Kutoka Mlango 2 Exodus

Kutoka 2:1 Exodus 2:1

Mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaondoka akaoa binti mmoja wa Lawi.

Kutoka 2:2 Exodus 2:2

Yule mwanamke akachukua mimba akazaa mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu.

Kutoka 2:3 Exodus 2:3

Na alipokuwa hawezi kumficha tena, akampatia kisafina cha manyasi akakipaka sifa na lami, akamtia mtoto ndani yake, akakiweka katika majani kando ya mto.

Kutoka 2:4 Exodus 2:4

Umbu lake mtoto akasimama mbali ili ajue yatakayompata.

Kutoka 2:5 Exodus 2:5

Basi binti Farao akashuka, aoge mtoni, na vijakazi wake wakatembea kando ya mto; naye akakiona kile kisafina katika majani, akamtuma kijakazi wake kwenda kukileta.

Kutoka 2:6 Exodus 2:6

Akakifungua, akamwona mtoto, na tazama, mtoto yule analia. Basi akamhurumia, akasema, Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania.

Kutoka 2:7 Exodus 2:7

Basi umbu lake mtoto akamwambia binti Farao, Je! Niende nikamwite mlezi katika wanawake wa Kiebrania, aje kwako, akunyonyeshee mtoto huyu?

Kutoka 2:8 Exodus 2:8

Binti Farao akamwambia, Haya! Enenda. Yule kijana akaenda akamwita mama yake yule mtoto.

Kutoka 2:9 Exodus 2:9

Binti Farao akamwambia, Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee, nami nitakupa mshahara wako. Yule mwanamke akamtwaa mtoto, akamnyonyesha.

Kutoka 2:10 Exodus 2:10

Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa, akasema, Ni kwa sababu nalimtoa majini.

Kutoka 2:11 Exodus 2:11

Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo wa ndugu zake.

Kutoka 2:12 Exodus 2:12

Basi akatazama huko na huko, na alipoona ya kuwa hapana mtu, akampiga Mmisri yule, akamficha ndani ya mchanga.

Kutoka 2:13 Exodus 2:13

Akatoka siku ya pili, na tazama, watu wawili wa Waebrania walikuwa wakipigana. Akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake, Mbona unampiga mwenzako?

Kutoka 2:14 Exodus 2:14

Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana.

Kutoka 2:15 Exodus 2:15

Basi Farao alipopata habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima.

Kutoka 2:16 Exodus 2:16

Basi kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza birika maji, wapate kunywesha kundi la baba yao.

Kutoka 2:17 Exodus 2:17

Wachungaji wakaja wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia, akalinywesha kundi lao.

Kutoka 2:18 Exodus 2:18

Walipofika kwa Reueli baba yao, akasema, Imekuwaje hata mkarejea mapema leo?

Kutoka 2:19 Exodus 2:19

Wakasema, Mmisri mmoja alituokoa katika mikono ya wachungaji, tena zaidi ya hayo, akatutekea maji, akalinywesha kundi.

Kutoka 2:20 Exodus 2:20

Akawaambia binti zake, Yuko wapi basi? Mbona mmemwacha mtu huyo? Mwiteni, ale chakula.

Kutoka 2:21 Exodus 2:21

Musa akawa radhi kukaa kwake mtu yule, naye akampa Musa binti yake, Sipora.

Kutoka 2:22 Exodus 2:22

Huyo akamzalia mwana, akamwita jina lake Gershomu, maana alisema, Nimekuwa mgeni katika nchi ya ugeni.

Kutoka 2:23 Exodus 2:23

Hata baada ya siku zile nyingi mfalme wa Misri akafa; wana wa Israeli wakaugua kwa sababu ya ule utumwa, wakalia; kilio chao kikafika juu kwa Mungu kwa sababu ya ule utumwa.

Kutoka 2:24 Exodus 2:24

Mungu akasikia kuugua kwao, Mungu akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo.

Kutoka 2:25 Exodus 2:25

Mungu akawaona wana wa Israeli, na Mungu akawaangalia.