Kutoka Mlango 15 Exodus

Kutoka 15:1 Exodus 15:1

Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia Bwana wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.

Kutoka 15:2 Exodus 15:2

Bwana ni nguvu zangu, na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu. Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu; Ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.

Kutoka 15:3 Exodus 15:3

Bwana ni mtu wa vita, Bwana ndilo jina lake.

Kutoka 15:4 Exodus 15:4

Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini, Maakida yake wateule wamezama katika bahari ya Shamu.

Kutoka 15:5 Exodus 15:5

Vilindi vimewafunikiza, Walizama vilindini kama jiwe.

Kutoka 15:6 Exodus 15:6

Bwana, mkono wako wa kuume umepata fahari ya uwezo, Bwana, mkono wako wa kuume wawaseta-seta adui.

Kutoka 15:7 Exodus 15:7

Kwa wingi wa ukuu wako wawaangusha chini wanaokuondokea, Wapeleka hasira yako, nayo huwateketeza kama mabua makavu.

Kutoka 15:8 Exodus 15:8

Kwa upepo wa mianzi ya pua yako maji yalipandishwa, Mawimbi yakasimama juu wima mfano wa chungu, Vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari.

Kutoka 15:9 Exodus 15:9

Adui akasema, Nitafuatia, nitapata, nitagawanya nyara, Nafsi yangu itashibishwa na wao; Nitaufuta upanga wangu, mkono wangu utawaangamiza.

Kutoka 15:10 Exodus 15:10

Ulivuma kwa upepo wako, bahari ikawafunikiza; Wakazama kama risasi ndani ya maji makuu.

Kutoka 15:11 Exodus 15:11

Ee Bwana, katika miungu ni nani aliye kama wewe? Ni nani aliye kama wewe, mtukufu katika utakatifu, Mwenye kuogopwa katika sifa zako, mfanya maajabu?

Kutoka 15:12 Exodus 15:12

Ulinyosha mkono wako wa kuume, Nchi ikawameza.

Kutoka 15:13 Exodus 15:13

Wewe kwa rehema zako umewaongoza watu uliowakomboa, Kwa uweza wako uliwaelekeza hata makao yako matakatifu.

Kutoka 15:14 Exodus 15:14

Kabila za watu wamesikia, wanatetemeka, Wakaao Ufilisti utungu umewashika.

Kutoka 15:15 Exodus 15:15

Ndipo majumbe wa Edomu wakashangaa, Watu wa Moabu wenye nguvu tetemeko limewapata, Watu wote wakaao Kanaani wameyeyuka.

Kutoka 15:16 Exodus 15:16

Hofu na woga umewaangukia; Kwa uweza wa mkono wako wanakaa kimya kama jiwe; Hata watakapovuka watu wako, Ee Bwana, Hata watakapovuka watu wako uliowanunua.

Kutoka 15:17 Exodus 15:17

Utawaingiza, na kuwapanda katika mlima wa urithi wako, Mahali pale ulipojifanyia, Ee Bwana, ili upakae, Pale patakatifu ulipopaweka imara, Bwana, kwa mikono yako.

Kutoka 15:18 Exodus 15:18

Bwana atatawala milele na milele.

Kutoka 15:19 Exodus 15:19

Kwa maana farasi za Farao na magari yake na wapanda farasi wake waliingia ndani ya bahari, Bwana akayarudisha maji ya bahari juu yao; bali wana wa Israeli walikwenda katika nchi kavu katikati ya bahari.

Kutoka 15:20 Exodus 15:20

Na Miriamu, nabii mke, ndugu yake Haruni, akatwaa tari mkononi mwake; wanawake wakatoka wote wakaenda nyuma yake, wenye matari na kucheza.

Kutoka 15:21 Exodus 15:21

Miriamu akawaitikia,Mwimbieni Bwana ,kwa maana ametukuka sana;Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.

Kutoka 15:22 Exodus 15:22

Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani wasione maji.

Kutoka 15:23 Exodus 15:23

Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara.

Kutoka 15:24 Exodus 15:24

Ndipo watu wakamnung'unikia Musa, wakisema, Tunywe nini?

Kutoka 15:25 Exodus 15:25

Naye akamlilia Bwana; Bwana akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko;

Kutoka 15:26 Exodus 15:26

akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye.

Kutoka 15:27 Exodus 15:27

Wakafikilia Elimu, palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na mitende sabini; wakapanga hapo, karibu na maji.