2 Samweli Mlango 13 2nd Samuel

2 Samweli 13:1 2ndSamuel 13:1

Ikawa baada ya hayo, Absalomu, mwana wa Daudi, alikuwa na umbu mzuri, jina lake akiitwa Tamari, naye Amnoni, mwana wa Daudi, akampenda.

2 Samweli 13:2 2ndSamuel 13:2

Akasononeka Amnoni, hata akaugua, kwa ajili ya umbu lake Tamari, maana huyu msichana alikuwa mwanamwali, Amnoni akaona ni vigumu kumtendea neno lo lote.

2 Samweli 13:3 2ndSamuel 13:3

Lakini Amnoni alikuwa na rafiki, jina lake Yonadabu, mwana wa Shama, nduguye Daudi; naye Yonadabu alikuwa mtu mwerevu sana.

2 Samweli 13:4 2ndSamuel 13:4

Naye akamwambia, Kwa nini, Ee mwana wa mfalme, unakonda hivi siku kwa siku? Hutaki kuniambia? Amnoni akamwambia, Nampenda Tamari, umbu la ndugu yangu, Absalomu.

2 Samweli 13:5 2ndSamuel 13:5

Yonadabu akamwambia, Lala kitandani mwako ujifanye mgonjwa na babako atakapokuja kukutazama, umwambie, Mwache ndugu yangu, Tamari, aje, nakusihi, anipe mkate nile, akaandae chakula machoni pangu nikione, nikakile mkononi mwake.

2 Samweli 13:6 2ndSamuel 13:6

Basi Amnoni akalala, akajifanya mgonjwa; na mfalme alipokuja kumtazama, Amnoni akamwambia mfalme Mwache ndugu yangu, Tamari, aje, nakusihi, aniandalie mikate miwili machoni pangu, nipate kula mkononi mwake.

2 Samweli 13:7 2ndSamuel 13:7

Basi Daudi akatuma mjumbe aende nyumbani kwa Tamari, akasema, Nenda sasa nyumbani kwa Amnoni, ndugu yako, ukamwandalie chakula.

2 Samweli 13:8 2ndSamuel 13:8

Akaenda Tamari nyumbani kwa nduguye Amnoni; naye alikuwa amelala. Akachukua unga, akaukanda, akaiandaa mikate machoni pake, akaioka mikate.

2 Samweli 13:9 2ndSamuel 13:9

Akalitwaa kaango, akaisongeza mbele yake; lakini alikataa kula. Naye Amnoni akasema, Toeni watu wote kwangu. Wakatoka kila mtu kwake.

2 Samweli 13:10 2ndSamuel 13:10

Amnoni akamwambia Tamari, Kilete chakula chumbani, nipate kula mkononi mwako. Basi Tamari akaitwaa mikate aliyoifanyiza, akamletea Amnoni nduguye mle chumbani.

2 Samweli 13:11 2ndSamuel 13:11

Naye alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia, Njoo ulale nami, ndugu yangu.

2 Samweli 13:12 2ndSamuel 13:12

Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinitenze nguvu; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu.

2 Samweli 13:13 2ndSamuel 13:13

Nami nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa.

2 Samweli 13:14 2ndSamuel 13:14

Walakini yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye, akamtenza nguvu, akalala naye.

2 Samweli 13:15 2ndSamuel 13:15

Kisha Amnoni akamchukia machukio makuu sana; kwa kuwa machukio aliyomchukia yakawa makuu kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza. Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako.

2 Samweli 13:16 2ndSamuel 13:16

Naye akamwambia, Sivyo, kwa kuwa mabaya haya ya kunitoa ni makuu kuliko yale uliyonitendea. Lakini alikataa kumsikiliza.

2 Samweli 13:17 2ndSamuel 13:17

Ndipo akamwita mtumishi wake aliyemtumikia, akasema, Mtoe sasa mwanamke huyu kwangu, ukafunge mlango nyuma yake.

2 Samweli 13:18 2ndSamuel 13:18

Naye alikuwa amevaa kanzu ndefu; kwa kuwa kwa nguo hizo huvikwa binti za mfalme waliokuwa wanawali. Ndipo mtumishi wake akamleta nje, akafunga mlango nyuma yake.

2 Samweli 13:19 2ndSamuel 13:19

Naye Tamari akatia majivu kichwani mwake, akairarua hiyo kanzu ndefu yake aliyoivaa, akaweka mkono kichwani akaenda zake huku akilia kwa sauti.

2 Samweli 13:20 2ndSamuel 13:20

Huyo Absalomu nduguye akamwambia, je! Amekuwa nawe Amnoni nduguyo? Ila sasa tulia, dada; ni nduguyo; usilitie moyoni jambo hili. Basi Tamari akakaa hali ya ukiwa nyumbani mwa nduguye Absalomu.

