Kutoka Mlango 33 Exodus

Kutoka 33:1 Exodus 33:1

Bwana akanena na Musa, Haya, ondokeni, katokeni hapo, wewe na hao watu uliowaleta wakwee kutoka nchi ya Misri, waende nchi hiyo niliyomwapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, niliposema, Nitakipa kizazi chako nchi hii;

Kutoka 33:2 Exodus 33:2

nami nitamtuma malaika aende mbele yako; nami nitawafukuza Mkanaani, na Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi;

Kutoka 33:3 Exodus 33:3

waifikilie nchi imiminikayo maziwa na asali; kwa maana mimi sitakwenda kati yenu; kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu; nisiwaangamize ninyi katika njia.

Kutoka 33:4 Exodus 33:4

Watu waliposikia habari hizo mbaya wakaomboleza wala hapana mtu aliyevaa vyombo vyake vya uzuri.

Kutoka 33:5 Exodus 33:5

Bwana akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli, Ninyi ni watu wenye shingo ngumu; kama mimi nikiingia kati yenu dakika moja, nitawaangamiza; basi sasa vueni vyombo vyenu vya uzuri ili nipate kujua nitakalowatenda.

Kutoka 33:6 Exodus 33:6

Basi wana wa Israeli wakavua vyombo vyao vyote vya uzuri, tangu mlima wa Horebu na mbele.

Kutoka 33:7 Exodus 33:7

Basi desturi ya Musa, ilikuwa kuitwaa ile hema, na kuikita nje ya marago mbali na hayo marago; akaiita, hema ya kukutania. Hata kila mtu aliyekuwa akitaka neno kwa Bwana, akatoka, akaenda hata hema ya kukutania, iliyokuwa nje ya marago.

Kutoka 33:8 Exodus 33:8

Hata Musa alipotoka kuiendea ile hema, watu wote waliondoka wakasimama, kila mtu mlangoni pa hema yake, akamtazama Musa, hata alipokwisha kuingia hemani.

Kutoka 33:9 Exodus 33:9

Ikawa Musa alipoingia humo hemani, ile nguzo ya wingu ikashuka, ikasimama mlangoni pa ile hema; naye Bwana akasema na Musa.

Kutoka 33:10 Exodus 33:10

Watu wote wakaiona nguzo ya wingu ikisimama penye mlango wa hema; watu wote wakaondoka wakasujudu, kila mtu mlangoni pa hema yake.

Kutoka 33:11 Exodus 33:11

Naye Bwana akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani.

Kutoka 33:12 Exodus 33:12

Musa akamwambia Bwana, Angalia, wewe waniambia, Wachukue watu hawa; nawe hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Walakini umesema, Nakujua jina lako, nawe umepata neema mbele zangu.

Kutoka 33:13 Exodus 33:13

Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako.

Kutoka 33:14 Exodus 33:14

Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha.

Kutoka 33:15 Exodus 33:15

Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa.

Kutoka 33:16 Exodus 33:16

Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi?

Kutoka 33:17 Exodus 33:17

Bwana akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako.

Kutoka 33:18 Exodus 33:18

Akasema, Nakusihi unionyeshe utukufu wako.

Kutoka 33:19 Exodus 33:19

Akasema, Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza jina la Bwana mbele yako; nami nitamfadhili yeye nitakayemfadhili; nitamrehemu yeye nitakayemrehemu.

Kutoka 33:20 Exodus 33:20

Kisha akasema, Huwezi kuniona uso wangu, maana mwanadamu hataniona akaishi.

Kutoka 33:21 Exodus 33:21

Bwana akasema, Tazama, hapa pana mahali karibu nami, nawe utasimama juu ya mwamba;

Kutoka 33:22 Exodus 33:22

kisha itakuwa wakati unapopita utukufu wangu, nitakutia katika ufa wa ule mwamba, na kukufunika kwa mkono wangu hata nitakapokuwa nimekwisha kupita;

Kutoka 33:23 Exodus 33:23

nami nitaondoa mkono wangu, nawe utaniona nyuma yangu, bali uso wangu hautaonekana.