2 Samweli Mlango 11 2nd Samuel

2 Samweli 11:1 2ndSamuel 11:1

Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akampeleka Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote; wakawaangamiza wana wa Amoni, wakauhusuru Raba. Lakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu.

2 Samweli 11:2 2ndSamuel 11:2

Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho.

2 Samweli 11:3 2ndSamuel 11:3

Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti?

2 Samweli 11:4 2ndSamuel 11:4

Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake.

2 Samweli 11:5 2ndSamuel 11:5

Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka na kumwambia Daudi, akasema, Ni mja-mzito.

2 Samweli 11:6 2ndSamuel 11:6

Ndipo Daudi akapeleka kwa Yoabu, akisema, Unipelekee Uria, Mhiti. Naye Yoabu akampeleka Uria kwa Daudi.

2 Samweli 11:7 2ndSamuel 11:7

Uria alipomwendea Daudi, Daudi alimwuliza habari za Yoabu, na habari za watu, na habari za vita.

2 Samweli 11:8 2ndSamuel 11:8

Daudi akamwambia Uria, Haya, shuka nyumbani kwako, ukanawe miguu yako. Basi Uria akatoka katika nyumba ya mfalme, na tunu ya vyakula ikamfuata, iliyotoka kwa mfalme.

2 Samweli 11:9 2ndSamuel 11:9

Lakini Uria akalala mlangoni pa nyumba ya mfalme, pamoja na watumishi wote wa bwana wake, wala hakushuka nyumbani kwake.

2 Samweli 11:10 2ndSamuel 11:10

Watu walipomwambia Daudi ya kwamba, Uria hakushuka nyumbani kwake, Daudi akamwambia Uria, Je! Hukutoka safarini? Mbona hukushuka nyumbani kwako?

2 Samweli 11:11 2ndSamuel 11:11

Naye Uria akamwambia Daudi, Sanduku, na Israeli, na Yuda, wanakaa vibandani; na bwana wangu Yoabu, na watumishi wa bwana wangu, wamepiga kambi waziwazi uwandani; nami niende nyumbani kwangu, kula na kunywa, na kulala na mke wangu? Uishivyo, na kama roho yako iishivyo, mimi sitafanya jambo hili.

2 Samweli 11:12 2ndSamuel 11:12

Basi Daudi akamwambia Uria, Ngoja hapa leo tena, na kesho nitakuacha kwenda zako. Basi Uria akakaa Yerusalemu siku ile, na siku ya pili yake.

2 Samweli 11:13 2ndSamuel 11:13

Naye Daudi akamwalika, akala, akanywa mbele yake; naye akamlevya; hata wakati wa jioni akatoka kwenda kulala kitandani mwake pamoja na watumishi wa bwana wake, lakini hakushuka nyumbani kwake.

2 Samweli 11:14 2ndSamuel 11:14

Hata ikawa asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu waraka, akaupeleka kwa mkono wa Uria.

2 Samweli 11:15 2ndSamuel 11:15

Akaandika katika waraka huo, kusema, Mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe akafe.

2 Samweli 11:16 2ndSamuel 11:16

Ikawa, Yoabu alipokuwa akiuhusuru mji, akamweka Uria mahali alipojua ya kuwa pana mashujaa.

2 Samweli 11:17 2ndSamuel 11:17

Watu wa mji wakatoka, wakapigana na Yoabu; na baadhi ya watu, watumishi wa Daudi, wakaanguka; Uria Mhiti naye akafa.

2 Samweli 11:18 2ndSamuel 11:18

Ndipo Yoabu akapeleka na kumwarifu Daudi habari zote za vita;

2 Samweli 11:19 2ndSamuel 11:19

akamwagiza yule mjumbe, akisema, Ukiisha kumpa mfalme habari zote za vita,

2 Samweli 11:20 2ndSamuel 11:20

itakuwa, hasira ya mfalme ikiwaka, akakuambia, Kwani mliukaribia mji namna ile ili kuupiga? Je! Hamkujua ya kuwa watapiga mishale toka ukutani?

2 Samweli 11:21 2ndSamuel 11:21

Ni nani aliyempiga Ahimeleki, mwana wa Yeru-beshethi? Je! Si mwanamke aliyemtupia jiwe la kusagia la juu kutoka ukutani? Hata akafa huko Thebesi? Kwani kuukaribia ukuta namna ile? Ndipo utakaposema, Mtumishi wako Uria, Mhiti, amekufa naye.

2 Samweli 11:22 2ndSamuel 11:22

Basi yule mjumbe akaenda, akafika na kumwonyesha Daudi yote aliyomtuma Yoabu.

2 Samweli 11:23 2ndSamuel 11:23

Yule mjumbe akamwambia Daudi, Watu hao walitushinda, wakatutokea nje hata uwandani, tukashindana nao hata mahali pa kuingilia langoni.

2 Samweli 11:24 2ndSamuel 11:24

Wapiga mishale wakatupiga sisi, watumishi wako, toka juu ya ukuta; na baadhi ya watumishi wa mfalme wamekufa, na Uria, Mhiti, mtumishi wako, amekufa naye.

2 Samweli 11:25 2ndSamuel 11:25

Basi Daudi akamwambia yule mjumbe, Basi, mwambie Yoabu maneno haya, Jambo hili lisiwe baya machoni pako, maana upanga hula huyu kama unavyomla huyu; zidi kutia nguvu vita vyako juu ya mji ukauangushe; nawe mtie moyo.

2 Samweli 11:26 2ndSamuel 11:26

Na yule mke wa Uria alipopata habari ya kuwa Uria mumewe amekufa, akamwombolezea mumewe.

2 Samweli 11:27 2ndSamuel 11:27

Hata maombolezo hayo yalipokwisha, Daudi akatuma mtu, akamtwaa, akamtia nyumbani mwake; naye akawa mkewe, akamzalia mwana. Lakini jambo lile alilolitenda Daudi likamchukiza Bwana.