2 Samweli 13:21 2ndSamuel 13:21

Na mfalme Daudi alipoyasikia maneno hayo yote, alikasirika sana.

2 Samweli 13:22 2ndSamuel 13:22

Ila Absalomu hakusema na Amnoni wala kwa heri wala kwa shari; kwa maana Absalomu alimchukia Amnoni kwa kumtenza nguvu umbu lake Tamari.

2 Samweli 13:23 2ndSamuel 13:23

Ikawa baada ya miaka miwili mizima, Absalomu alikuwa na wenye kukata manyoya ya kondoo huko Baal-hasori uliopo upande wa Efraimu; naye Absalomu akawaalika wana wote wa mfalme.

2 Samweli 13:24 2ndSamuel 13:24

Absalomu akamjia mfalme, akasema, Tazama sasa, mimi mtumwa wako ninao wakata manyoya ya kondoo; basi mfalme na aende, nakusihi, na watumishi wake pamoja nami mtumwa wako.

2 Samweli 13:25 2ndSamuel 13:25

Mfalme akamwambia Absalomu, Sivyo, mwanangu, tusiende sote, tusije tukakulemea. Akamsihi sana; asikubali kwenda, ila akambariki.

2 Samweli 13:26 2ndSamuel 13:26

Ndipo akasema Absalomu, Kwamba huji, nakusihi, mwache ndugu yangu Amnoni aende nasi.

2 Samweli 13:27 2ndSamuel 13:27

Mfalme akamwambia, Kwa nini aende nawe? Lakini Absalomu akamsihi sana, naye akamwacha Amnoni na wana wote wa mfalme waende naye.

2 Samweli 13:28 2ndSamuel 13:28

Kisha Absalomu akawaamuru watumishi wake, akasema, Angalieni basi, moyo wake Amnoni utakapofurahiwa kwa mvinyo; nami nitakapowaambia, Mpigeni Amnoni, ndipo mwueni, msiogope; si mimi niliyewaamuru? Iweni hodari, iweni na ujasiri.

2 Samweli 13:29 2ndSamuel 13:29

Basi watumishi wa Absalomu wakamfanyia Amnoni kama alivyoamuru Absalomu. Ndipo wakaondoka wana wote wa mfalme, wakapanda kila mtu nyumbu wake, wakakimbia.

2 Samweli 13:30 2ndSamuel 13:30

Ikawa, walipokuwa njiani, habari zikamwasilia Daudi, kusema, Absalomu amewaua wana wote wa mfalme, wala hata mmoja wao hakusalia.

2 Samweli 13:31 2ndSamuel 13:31

Ndipo mfalme akainuka, akararua nguo zake, akalala chini; nao watumishi wake wote wakasimama karibu naye, wenye nguo zao zimeraruliwa.

2 Samweli 13:32 2ndSamuel 13:32

Akajibu Yonadabu, mwana wa Shama, nduguye Daudi, akasema, Asidhani bwana wangu ya kwamba wamewaua vijana wote, wana wa mfalme; maana ndiye Amnoni peke yake aliyekufa; yakini haya yamekusudiwa kwa kinywa chake Absalomu tangu siku ile alipotenzwa nguvu umbu lake, Tamari.

2 Samweli 13:33 2ndSamuel 13:33

Basi sasa bwana wangu mfalme asilitie neno hili moyoni, kudhani ya kwamba wana wote wa mfalme wamekufa maana ni Amnoni peke yake aliyekufa.

2 Samweli 13:34 2ndSamuel 13:34

Lakini Absalomu akakimbia. Na kijana yule aliyekuwa mlinzi akainua macho yake, akaona, na tazama, kuna watu wengi wanakuja kwa njia ya upande wa kilima nyuma yake.

2 Samweli 13:35 2ndSamuel 13:35

Ndipo Yonadabu akamwambia mfalme, Tazama, wana wa mfalme wamekuja; kama mimi mtumwa wako nilivyosema, ndivyo ilivyo.

2 Samweli 13:36 2ndSamuel 13:36

Ikawa alipokwisha kusema, tazama, wana wa mfalme walikuja, nao wakapaza sauti zao wakalia; mfalme naye akalia, na watumishi wake wote, kilio kikubwa mno.

2 Samweli 13:37 2ndSamuel 13:37

Lakini Absalomu akakimbia, akamwendea Talmai, mwana wa Amihuri, mfalme wa Geshuri. Naye Daudi akamlilia mwanawe kila siku.

2 Samweli 13:38 2ndSamuel 13:38

Basi Absalomu akakimbia, akaenda Geshuri, akakaa huko muda wa miaka mitatu.

2 Samweli 13:39 2ndSamuel 13:39

Mfalme Daudi akatamani kutoka kumwendea Absalomu kwa kuwa ametulizwa kwa habari ya Amnoni, kwa maana amekufa.