2 Samweli Mlango 24 2nd Samuel

2 Samweli 24:1 2ndSamuel 24:1

Tena hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, akamtia Daudi nia juu yao, akisema, Nenda, ukawahesabu Israeli na Yuda.

2 Samweli 24:2 2ndSamuel 24:2

Basi mfalme akamwambia Yoabu, jemadari wa jeshi la askari, waliokuwa pamoja naye, Zunguka sasa katikati ya kabila zote za Israeli, tangu Dani mpaka Beer-sheba, mkawahesabu watu, nipate kujua jumla ya hao watu.

2 Samweli 24:3 2ndSamuel 24:3

Naye Yoabu akamwambia mfalme, Bwana, Mungu wako, na awaongeze watu, hesabu yao ikiwa yo yote, mara mia, tena macho ya bwana wangu mfalme na yawaone; ila kwa nini neno hili limempendeza bwana wangu mfalme?

2 Samweli 24:4 2ndSamuel 24:4

Lakini neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu, na juu ya majemadari wa jeshi. Basi Yoabu akatoka na majemadari wa jeshi machoni pa mfalme, kwenda kuwahesabu watu wa Israeli.

2 Samweli 24:5 2ndSamuel 24:5

Wakavuka Yordani, wakapiga kambi huko Aroeri, upande wa kuume wa mji ulioko kati ya bonde la Gadi, na mpaka Yazeri;

2 Samweli 24:6 2ndSamuel 24:6

kisha wakaja Gileadi, na nchi ya Wahiti huko Kadeshi; kisha wakaja Dani, na kutoka Dani wakazunguka mpaka Sidoni,

2 Samweli 24:7 2ndSamuel 24:7

wakaja ngomeni kwa Tiro, na kwa miji yote ya Wahivi, na ya Wakanaani; tena wakatoka kusini kwa Yuda huko Beer-sheba.

2 Samweli 24:8 2ndSamuel 24:8

Nao walipokwisha kuzunguka nchi yote, wakaja Yerusalemu mwisho wa miezi kenda na siku ishirini.

2 Samweli 24:9 2ndSamuel 24:9

Naye Yoabu akamtolea mfalme jumla ya hesabu ya watu; nao walikuwa wa Israeli mashujaa wenye kufuta panga mia nane elfu; nao wa Yuda walikuwa watu mia tano elfu.

2 Samweli 24:10 2ndSamuel 24:10

Ndipo moyo wake Daudi ukamchoma baada ya kuwahesabu hao watu. Naye Daudi akamwambia Bwana, Nimekosa sana kwa haya niliyoyafanya; lakini sasa, Ee Bwana, nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa.

2 Samweli 24:11 2ndSamuel 24:11

Na Daudi alipoondoka asubuhi, neno la Bwana likamjia nabii Gadi, mwonaji wake Daudi, kusema,

2 Samweli 24:12 2ndSamuel 24:12

Nenda, ukanene na Daudi, Bwana asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya uchague moja, nikutendee hilo.

2 Samweli 24:13 2ndSamuel 24:13

Basi Gadi akamwendea Daudi, akamweleza, akamwambia, Basi, miaka saba ya njaa ikujie katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui zako, huku wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako? Fanya shauri sasa, ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma.

2 Samweli 24:14 2ndSamuel 24:14

Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na tuanguke katika mkono wa Bwana; kwa kuwa rehema zake ni nyingi; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu.

2 Samweli 24:15 2ndSamuel 24:15

Basi Bwana akawaletea Israeli tauni tangu asubuhi hata wakati ulioamriwa; nao wakafa watu toka Dani mpaka Beer-sheba sabini elfu.

2 Samweli 24:16 2ndSamuel 24:16

Lakini huyo malaika aliponyosha mkono wake kuelekea Yerusalemu ili auharibu, Bwana akaghairi katika mabaya, akamwambia huyo malaika mwenye kuwaharibu watu, Yatosha, sasa ulegeze mkono wako. Naye yule malaika wa Bwana alikuwako karibu na kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi.

2 Samweli 24:17 2ndSamuel 24:17

Daudi, alipomwoma malaika aliyewapiga watu, akanena na Bwana, akasema, Tazama, ni mimi niliyekosa, ni mimi niliyepotoka; lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Mkono wako na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya baba yangu.

2 Samweli 24:18 2ndSamuel 24:18

Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, Haya! Kwea wewe, ukamwinulie Bwana madhabahu penye kiwanja cha Arauna, Myebusi.

2 Samweli 24:19 2ndSamuel 24:19

Basi Daudi akakwea sawasawa na neno la Gadi, kama Bwana alivyoamuru.

2 Samweli 24:20 2ndSamuel 24:20

Huyo Arauna akatazama, akamwona mfalme na watumishi wake wakimjia; Arauna akatoka, akasujudu mbele ya mfalme kifulifuli hata nchi.

2 Samweli 24:21 2ndSamuel 24:21

Arauna akasema, Bwana wangu mfalme amemjia mtumwa wake kwa kusudi gani? Naye Daudi akasema, Makusudi ninunue kwako kiwanja hiki, ili nimjengee Bwana madhabahu, ili kwamba tauni ipate kuzuiliwa katika watu.

2 Samweli 24:22 2ndSamuel 24:22

Arauna akamwambia Daudi, Bwana wangu mfalme na akitwae, akatolee yaliyo mema machoni pake; tazama, ng'ombe hawa kwa sadaka ya kuteketezwa, tena vyombo vya kupuria, na vyombo vya ng'ombe, viko kwa kuni,

2 Samweli 24:23 2ndSamuel 24:23

vitu hivi vyote, Ee mfalme, mimi Arauna nakupa wewe mfalme. Kisha Arauna akamwambia mfalme, Bwana, Mungu wako, na akukubali.

2 Samweli 24:24 2ndSamuel 24:24

Lakini mfalme akamwambia Arauna, La, sivyo; lakini kweli nitavinunua kwako kwa thamani yake; wala sitamtolea Bwana, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa nisizozigharimia. Hivyo Daudi akakinunua hicho kiwanja cha kupuria na wale ng'ombe kwa shekeli hamsini za fedha.

2 Samweli 24:25 2ndSamuel 24:25

Naye Daudi akamjengea Bwana madhabahu huko, akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Basi Bwana aliiridhia nchi, na tauni ikazuiliwa katika Israeli.