Kutoka Mlango 19 Exodus

Kutoka 19:1 Exodus 19:1

Mwezi wa tatu baada ya kutoka Waisraeli katika nchi ya Misri, siku iyo hiyo wakafika jangwa la Sinai.

Kutoka 19:2 Exodus 19:2

Nao walipokuwa wameondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile jangwa; Israeli wakapiga kambi huko wakiukabili mlima.

Kutoka 19:3 Exodus 19:3

Musa akapanda kwa Mungu, na Bwana akamwita toka mlima ule, akisema, Utawaambia nyumba ya Yakobo, na kuwaarifu wana wa Israeli, maneno haya;

Kutoka 19:4 Exodus 19:4

Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta ninyi kwangu mimi.

Kutoka 19:5 Exodus 19:5

Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu,

Kutoka 19:6 Exodus 19:6

nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli.

Kutoka 19:7 Exodus 19:7

Musa akaenda akawaita wazee wa watu, akawafunulia maneno hayo yote, Bwana aliyokuwa amemwagiza.

Kutoka 19:8 Exodus 19:8

Watu wote wakaitika pamoja wakisema, Hayo yote aliyoyasema Bwana tutayatenda. Naye Musa akamwambia Bwana maneno ya hao watu.

Kutoka 19:9 Exodus 19:9

Bwana akamwambia Musa, Tazama, mimi naja kwako katika wingu zito ili watu hawa wasikie nitakaposema nawe, nao wapate kukuamini wewe nawe hata milele. Musa akamwambia Bwana hayo maneno ya watu.

Kutoka 19:10 Exodus 19:10

Bwana akamwambia Musa, Enenda kwa watu hawa, ukawatakase leo na kesho, wakazifue nguo zao,

Kutoka 19:11 Exodus 19:11

wawe tayari kwa siku ya tatu; maana siku ya tatu Bwana atashuka katika mlima wa Sinai machoni pa watu hawa wote.

Kutoka 19:12 Exodus 19:12

Nawe utawawekea mipaka watu hawa pande zote, ukisema, Jihadharini, msipande mlima huu, wala msiuguse, hata mapambizo yake; kila mtu atakayeugusa mlima huu, bila shaka atauawa.

Kutoka 19:13 Exodus 19:13

Mkono wa mtu awaye yote usimguse mtu huyo, ila hakika yake atapigwa kwa mawe, au kupigwa kwa mkuki; kwamba ni mnyama au kwamba ni mwanadamu, hataishi. Hapo panda itakapotoa sauti kwa kufuliza ndipo watakapoukaribia mlima.

Kutoka 19:14 Exodus 19:14

Musa akatelemka mlimani akawaendea watu akawatakasa, nao wakafua nguo zao.

Kutoka 19:15 Exodus 19:15

Akawaambia watu; Mwe tayari siku ya tatu; msimkaribie mwanamke.

Kutoka 19:16 Exodus 19:16

Ikawa siku ya tatu, wakati wa asubuhi, palikuwa na ngurumo na umeme, na wingu zito juu ya mlima, na sauti ya baragumu iliyolia sana. Watu wote waliokuwa kituoni wakatetemeka.

Kutoka 19:17 Exodus 19:17

Musa akawatoa hao watu katika kituo, akawaleta ili waonane na Mungu; wakasimama pande za chini za kile kilima.

Kutoka 19:18 Exodus 19:18

Mlima wa Sinai wote pia ukatoa moshi, kwa sababu Bwana alishuka katika moto; na ule moshi wake ukapanda juu kama moshi wa tanuu, mlima wote ukatetemeka sana.

Kutoka 19:19 Exodus 19:19

Na hapo sauti ya baragumu ilipozidi kulia sana, Musa akanena, naye Mungu akamwitikia kwa sauti.

Kutoka 19:20 Exodus 19:20

Bwana akaushukia mlima, juu ya kilele cha mlima; Bwana akamwita Musa aende hata kilele cha mlima; Musa akapanda juu.

Kutoka 19:21 Exodus 19:21

Ndipo Bwana akamwambia Musa, Shuka chini, uwaonye watu wasije wakapasua njia waje kwa Bwana kutazama, kisha wengi miongoni mwao wakaangamia.

Kutoka 19:22 Exodus 19:22

Makuhani nao, wamkaribiao Bwana, na wajitakase, Bwana asije akawafurikia.

Kutoka 19:23 Exodus 19:23

Musa akamwambia Bwana, Watu hawa hawawezi kuukaribia mlima wa Sinai; kwa kuwa wewe ulituusia, ukisema, Wekeni mipaka kando-kando ya mlima, na kuutenga.

Kutoka 19:24 Exodus 19:24

Bwana akamwambia, Nenda, ushuke wewe; nawe utakwea, wewe, na Haruni pamoja nawe; lakini wale makuhani na watu wasipenye kumkaribia Bwana, asije yeye akawafurikia juu yao.

Kutoka 19:25 Exodus 19:25

Basi Musa akawatelemkia hao watu na kuwaambia hayo.