Warumi Mlango 11 Romans

Warumi 11:1 Romans 11:1

Basi, nauliza, Je! Mungu aliwasukumia mbali watu wake? Hasha! Kwa kuwa mimi nami ni Mwisraeli, mmoja wa wazao wa Ibrahimu, mtu wa kabila ya Benyamini.

Warumi 11:2 Romans 11:2

Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa na maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu,

Warumi 11:3 Romans 11:3

Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho yangu.

Warumi 11:4 Romans 11:4

Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali.

Warumi 11:5 Romans 11:5

Basi ni vivi hivi wakati huu wa sasa, yako mabaki waliochaguliwa kwa neema.

Warumi 11:6 Romans 11:6

Lakini ikiwa ni kwa neema, haiwi kwa matendo tena, au hapo neema isingekuwa neema.

Warumi 11:7 Romans 11:7

Imekuwaje basi? Kitu kile ambacho Israeli alikuwa akikitafuta hakukipata; lakini wale waliochaguliwa walikipata, na wengine walitiwa uzito.

Warumi 11:8 Romans 11:8

Kama ilivyoandikwa, Mungu aliwapa roho ya usingizi, macho hata wasione, na masikio hata wasisikie, hata siku hii ya leo.

Warumi 11:9 Romans 11:9

Na Daudi asema, Meza yao na iwe tanzi na mtego, Na kitu cha kuwakwaza, na malipo kwao;

Warumi 11:10 Romans 11:10

Macho yao yatiwe giza ili wasione, Ukawainamishe mgongo wao siku zote.

Warumi 11:11 Romans 11:11

Basi nasema, Je! Wamejikwaa hata waanguke kabisa? Hasha! Lakini kwa kosa lao wokovu umewafikilia Mataifa, ili wao wenyewe watiwe wivu.

Warumi 11:12 Romans 11:12

Basi, ikiwa kosa lao limekuwa utajiri wa ulimwengu, na upungufu wao umekuwa utajiri wa Mataifa, je! Si zaidi sana utimilifu wao?

Warumi 11:13 Romans 11:13

Lakini nasema na ninyi, mlio watu wa Mataifa. Basi, kwa kadiri nilivyo mtume wa watu wa Mataifa, naitukuza huduma iliyo yangu,

Warumi 11:14 Romans 11:14

nipate kuwatia wivu walio damu moja na mimi na kuwaokoa baadhi yao.

Warumi 11:15 Romans 11:15

Maana ikiwa kutupwa kwao kumeleta upatanisho kwa ulimwengu, je! Kukubaliwa kwao kutakuwa nini kama si uhai baada ya kufa?

Warumi 11:16 Romans 11:16

Tena malimbuko yakiwa matakatifu, kadhalika na donge lote; na shina likiwa takatifu, matawi nayo kadhalika.

Warumi 11:17 Romans 11:17

Lakini iwapo matawi mengine yamekatwa, na wewe mzeituni mwitu ulipandikizwa kati yao, ukawa mshirika wa shina la mzeituni na unono wake,

Warumi 11:18 Romans 11:18

usijisifu juu ya matawi yale; au ikiwa wajisifu, si wewe ulichukuaye shina, bali ni shina likuchukualo wewe.

Warumi 11:19 Romans 11:19

Basi utasema, Matawi yale yalikatwa kusudi ili nipandikizwe mimi.

Warumi 11:20 Romans 11:20

Vema. Yalikatwa kwa kutokuamini kwao, na wewe wasimama kwa imani yako. Usijivune, bali uogope.

Warumi 11:21 Romans 11:21

Kwa maana ikiwa Mungu hakuyaachia matawi ya asili, wala hatakuachia wewe.

Warumi 11:22 Romans 11:22

Tazama, basi, wema na ukali wa Mungu; kwa wale walioanguka, ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, ukikaa katika wema huo; kama sivyo, wewe nawe utakatiliwa mbali.

Warumi 11:23 Romans 11:23

Na hao pia, wasipokaa katika kutokuamini kwao, watapandikizwa; kwa kuwa Mungu aweza kuwapandikiza tena.

Warumi 11:24 Romans 11:24

Kwa maana ikiwa wewe ulikatwa ukatolewa katika mzeituni, ulio mzeituni mwitu kwa asili yake, kisha ukapandikizwa, kinyume cha asili, katika mzeituni ulio mwema, si zaidi sana wale walio wa asili kuweza kupandikizwa katika mzeituni wao wenyewe?

Warumi 11:25 Romans 11:25

Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili.

Warumi 11:26 Romans 11:26

Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake.

Warumi 11:27 Romans 11:27

Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao.

Warumi 11:28 Romans 11:28

Basi kwa habari ya Injili wamekuwa adui kwa ajili yenu; bali kwa habari ya kule kuchaguliwa wamekuwa wapenzi kwa ajili ya baba zetu.

Warumi 11:29 Romans 11:29

Kwa sababu karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake.

Warumi 11:30 Romans 11:30

Kwa maana kama ninyi zamani mlivyomwasi Mungu, lakini sasa mmepata rehema kwa kuasi kwao;

Warumi 11:31 Romans 11:31

kadhalika na hao wameasi sasa, ili kwa kupata rehema kwenu wao nao wapate rehema.

Warumi 11:32 Romans 11:32

Maana Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote.

Warumi 11:33 Romans 11:33

Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani!

Warumi 11:34 Romans 11:34

Maana ni nani aliyeijua nia ya Bwana? Au ni nani aliyekuwa mshauri wake?

Warumi 11:35 Romans 11:35

Au ni nani aliyempa yeye kitu kwanza, naye atalipwa tena?

Warumi 11:36 Romans 11:36

Kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina.