Matendo ya Mitume Mlango 16 Acts

Matendo ya Mitume 16:1 Acts 16:1

Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Myunani.

Matendo ya Mitume 16:2 Acts 16:2

Mtu huyo alishuhudiwa vema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio.

Matendo ya Mitume 16:3 Acts 16:3

Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni Myunani.

Matendo ya Mitume 16:4 Acts 16:4

Basi walipokuwa wakipita kati ya miji ile, wakawapa zile amri zilizoamriwa na mitume na wazee walioko Yerusalemu, ili wazishike.

Matendo ya Mitume 16:5 Acts 16:5

Makanisa yakatiwa nguvu katika ile Imani, hesabu yao ikaongezeka kila siku.

Matendo ya Mitume 16:6 Acts 16:6

Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia.

Matendo ya Mitume 16:7 Acts 16:7

Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa,

Matendo ya Mitume 16:8 Acts 16:8

wakapita Misia wakatelemkia Troa.

Matendo ya Mitume 16:9 Acts 16:9

Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie.

Matendo ya Mitume 16:10 Acts 16:10

Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari Njema.

Matendo ya Mitume 16:11 Acts 16:11

Basi tukang'oa nanga kutoka Troa, tukafika Samothrake kwa tanga moja, na siku ya pili tukafika Neapoli;

Matendo ya Mitume 16:12 Acts 16:12

na kutoka hapo tukafika Filipi, mji wa Makedonia, mji ulio mkuu katika jimbo lile, mahali walipohamia Warumi; tukawa katika mji huu, tukikaa siku kadha wa kadha.

Matendo ya Mitume 16:13 Acts 16:13

Hata siku ya sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale.

Matendo ya Mitume 16:14 Acts 16:14

Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo.

Matendo ya Mitume 16:15 Acts 16:15

Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, Kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatushurutisha.

Matendo ya Mitume 16:16 Acts 16:16

Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua.

Matendo ya Mitume 16:17 Acts 16:17

Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu.

Matendo ya Mitume 16:18 Acts 16:18

Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.

Matendo ya Mitume 16:19 Acts 16:19

Basi bwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limewapotea, wakawakamata Paulo na Sila, wakawakokota mpaka sokoni mbele ya wakuu wa mji;

Matendo ya Mitume 16:20 Acts 16:20

wakawachukua kwa makadhi, wakasema, Watu hawa wanachafua sana mji wetu, nao ni Wayahudi;

Matendo ya Mitume 16:21 Acts 16:21

tena wanatangaza habari ya desturi zisizokuwa halali kwetu kuzipokea wala kuzifuata, kwa kuwa sisi tu Warumi.

Matendo ya Mitume 16:22 Acts 16:22

Makutano wote wakaondoka wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora.

Matendo ya Mitume 16:23 Acts 16:23

Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana.

Matendo ya Mitume 16:24 Acts 16:24

Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale.

Matendo ya Mitume 16:25 Acts 16:25

Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.

Matendo ya Mitume 16:26 Acts 16:26

Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa.

Matendo ya Mitume 16:27 Acts 16:27

Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia.

Matendo ya Mitume 16:28 Acts 16:28

Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa.

Matendo ya Mitume 16:29 Acts 16:29

Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila;

Matendo ya Mitume 16:30 Acts 16:30

kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka?

Matendo ya Mitume 16:31 Acts 16:31

Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.

Matendo ya Mitume 16:32 Acts 16:32

Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake.

Matendo ya Mitume 16:33 Acts 16:33

Akawakaribisha saa ile ile ya usiku, akawaosha mapigo yao, kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati uo huo.

Matendo ya Mitume 16:34 Acts 16:34

Akawaleta juu nyumbani kwake, akawaandalia chakula, akafurahi sana, yeye na nyumba yake yote, maana amekwisha kumwamini Mungu.

Matendo ya Mitume 16:35 Acts 16:35

Kulipopambauka makadhi wakawatuma wakubwa wa askari wakisema, Waacheni watu wale waende zao.

Matendo ya Mitume 16:36 Acts 16:36

Yule mlinzi wa gereza akamwarifu Paulo maneno haya akisema, Makadhi wametuma watu ili mfunguliwe; basi, sasa tokeni nje, enendeni zenu kwa amani.

Matendo ya Mitume 16:37 Acts 16:37

Paulo akawaambia, Wametupiga mbele ya watu wote bila kutuhukumu, na sisi tu Warumi, tena wametutupa gerezani; na sasa wanataka kututoa kwa siri? Sivyo, lakini na waje wenyewe wakatutoe.

Matendo ya Mitume 16:38 Acts 16:38

Wakubwa wa askari wakawapasha makadhi habari za maneno haya; nao wakaogopa, waliposikia ya kwamba hao ni Warumi.

Matendo ya Mitume 16:39 Acts 16:39

Wakaja wakawasihi; na walipokwisha kuwatoa nje, wakawaomba watoke katika mji ule.

Matendo ya Mitume 16:40 Acts 16:40

Nao wakatoka gerezani wakaingia nyumbani mwa Lidia; na walipokwisha kuonana na ndugu wakawafariji, wakaenda zao.