 14:17 2ndKings 14:17

Naye Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda akaishi baada ya kufa kwake Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli miaka kumi na mitano.

2 Wafalme 14:18 2ndKings 14:18

Basi mambo yote ya Amazia yaliyosalia, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?

2 Wafalme 14:19 2ndKings 14:19

Wakafanya fitina juu yake katika Yerusalemu, naye akakimbia mpaka Lakishi, lakini wakatuma watu kumfuata mpaka Lakishi, wakamwua huko.

2 Wafalme 14:20 2ndKings 14:20

Wakamleta juu ya farasi; naye akazikwa huko Yerusalemu pamoja na babaze katika mji wa Daudi.

2 Wafalme 14:21 2ndKings 14:21

Na watu wote wa Yuda wakamtwaa Uzia aliyekuwa mwenye umri wa miaka kumi na sita,wakamfanya awe mfalme mahali pa baba yake Amazia.

2 Wafalme 14:22 2ndKings 14:22

Huyo akajenga Elathi, akaurudisha kwa Yuda, baada ya kulala mfalme pamoja na babaze.

2 Wafalme 14:23 2ndKings 14:23

Katika mwaka wa kumi na tano wa Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda Yeroboamu mwana wa Yehoashi mfalme wa Israeli alianza kutawala katika Samaria; akatawala miaka arobaini na mmoja.

2 Wafalme 14:24 2ndKings 14:24

Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana; wala hakuyaacha makosa yote ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.

2 Wafalme 14:25 2ndKings 14:25

Yeye akaurudisha mpaka wa Israeli toka kuingia kwa Hamathi hata bahari ya Araba, sawasawa na neno la Bwana, Mungu wa Israeli, alilolinena kwa mkono wa mtumishi wake Yona mwana wa Amitai, nabii, aliyekuwa wa Gath-heferi.

2 Wafalme 14:26 2ndKings 14:26

Kwani Bwana akayaona mateso ya Israeli, kwamba yalikuwa machungu sana; maana hakukuwa na mfungwa wala asiyefungwa, wala msaidizi kwa ajili ya Israeli.

2 Wafalme 14:27 2ndKings 14:27

Wala Bwana hakusema ya kwamba atalifuta jina la Israeli litoke chini ya mbingu; lakini akawaokoa kwa mkono wa Yeroboamu mwana wa Yehoashi.

2 Wafalme 14:28 2ndKings 14:28

Basi mambo yote ya Yeroboamu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake, na jinsi aliyvopigana, akawapatia tena Israeli Dameski na Hamathi, iliyokuwa kwanza ya Yuda, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?

2 Wafalme 14:29 2ndKings 14:29

Yeroboamu akalala na babaze, yaani, na wafalme wa Israeli. Na Zekaria mwanawe akatawala mahali pake.