2 Wafalme Mlango 4 2nd Kings

2 Wafalme 4:1 2ndKings 4:1

Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha Bwana; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa.

2 Wafalme 4:2 2ndKings 4:2

Elisha akamwambia, Nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta.

2 Wafalme 4:3 2ndKings 4:3

Akasema, Nenda, ukatake vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usitake vichache.

2 Wafalme 4:4 2ndKings 4:4

Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge.

2 Wafalme 4:5 2ndKings 4:5

Basi akamwacha, akajifungia mlango yeye na wanawe; hao wakamletea vile vyombo, na yeye akamimina.

2 Wafalme 4:6 2ndKings 4:6

Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe, Niletee tena chombo. Akamwambia, Hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma.

2 Wafalme 4:7 2ndKings 4:7

Ndipo akaja akamwambia yule mtu wa Mungu. Naye akasema, Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako.

2 Wafalme 4:8 2ndKings 4:8

Hata ikawa siku moja, Elisha alikwenda Shunemu; na huko kulikuwa na mwanamke mmoja mwenye cheo; naye akamshurutisha aje ale chakula. Ikawa kila alipopita njia ile, huingia kula chakula.

2 Wafalme 4:9 2ndKings 4:9

Yule mwanamke akamwambia mumewe, Tazama, mimi naona ya kuwa mtu huyu apitaye kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa Mungu.

2 Wafalme 4:10 2ndKings 4:10

Nakuomba, tumfanyie chumba kidogo ukutani; na ndani yake tumwekee kitanda, na meza, na kiti, na kinara cha taa; na itakuwa, atujiapo, ataingia humo.

2 Wafalme 4:11 2ndKings 4:11

Ikawa siku moja akafika huko, akaingia katika chumba kile akalala.

2 Wafalme 4:12 2ndKings 4:12

Akamwambia Gehazi mtumishi wake, Mwite yule Mshunami. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mbele yake.

2 Wafalme 4:13 2ndKings 4:13

Akamwambia, Sema naye sasa, Tazama, wewe umetutunza sana namna hii; utendewe nini basi? Je! Uombewe neno kwa mfalme, au kwa amiri wa jeshi? Yule mwanamke akamjibu, Mimi ninakaa katika watu wangu mwenyewe.

2 Wafalme 4:14 2ndKings 4:14

Akasema, Basi, atendewe nini? Gehazi akajibu, Hakika hana mwana, na mumewe ni mzee.

2 Wafalme 4:15 2ndKings 4:15

Akamwambia, Kamwite. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mlangoni.

2 Wafalme 4:16 2ndKings 4:16

Akasema, Panapo wakati huu mwakani, utamkumbatia mwana. Akasema, La! Bwana wangu, wewe mtu wa Mungu, usiniambie mimi mjakazi wako uongo.

2 Wafalme 4:17 2ndKings 4:17

Yule mwanamke akachukua mimba, akazaa mtoto mume wakati uo huo mwakani, kama Elisha alivyomwambia.

2 Wafalme 4:18 2ndKings 4:18

Hata yule mtoto alipokua, ikawa siku moja alitoka kwenda kwa baba yake kwenye wavunao.

2 Wafalme 4:19 2ndKings 4:19

Akamwambia baba yake, Kichwa changu! Kichwa changu! Naye akamwambia mtumishi wake, Mchukue kwa mama yake.

2 Wafalme 4:20 2ndKings 4:20

Akamchukua, akampeleka kwa mama yake, naye akakaa magotini mwake hata adhuhuri, kisha akafa.

2 Wafalme 4:21 2ndKings 4:21

Mamaye akapanda juu, akamlaza juu ya kitanda cha yule mtu wa Mungu, akamfungia mlango, akatoka.

2 Wafalme 4:22 2ndKings 4:22

Kisha akamwita mumewe, akasema, Tafadhali, uniletee mtu mmoja wa watumishi, na punda mmoja, ili nimwendee yule mtu wa Mungu kwa haraka, nikarudi tena.

2 Wafalme 4:23 2ndKings 4:23

Akasema, Kwa nini kumwendea leo? Sio mwandamo wa mwezi, wala sabato. Akasema, Si neno.

2 Wafalme 4:24 2ndKings 4:24

Akatandika punda, akamwambia mtumishi wake, Mwendeshe, twendelee mbele. Usinipunguzie mwendo, nisipokuambia.

2 Wafalme 4:25 2ndKings 4:25

Basi akaenda, akafika kwa yule mtu wa Mungu, katika mlima wa Karmeli. Ikawa, yule mtu wa Mungu alipomwona kwa mbali, akamwambia Gehazi mtumishi wake, Tazama, Mshunami yule kule.

