2 Wafalme Mlango 13 2nd Kings

2 Wafalme 13:1 2ndKings 13:1

Katika mwaka wa ishirini na tatu wa Yoashi mwana wa Ahazia, mfalme wa Yuda, Yehoahazi mwana wa Yehu alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria; akatawala miaka kumi na saba.

2 Wafalme 13:2 2ndKings 13:2

Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, akayafuata makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; wala hakuyaacha.

2 Wafalme 13:3 2ndKings 13:3

Hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, akawatia mkononi mwa Hazaeli mfalme wa Shamu, na mkononi mwa Ben-hadadi mwana wa Hazaeli, siku zote.

2 Wafalme 13:4 2ndKings 13:4

Naye Yehoahazi akamsihi Bwana, Bwana akamsikiliza; kwa kuwa aliyaona mateso ya Israeli, jinsi mfalme wa Shamu alivyowatesa.

2 Wafalme 13:5 2ndKings 13:5

(Bwana akawapa Israeli mwokozi, nao wakatoka mikononi mwa Washami; wana wa Israeli wakakaa hemani mwao kama zamani za kwanza.

2 Wafalme 13:6 2ndKings 13:6

Lakini hawakuyaacha makosa ya nyumba ya Yeroboamu, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli, lakini wakaendelea katika hayo; nayo ile Ashera ikakaa vivyo katika Samaria).

2 Wafalme 13:7 2ndKings 13:7

Kwa kuwa hakumwachia Yehoahazi watu ila wapandao farasi hamsini, na magari kumi, na askari elfu kumi waendao kwa miguu; kwa kuwa mfalme wa Shamu aliwaharibu, akawaponda mfano wa mavumbi yaliyokanyagwa.

2 Wafalme 13:8 2ndKings 13:8

Basi mambo yote ya Yehoahazi yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?

2 Wafalme 13:9 2ndKings 13:9

Yehoahazi akalala na babaze; wakamzika katika Samaria. Na Yehoashi mwanawe akatawala mahali pake.

2 Wafalme 13:10 2ndKings 13:10

Katika mwaka wa thelathini na saba wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yehoashi mwana wa Yehoahazi alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria, akatawala miaka kumi na sita.

2 Wafalme 13:11 2ndKings 13:11

Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; lakini akaendelea katika hayo.

2 Wafalme 13:12 2ndKings 13:12

Basi mambo yote ya Yehoashi yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake aliopigania na Amazia mfalme wa Yuda, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?

2 Wafalme 13:13 2ndKings 13:13

Yehoashi akalala na babaze; na Yeroboamu akakaa katika kiti chake cha enzi; naye Yehoashi akazikwa huko Samaria, pamoja na wafalme wa Israeli.

2 Wafalme 13:14 2ndKings 13:14

Basi Elisha alikuwa ameshikwa na ugonjwa wake uliomwua; naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatelemka amtazame, akamlilia mbele yake, akasema, Baba yangu! Baba yangu! Gari la Israeli na wapanda farasi wake!

2 Wafalme 13:15 2ndKings 13:15

Elisha akamwambia, Twaa uta na mishale; naye akatwaa uta na mishale.

2 Wafalme 13:16 2ndKings 13:16

Akamwambia mfalme wa Israeli, Weka mkono wako katika uta; naye akaweka mkono wake juu yake. Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme.

2 Wafalme 13:17 2ndKings 13:17

Akasema, Lifungue dirisha linaloelekea mashariki; akalifungua. Basi Elisha akasema, Piga; akapiga. Akasema, Mshale wa Bwana wa kushinda, naam, mshale wa kushinda Shamu, kwa maana utawapiga Washami katika Afeki hata utakapowaangamiza.

2 Wafalme 13:18 2ndKings 13:18

Akasema, Itwae mishale; akaitwaa. Akamwambia mfalme wa Israeli, Piga chini; akaipiga nchi mara tatu, akaacha.

2 Wafalme 13:19 2ndKings 13:19

Yule mtu wa Mungu akamkasirikia, akasema, Ingalikupasa kupiga mara tano au mara sita; ndipo ungaliipiga Shamu hata kuiangamiza; bali sasa utaipiga Shamu mara tatu tu.

2 Wafalme 13:20 2ndKings 13:20

Elisha akafa, nao wakamzika. Basi vikosi vya Wamoabi wakaingia katika nchi mwanzo wa mwaka.

2 Wafalme 13:21 2ndKings 13:21

Ikawa, walipokuwa wakimzika mtu, angalia, waliona kikosi; wakamtupa yule mtu kaburini mwa Elisha; mara yule maiti alipoigusa mifupa ya Elisha, alifufuka, akasimama kwa miguu.

2 Wafalme 13:22 2ndKings 13:22

Na Hazaeli mfalme wa Shamu akawaonea Israeli siku zote za Yehoahazi.

2 Wafalme 13:23 2ndKings 13:23

Lakini Bwana akawahurumia, akawasikitikia, na kuwaangalia, kwa ajili ya agano lake na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, wala hakutaka kuwaangamiza, wala hakuwatupa usoni pake bado.

2 Wafalme 13:24 2ndKings 13:24

Akafa Hazaeli mfalme wa Shamu, na Ben-hadadi mwanawe akatawala mahali pake.

2 Wafalme 13:25 2ndKings 13:25

Naye Yehoashi, mwana wa Yehoahazi, akaitwaa tena mkononi mwa Ben-hadadi mwana wa Hazaeli miji ile aliyoitwaa yeye mkononi mwa Yehoahazi baba yake vitani. Mara tatu Yehoashi akamshinda, akairudisha miji ya Israeli.