Matendo ya Mitume Mlango 8 Acts

Matendo ya Mitume 8:1 Acts 8:1

Siku ile kukatukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume.

Matendo ya Mitume 8:2 Acts 8:2

Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu.

Matendo ya Mitume 8:3 Acts 8:3

Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani.

Matendo ya Mitume 8:4 Acts 8:4

Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno.

Matendo ya Mitume 8:5 Acts 8:5

Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo.

Matendo ya Mitume 8:6 Acts 8:6

Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya.

Matendo ya Mitume 8:7 Acts 8:7

Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa.

Matendo ya Mitume 8:8 Acts 8:8

Ikawa furaha kubwa katika mji ule.

Matendo ya Mitume 8:9 Acts 8:9

Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa.

Matendo ya Mitume 8:10 Acts 8:10

Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu.

Matendo ya Mitume 8:11 Acts 8:11

Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake.

Matendo ya Mitume 8:12 Acts 8:12

Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake.

Matendo ya Mitume 8:13 Acts 8:13

Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka.

Matendo ya Mitume 8:14 Acts 8:14

Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana;

Matendo ya Mitume 8:15 Acts 8:15

ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu;

Matendo ya Mitume 8:16 Acts 8:16

kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu.

Matendo ya Mitume 8:17 Acts 8:17

Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu.

Matendo ya Mitume 8:18 Acts 8:18

Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema,

Matendo ya Mitume 8:19 Acts 8:19

Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu.

Matendo ya Mitume 8:20 Acts 8:20

Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali.

Matendo ya Mitume 8:21 Acts 8:21

Huna fungu wala huna sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu.

Matendo ya Mitume 8:22 Acts 8:22

Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili kama yamkini, usamehewe fikira hii ya moyo wako.

Matendo ya Mitume 8:23 Acts 8:23

Kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena u katika kifungo cha uovu.

Matendo ya Mitume 8:24 Acts 8:24

Simoni akajibu, akasema, Niombeeni ninyi kwa Bwana, yasinifikilie mambo haya mliyosema hata moja.

Matendo ya Mitume 8:25 Acts 8:25

Nao walipokwisha kushuhudia na kulihubiri neno la Bwana wakarudi Yerusalemu, wakaihubiri Injili katika vijiji vingi vya Wasamaria.

Matendo ya Mitume 8:26 Acts 8:26

Malaika wa Bwana akasema na Filipo, akamwambia, Ondoka ukaende upande wa kusini hata njia ile itelemkayo kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa.

Matendo ya Mitume 8:27 Acts 8:27

Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu,

Matendo ya Mitume 8:28 Acts 8:28

akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya.

Matendo ya Mitume 8:29 Acts 8:29

Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo.

Matendo ya Mitume 8:30 Acts 8:30

Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma?

Matendo ya Mitume 8:31 Acts 8:31

Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye.

Matendo ya Mitume 8:32 Acts 8:32

Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake.

Matendo ya Mitume 8:33 Acts 8:33

Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi.

Matendo ya Mitume 8:34 Acts 8:34

Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine?

Matendo ya Mitume 8:35 Acts 8:35

Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu.

Matendo ya Mitume 8:36 Acts 8:36

Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?

Matendo ya Mitume 8:37 Acts 8:37

Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.]

Matendo ya Mitume 8:38 Acts 8:38

Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza.

Matendo ya Mitume 8:39 Acts 8:39

Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi.

Matendo ya Mitume 8:40 Acts 8:40

Lakini Filipo akaonekana katika Azoto, na alipokuwa akipita akahubiri Injili katika miji yote, hata akafika Kaisaria.