Matendo ya Mitume Mlango 22 Acts

Matendo ya Mitume 22:1 Acts 22:1

Enyi wanaume, ndugu zangu na baba zangu, nisikilizeni, nikijitetea mbele yenu sasa.

Matendo ya Mitume 22:2 Acts 22:2

Waliposikia kwamba anasema nao kwa lugha ya Kiebrania wakazidi kunyamaza; akasema,

Matendo ya Mitume 22:3 Acts 22:3

Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi;

Matendo ya Mitume 22:4 Acts 22:4

nikawaudhi watu wa Njia hii hata kuwaua, nikawafunga, nikiwatia gerezani, wanaume na wanawake.

Matendo ya Mitume 22:5 Acts 22:5

Kama Kuhani Mkuu naye anishuhudiavyo, na wazee wa baraza wote pia, ambao nalipokea barua kwao kuwapelekea ndugu wale, nikaenda Dameski, ili niwalete wale waliokuwa huko hata Yerusalemu, hali wamefungwa, ili waadhibiwe.

Matendo ya Mitume 22:6 Acts 22:6

Ikawa nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote.

Matendo ya Mitume 22:7 Acts 22:7

Nikaanguka nchi, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi?

Matendo ya Mitume 22:8 Acts 22:8

Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi.

Matendo ya Mitume 22:9 Acts 22:9

Na wale waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti ya yule aliyesema nami.

Matendo ya Mitume 22:10 Acts 22:10

Nikasema, Nifanye nini, Bwana? Bwana akaniambia, Simama, uingie Dameski, na huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye.

Matendo ya Mitume 22:11 Acts 22:11

Na nilipokuwa sioni kwa sababu ya fahari ya nuru ile, nikaongozwa na mikono yao waliokuwa pamoja nami, nikaingia Dameski.

Matendo ya Mitume 22:12 Acts 22:12

Basi mtu mmoja, Anania, mtauwa kwa kuifuata sheria, aliyeshuhudiwa wema na Wayahudi wote waliokaa huko,

Matendo ya Mitume 22:13 Acts 22:13

Akanijia, akasimama karibu nami, akaniambia, Ndugu yangu Sauli, uone. Nikamwinulia macho yangu saa ile ile.

Matendo ya Mitume 22:14 Acts 22:14

Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule Mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake.

Matendo ya Mitume 22:15 Acts 22:15

Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia.

Matendo ya Mitume 22:16 Acts 22:16

Basi sasa, unakawilia nini? Simama, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake.

Matendo ya Mitume 22:17 Acts 22:17

Ikawa nilipokwisha kurudi Yerusalemu, nilipokuwa nikisali ndani ya hekalu, nikawa hali ya kuzimia roho,

Matendo ya Mitume 22:18 Acts 22:18

nikamwona, naye akiniambia, Hima, utoke Yerusalemu upesi, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako katika habari zangu.

Matendo ya Mitume 22:19 Acts 22:19

Nami nikasema, Bwana, wanajua hao ya kuwa mimi nalikuwa nikiwafunga gerezani wale wanaokuamini na kuwapiga katika kila sinagogi.

Matendo ya Mitume 22:20 Acts 22:20

Na damu ya Stefano shahidi wako ilipomwagwa, mimi nami nilikuwa nikisimama karibu, nikikubali, na kuzitunza nguo zao waliomwua.

Matendo ya Mitume 22:21 Acts 22:21

Naye akaniambia, Enenda zako; kwa kuwa mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa Mataifa.

Matendo ya Mitume 22:22 Acts 22:22

Wakamsikiliza mpaka neno lile, wakapaza sauti zao, wakisema, Mwondoe huyu katika nchi, kwa maana haifai aishi.

Matendo ya Mitume 22:23 Acts 22:23

Walipokuwa wakipiga kelele na kutupa mavazi yao na kurusha-rusha mavumbi juu,

Matendo ya Mitume 22:24 Acts 22:24

yule jemadari akaamuru aletwe ndani ya ngome, akisema aulizwe habari zake kwa kupigwa mijeledi, ili ajue sababu hata wakampigia kelele namna hii.

Matendo ya Mitume 22:25 Acts 22:25

Hata walipokwisha kumfunga kwa kamba, Paulo akamwambia yule akida aliyesimama karibu, Je! Ni halali ninyi kumpiga mtu aliye Mrumi naye hajakuhumiwa bado?

Matendo ya Mitume 22:26 Acts 22:26

Yule akida aliposikia, akaenda akamwarifu yule jemadari, akisema, Unataka kufanya nini? Kwa maana mtu huyu ni Mrumi.

Matendo ya Mitume 22:27 Acts 22:27

Jemadari akaja, akamwuliza, Niambie, u Mrumi? Akasema, Ndiyo.

Matendo ya Mitume 22:28 Acts 22:28

Jemadari akajibu, Mimi nalipata wenyeji huu kwa mali nyingi. Paulo akasema, Na mimi ni Mrumi wa kuzaliwa.

Matendo ya Mitume 22:29 Acts 22:29

Basi wale waliokuwa tayari kumwuliza wakaondoka wakamwacha. Na yule jemadari naye akaogopa, alipojua ya kuwa ni Mrumi, na kwa sababu amemfunga.

Matendo ya Mitume 22:30 Acts 22:30

Siku ya pili yake akitaka kujua hakika, ni kwa sababu gani ameshitakiwa na Wayahudi, akamfungua, akawaamuru wakuu wa makuhani na baraza yote wakutane. Akamleta Paulo chini, akamweka mbele yao.