Warumi Mlango 10 Romans

Warumi 10:1 Romans 10:1

Ndugu zangu, nitakayo sana moyoni mwangu, na dua yangu nimwombayo Mungu, ni kwa ajili yao, ili waokolewe.

Warumi 10:2 Romans 10:2

Kwa maana nawashuhudia kwamba wana juhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si katika maarifa.

Warumi 10:3 Romans 10:3

Kwa maana, wakiwa hawaijui haki ya Mungu, na wakitaka kuithibitisha haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu.

Warumi 10:4 Romans 10:4

Kwa maana Kristo ni mwisho wa sheria, ili kila aaminiye ahesabiwe haki.

Warumi 10:5 Romans 10:5

Kwa maana Musa aliandika juu ya haki itokayo kwa sheria, ya kuwa, Mtu afanyaye hiyo ataishi kwa hiyo.

Warumi 10:6 Romans 10:6

Bali ile haki ipatikanayo kwa imani yanena hivi, Usiseme moyoni mwako, Ni nani atakayepanda kwenda mbinguni? (Yaani, ni kumleta Kristo chini),

Warumi 10:7 Romans 10:7

au, Ni nani atakayeshuka kwenda kuzimuni? (Yaani, ni kumleta Kristo juu, kutoka kwa wafu.)

Warumi 10:8 Romans 10:8

Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo.

Warumi 10:9 Romans 10:9

Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.

Warumi 10:10 Romans 10:10

Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.

Warumi 10:11 Romans 10:11

Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika.

Warumi 10:12 Romans 10:12

Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao;

Warumi 10:13 Romans 10:13

kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.

Warumi 10:14 Romans 10:14

Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri?

Warumi 10:15 Romans 10:15

Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!

Warumi 10:16 Romans 10:16

Lakini si wote walioitii ile habari njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu?

Warumi 10:17 Romans 10:17

Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.

Warumi 10:18 Romans 10:18

Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.

Warumi 10:19 Romans 10:19

Lakini nasema, Je! Waisraeli hawakufahamu? Kwanza Musa anena, Nitawatia wivu kwa watu ambao si taifa, Kwa taifa lisilo na fahamu nitawaghadhibisha.

Warumi 10:20 Romans 10:20

Na Isaya anao ujasiri mwingi, asema, Nalipatikana nao wasionitafuta, Nalidhihirika kwao wasioniulizia.

Warumi 10:21 Romans 10:21

Lakini kwa Israeli asema, Mchana kutwa naliwanyoshea mikono watu wasiotii na wakaidi.