2 Wafalme Mlango 24 2nd Kings

2 Wafalme 24:1 2ndKings 24:1

Katika siku zake akakwea Nebukadreza, mfalme wa Babeli na Yehoyakimu akawa mtumishi wake muda wa miaka mitatu;kisha ,akageuka,akamwasi.

2 Wafalme 24:2 2ndKings 24:2

Naye Bwana akatuma juu yake vikosi vya Wakaldayo, na vikosi vya Washami, na vikosi vya Wamoabi, na vikosi vya wana wa Amoni, akawatuma juu ya Yuda ili kuiharibu, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa mkono wa watumishi wake manabii.

2 Wafalme 24:3 2ndKings 24:3

Hakika kwa amri ya Bwana mambo hayo yalimpata Yuda, ili waondoshwe kutoka machoni pake, kwa sababu ya dhambi zake Manase, kadiri ya yote aliyoyafanya;

2 Wafalme 24:4 2ndKings 24:4

tena kwa ajili ya damu zisizo na hatia alizozimwaga; kwani aliujaza Yerusalemu damu zisizo na hatia; wala Bwana hakukubali kusamehe.

2 Wafalme 24:5 2ndKings 24:5

Basi mambo yote ya Yehoyakimu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?

2 Wafalme 24:6 2ndKings 24:6

Yehoyakimu akalala na babaze; na mwanawe Yekonia akatawala mahali pake.

2 Wafalme 24:7 2ndKings 24:7

Basi mfalme wa Misri hakuja tena kutoka nchi yake; kwa kuwa mfalme wa Babeli alikuwa amemnyang'anya nchi, tangu kijito cha Misri mpaka mto wa Frati, yote aliyokuwa nayo mfalme wa Misri.

2 Wafalme 24:8 2ndKings 24:8

Yekonia alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani wa Yerusalemu.

2 Wafalme 24:9 2ndKings 24:9

Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, mfano wa yote aliyoyafanya baba yake.

2 Wafalme 24:10 2ndKings 24:10

Wakati ule watumishi wa Nebukadreza mfalme wa Babeli wakakwea kwenda Yerusalemu, na mji ukahusuriwa.

2 Wafalme 24:11 2ndKings 24:11

Na Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akaufikilia huo mji, hapo watumishi wake walipokuwa wakiuhusuru.

2 Wafalme 24:12 2ndKings 24:12

Na Yekonia, mfalme wa Yuda, akatoka akamwendea mfalme wa Babeli, yeye na mama yake, na watumishi wake, na wakuu wa watu wake, na maakida wake; mfalme wa Babeli akamchukua mateka katika mwaka wa nane wa kutawala kwake.

2 Wafalme 24:13 2ndKings 24:13

Akatoa huko hazina zote za nyumba ya Bwana, na hazina za nyumba ya mfalme, akavikata-kata vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Sulemani, mfalme wa Israeli, alivifanya katika hekalu la Bwana, kama Bwana alivyosema.

2 Wafalme 24:14 2ndKings 24:14

Akawachukua mateka watu wa Yerusalemu wote pia, na wakuu wote, na mashujaa wote, watu elfu kumi; na mafundi wote, na wafua chuma wote; hapana mtu aliyebaki, ila waliokuwa wanyonge wa watu wa nchi.

2 Wafalme 24:15 2ndKings 24:15

Akamchukua Yekonia mpaka Babeli; na mama yake mfalme, na wake zake mfalme, na maakida wake, na wakuu wa nchi, aliwachukua mateka toka Yerusalemu mpaka Babeli.

2 Wafalme 24:16 2ndKings 24:16

Na mashujaa wote, watu elfu saba, na mafundi na wafua chuma elfu moja, wote pia wenye nguvu, tayari kwa vita, hao wote mfalme wa Babeli aliwachukua mateka mpaka Babeli.

2 Wafalme 24:17 2ndKings 24:17

Mfalme wa Babeli akamtawaza Matania, ndugu ya baba yake, awe mfalme badala yake, akalibadili jina lake, akamwita Sedekia.

2 Wafalme 24:18 2ndKings 24:18

Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na mmoja katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Hamutali, binti Yeremia wa Libna.

2 Wafalme 24:19 2ndKings 24:19

Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, sawasawa na yote aliyoyafanya Yehoyakimu.

2 Wafalme 24:20 2ndKings 24:20

Maana kwa sababu ya hasira ya Bwana mambo hayo yalitokea katika Yerusalemu na katika Yuda, hata alipokuwa amewaondosha wasiwe mbele ya uso wake; naye Sedekia akamwasi mfalme wa Babeli.