Warumi Mlango 13 Romans

Warumi 13:1 Romans 13:1

Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu.

Warumi 13:2 Romans 13:2

Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu.

Warumi 13:3 Romans 13:3

Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya mema, nawe utapata sifa kwake;

Warumi 13:4 Romans 13:4

kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu kwako kwa ajili ya mema. Lakini ufanyapo mabaya, ogopa; kwa maana hauchukui upanga bure; kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu, amlipizaye kisasi mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu.

Warumi 13:5 Romans 13:5

Kwa hiyo ni lazima kutii, si kwa sababu ya ile ghadhabu tu, ila na kwa sababu ya dhamiri.

Warumi 13:6 Romans 13:6

Kwa sababu hiyo tena mwalipa kodi; kwa kuwa wao ni wahudumu wa Mungu, wakidumu katika kazi iyo hiyo.

Warumi 13:7 Romans 13:7

Wapeni wote haki zao; mtu wa kodi, kodi; mtu wa ushuru, ushuru; astahiliye hofu, hofu; astahiliye heshima, heshima.

Warumi 13:8 Romans 13:8

Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria.

Warumi 13:9 Romans 13:9

Maana kule kusema, Usizini, Usiue, Usiibe, Usitamani; na ikiwapo amri nyingine yo yote, inajumlishwa katika neno hili, ya kwamba, Mpende jirani yako kama nafsi yako.

Warumi 13:10 Romans 13:10

Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria.

Warumi 13:11 Romans 13:11

Naam, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini

Warumi 13:12 Romans 13:12

Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia, basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru.

Warumi 13:13 Romans 13:13

Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu.

Warumi 13:14 Romans 13:14

Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake.