2 Samweli Mlango 17 2nd Samuel

2 Samweli 17:1 2ndSamuel 17:1

Zaidi ya hayo Ahithofeli akamwambia Absalomu, Niache nichague watu kumi na mbili elfu, nami nitaondoka na kumfuatia Daudi usiku huu;

2 Samweli 17:2 2ndSamuel 17:2

nami nitamshambulia wakati atakaokuwa amechoka, na mikono yake imekuwa dhaifu, nami nitamtia hofu; na watu wote walio pamoja naye watakimbia; nami nitampiga mfalme peke yake;

2 Samweli 17:3 2ndSamuel 17:3

na hao watu wote nitawarejeza kwako; mtu yule umtafutaye ni kana kwamba wamerudi wote; na hivyo watu wote watakuwa katika amani.

2 Samweli 17:4 2ndSamuel 17:4

Shauri hili likawa jema machoni pa Absalomu, na machoni pa wazee wote wa Israeli.

2 Samweli 17:5 2ndSamuel 17:5

Ndipo Absalomu akasema, Basi, mwiteni Hushai, Mwarki, naye, tukasikie atakayosema yeye pia.

2 Samweli 17:6 2ndSamuel 17:6

Basi Hushai alipofika kwa Absalomu, Absalomu akamwambia, akasema, Ahithofeli amesema hivi; je! Tufanye kama alivyosema? Kama sivyo, sema maneno yako.

2 Samweli 17:7 2ndSamuel 17:7

Hushai akamwambia Absalomu, Shauri hili alilolitoa Ahithofeli si jema wakati huu.

2 Samweli 17:8 2ndSamuel 17:8

Hushai akafuliza kusema, Wamjua baba yako na watu wake, ya kuwa ni watu mashujaa hawa, nao wana uchungu katika mioyo yao, kama dubu aliyenyang'anywa watoto wake nyikani; tena baba yako ni mtu wa vita, hatalala pamoja na watu wake.

2 Samweli 17:9 2ndSamuel 17:9

Angalia, amefichwa sasa katika shimo, au penginepo; kisha itakuwa, watakapoanguka baadhi yao mwanzo, kila mtu atakayesikia, atasema, Kuna machinjo katika watu wanaofuatana na Absalomu.

2 Samweli 17:10 2ndSamuel 17:10

Basi hata yeye aliye shujaa, mwenye moyo kama moyo wa simba, atayeyuka kabisa; maana Israeli wote wanajua ya kuwa baba yako ni shujaa, na ya kuwa watu wale walio pamoja naye ni mashujaa.

2 Samweli 17:11 2ndSamuel 17:11

Kwa hiyo shauri langu ni hili, Waisraeli wote toka Dani mpaka Beer-sheba wakusanyike kwako, kama mchanga wa bahari kwa wingi; na wewe uende vitani mwenyewe.

2 Samweli 17:12 2ndSamuel 17:12

Hivyo tutamfikia mahali po pote atakapoonekana, na kumwangukia kama vile umande uangukavyo juu ya nchi; wala hatutaacha hata mmoja wao, yeye na watu wote walio pamoja naye.

2 Samweli 17:13 2ndSamuel 17:13

Tena, ikiwa amejitia katika mji uwao wote, basi Israeli wote wataleta kamba, na kuuendea mji ule, nasi tutaukokota mpaka mtoni, wala halitaonekana huko hata jiwe dogo moja la mawe yake.

2 Samweli 17:14 2ndSamuel 17:14

Naye Absalomu na watu wote wa Israeli wakasema, Shauri la Hushai, Mwarki, ni jema kuliko shauri la Ahithofeli. Kwa maana Bwana alikuwa amekusudia kulivunja shauri jema la Ahithofeli, ili Bwana alete mabaya juu ya Absalomu.

2 Samweli 17:15 2ndSamuel 17:15

Ndipo Hushai akawaambia Sadoki na Abiathari, makuhani, Ahithofeli amempa Absalomu na wazee wa Israeli mashauri kadha wa kadha; na mimi nimetoa mashauri kadha wa kadha.