2 Wafalme 4:26 2ndKings 4:26

Tafadhali piga mbio sasa kwenda kumlaki, ukamwambie, Hujambo? Mume wako hajambo? Mtoto hajambo? Akajibu, Hawajambo.

2 Wafalme 4:27 2ndKings 4:27

Naye alipofika kwa yule mtu wa Mungu kilimani, alimshika miguu. Gehazi akakaribia amwondoe; lakini mtu wa Mungu akamwambia, Mwache; maana roho yake ndani yake ina uchungu; na Bwana amenificha, wala hakuniambia.

2 Wafalme 4:28 2ndKings 4:28

Yule mwanamke akasema, Je! Naliomba mwana kwa bwana wangu? Mimi sikusema, Usinidanganye?

2 Wafalme 4:29 2ndKings 4:29

Ndipo Elisha akamwambia Gehazi, Jikaze viuno, ukachukue fimbo yangu mkononi mwako, ukaende zako; ukikutana na mtu, usimsalimu; na mtu akikusalimu, usimjibu; ukaweke fimbo yangu juu ya uso wa mtoto.

2 Wafalme 4:30 2ndKings 4:30

Na mama yake yule mtoto akasema, Kama Bwana aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Basi akaondoka, akamfuata.

2 Wafalme 4:31 2ndKings 4:31

Na Gehazi akawatangulia, akaiweka ile fimbo juu ya uso wa mtoto; lakini hapakuwa na sauti, wala majibu. Basi akarudi ili kumlaki, akamwambia, akisema, Mtoto hakuamka.

2 Wafalme 4:32 2ndKings 4:32

Basi Elisha alipofika nyumbani, tazama, mtoto amekwisha kufa, amelazwa kitandani pake.

2 Wafalme 4:33 2ndKings 4:33

Basi akaingia ndani, akajifungia mlango, yeye na yule mtoto wote wawili, akamwomba Bwana.

2 Wafalme 4:34 2ndKings 4:34

Akapanda juu ya kitanda, akajilaza juu ya mtoto, akaweka kinywa chake juu ya kinywa chake, na macho yake juu ya macho yake, na mikono yake juu ya mikono yake; akajinyosha juu yake; mwili wake yule mtoto ukaanza kupata moto.

2 Wafalme 4:35 2ndKings 4:35

Kisha akarudi, akatembea nyumbani, huko na huko mara moja; akapanda, akajinyosha juu yake; na yule mtoto akapiga chafya mara saba, na mtoto akafumbua macho yake.

2 Wafalme 4:36 2ndKings 4:36

Akamwita Gehazi, akasema, Mwite yule Mshunami. Basi akamwita. Na alipofika kwake, Elisha akasema, Haya! Mchukue mwanao.

2 Wafalme 4:37 2ndKings 4:37

Ndipo akaingia, akamwangukia miguu akainama mpaka nchi; kisha akamchukua mwanawe, akatoka.

2 Wafalme 4:38 2ndKings 4:38

Elisha akafika Gilgali tena; na kulikuwa na njaa katika nchi; na hao wana wa manabii walikuwa wakikaa mbele yake. Akamwambia mtumishi wake, Teleka sufuria kubwa, uwapikie wana wa manabii.

2 Wafalme 4:39 2ndKings 4:39

Na mmoja wao akaenda nje kondeni ili kuchuma mboga, akaona mtango-mwitu, akayachuma matango-mwitu, hata nguo yake ikawa imejaa, akaja akayapasua-pasua sufuriani; kwa maana hawakuyajua.

2 Wafalme 4:40 2ndKings 4:40

Basi wakawapakulia hao watu ili wale. Ikawa, walipokuwa katika kula chakula, wakapiga kelele, wakasema, Mauti imo sufuriani, Ee mtu wa Mungu. Wala hawakuweza kula.

2 Wafalme 4:41 2ndKings 4:41

Lakini yeye akasema, Leteni unga. Naye akautupa ndani ya sufuria; akasema, Wapakulie watu, ili wale. Wala hakikuwamo kitu kibaya sufuriani.

2 Wafalme 4:42 2ndKings 4:42

Tena, akaja mtu kutoka Baal-shalisha, akamletea mtu wa Mungu chakula cha malimbuko, mikate ishirini ya shayiri, na masuke mabichi ya ngano guniani. Akasema, Uwape watu, ili wale.

2 Wafalme 4:43 2ndKings 4:43

Na mtumishi wake akasema, Je! Niwaandikie hiki watu mia? Lakini akasema, Uwape watu, ili wale; kwa kuwa Bwana asema hivi, Watakula na kusaza.

2 Wafalme 4:44 2ndKings 4:44

Basi akawaandikia, nao wakala, wakasaza, sawasawa na neno la Bwana.