2 Samweli 17:16 2ndSamuel 17:16

Basi sasa pelekeni habari upesi kamwambieni Daudi ya kwamba, Usilale usiku huu karibu na vivuko vya jangwani; bali usikose kuvuka; asije akamezwa mfalme, na watu wote walio pamoja naye.

2 Samweli 17:17 2ndSamuel 17:17

Basi Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakikaa karibu na Enrogeli; na mjakazi mmoja alikuwa akienda na kuwapa habari; nao huenda kumwambia mfalme Daudi; maana ilikuwa lazima wasionekane wakiingia mjini.

2 Samweli 17:18 2ndSamuel 17:18

Lakini kijana mmoja aliwaona, akamwambia Absalomu; basi wakaenda wote wawili kwa haraka, wakafika Bahurimu, nyumbani kwa mtu aliyekuwa na kisima uani mwake; wakashuka ndani yake.

2 Samweli 17:19 2ndSamuel 17:19

Na mwanamke akatwaa kifuniko akakiweka juu ya mdomo wa kile kisima, akaanika ngano iliyotwangwa juu yake; wala halikujulikana neno lo lote.

2 Samweli 17:20 2ndSamuel 17:20

Nao watumishi wa Absalomu wakamwendea yule mwanamke mle nyumbani; wakasema, Wako wapi Yonathani na Ahimaasi? Yule mwanamke akawaambia, Wamevuka kijito cha maji. Basi walipokwisha kuwatafuta wasiwaone, wakarudi Yerusalemu.

2 Samweli 17:21 2ndSamuel 17:21

Kisha ikawa, baada ya kuondoka kwao, wale wakatoka kisimani, wakaenda wakamwarifu mfalme Daudi; wakamwambia Daudi, Ondokeni, mkavuke maji haya upesi; maana ndivyo alivyotoa shauri Ahithofeli juu yenu.

2 Samweli 17:22 2ndSamuel 17:22

Ndipo Daudi, na watu wote waliokuwa pamoja naye, wakaondoka, wakavuka Yordani; na kulipopambazuka hakubaki mmojawapo wao asiyevuka Yordani.

2 Samweli 17:23 2ndSamuel 17:23

Naye Ahithofeli alipoona ya kuwa shauri lake halikufuatwa, akatandika punda wake, akaondoka, akaenda nyumbani kwake, mjini mwake, akaitengeneza nyumba yake, akajisonga; akafa, akazikwa kaburini mwa babaye.

2 Samweli 17:24 2ndSamuel 17:24

Basi Daudi akaja Mahanaimu. Naye Absalomu akauvuka Yordani yeye na watu wote wa Israeli pamoja naye.

2 Samweli 17:25 2ndSamuel 17:25

Naye Absalomu akamweka Amasa awe juu ya jeshi mahali pa Yoabu. Basi huyo Amasa alikuwa mwana wa mtu, jina lake Yetheri, Mwishmaeli, aliyeingia kwa Abigali, binti Nahashi, nduguye Seruya, mamaye Yoabu.

2 Samweli 17:26 2ndSamuel 17:26

Israeli na Absalomu wakapiga kambi katika nchi ya Gileadi.

2 Samweli 17:27 2ndSamuel 17:27

Ikawa, Daudi alipofika Mahanaimu, Shobi, mwana wa Nahashi wa Raba, wa wana wa Amoni, na Makiri, mwana wa Amieli wa Lo-debari, na Barzilai, Mgileadi wa Rogelimu,

2 Samweli 17:28 2ndSamuel 17:28

wakaleta magodoro, na mabakuli, na vyungu, na ngano, na shayiri, na unga, na bisi, na kunde, na dengu,

2 Samweli 17:29 2ndSamuel 17:29

na asali, na siagi, na kondoo, na samli ya ng'ombe, wapate kula Daudi na watu waliokuwa pamoja naye; kwani walisema, Watu hao waona njaa, tena wamechoka, nao wana kiu huku nyikani.