Kutoka Mlango 39 Exodus

Kutoka 39:1 Exodus 39:1

Na zile nyuzi za rangi ya samawi, na nyuzi za rangi ya zambarau, na nyekundu, wakafanya mavazi yaliyofumwa kwa ustadi sana kwa ajili ya kutumika katika mahali patakatifu, na kuyafanya hayo mavazi matakatifu ya Haruni, vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa.

Kutoka 39:2 Exodus 39:2

Naye akaifanya hiyo naivera, ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa.

Kutoka 39:3 Exodus 39:3

Nao wakaifua hiyo dhahabu hata ikawa mabamba membamba sana, kisha wakaikata iwe nyuzi, ili wapate kuifuma pamoja na hizo nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyuzi nyekundu na za kitani nzuri, kazi ya fundi stadi sana.

Kutoka 39:4 Exodus 39:4

Nao wakafanya na vipande vya mabegani kwa ajili yake, vilivyoungwa pamoja; viliungwa pamoja kwa ncha zake mbili.

Kutoka 39:5 Exodus 39:5

Na huo mshipi wa kazi ya werevu, uliokuwa juu yake ili kuifunga mahali pake; ulikuwa wa kitu kimoja, na wa kazi moja na naivera ya dhahabu, na rangi ya samawi, na rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa; vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa.

Kutoka 39:6 Exodus 39:6

Nao wakavitengeza vile vito vya shohamu, vilivyotiwa katika vijalizo vya dhahabu, vilivyochorwa mfano wa kuchora kwake muhuri, kwa majina ya hao wana wa Israeli.

Kutoka 39:7 Exodus 39:7

Naye akavitia katika vile vipande vya mabegani vya hiyo naivera, viwe vito vya ukumbusho kwa wana wa Israeli, kama Bwana alivyomwagiza Musa.

Kutoka 39:8 Exodus 39:8

Naye akafanya kile kifuko cha kifuani, kazi ya fundi stadi, kama hiyo kazi ya naivera; ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa.

Kutoka 39:9 Exodus 39:9

Kilikuwa mraba; wakakifanya kile kifuko cha kifuani kwa kukikunja; urefu wake ulikuwa shibiri, na upana wake ulikuwa shibiri, tena kilikuwa ni cha kukunjwa.

Kutoka 39:10 Exodus 39:10

Nao wakatia safu nne za vito ndani yake, safu moja ilikuwa ni akiki, na yakuti ya rangi ya manjano, na baharamani, vilikuwa ni safu ya kwanza.

Kutoka 39:11 Exodus 39:11

Na safu ya pili ilikuwa zumaridi, na yakuti samawi, na almasi.

Kutoka 39:12 Exodus 39:12

Na safu ya tatu ilikuwa ni hiakintho, na akiki nyekundu, na amethisto.

Kutoka 39:13 Exodus 39:13

Na safu ya nne ilikuwa ni zabarajadi, na shohamu, na yaspi: vito hivyo vilikuwa vimetiwa katika vijalizo vya dhahabu, kila kimoja mahali pake.

Kutoka 39:14 Exodus 39:14

Na hivyo vito vilikuwa vyaandama majina ya wana wa Israeli, kumi na mawili, sawasawa na majina yao; mfano wa kuchora muhuri, kila moja kwa jina lake, kwa zile kabila kumi na mbili.

Kutoka 39:15 Exodus 39:15

Nao wakafanya katika kile kifuko cha kifuani mikufu mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa ya dhahabu safi.

Kutoka 39:16 Exodus 39:16

Nao wakafanya vijalizo viwili vya dhahabu, na pete mbili za dhahabu; nao wakazitia hizo pete mbili katika ncha mbili za hicho kifuko.

Kutoka 39:17 Exodus 39:17

Nao wakaitia hiyo mikufu miwili iliyosokotwa katika hizo pete mbili zilizokuwa katika ncha mbili za hicho kifuko.

Kutoka 39:18 Exodus 39:18

Na ncha hizo mbili nyingine, za hiyo mikufu miwili ya kusokotwa, wakazitia katika vile vijalizo viwili, na kuvitia katika vile vipande vya mabegani vya naivera, upande wa mbele.

Kutoka 39:19 Exodus 39:19

Nao wakafanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika ncha mbili za kifuko cha kifuani, katika ukingo wake, ulio upande wa naivera ulio ndani.

Kutoka 39:20 Exodus 39:20

Nao wakafanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika vile vipande viwili vya ile naivera chini yake, upande wa mbele, karibu na kifungo chake, juu ya huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi.

Kutoka 39:21 Exodus 39:21

Nao wakakikaza kile kifuko kwa pete zake kwenye naivera kwa ukanda wa rangi ya samawi, ili kikae pale juu ya mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi, na ya kwamba kifuko cha kifuani kisiachane na naivera; vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa.

Kutoka 39:22 Exodus 39:22

Naye akafanya hiyo joho ya naivera ya kazi ya kusuka, rangi ya samawi yote;

Kutoka 39:23 Exodus 39:23

na hilo tundu lililokuwa katikati yake, mfano wa tundu lililo katika kanzu ya chuma, na utepe wake kulizunguka hilo tundu, ili lisipasuke.

Kutoka 39:24 Exodus 39:24

Nao wakatia katika upindo wa joho makomamanga ya nyuzi za rangi ya samawi, na rangi ya zambarau, na rangi nyekundu, na kitani iliyosokotwa.

Kutoka 39:25 Exodus 39:25

Nao wakafanya njuga za dhahabu safi, na kuzitia hizo njuga kati ya hayo makomamanga pande zote, kati ya hayo makomamanga;

Kutoka 39:26 Exodus 39:26

njuga na komamanga, njuga na komamanga katika pindo za joho kuizunguka pande zote, ili kutumika kwa hiyo; vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa.

Kutoka 39:27 Exodus 39:27

Nao wakafanya hizo kanzu za nguo ya kitani nzuri ya kufumwa, kwa Haruni, na kwa wanawe

Kutoka 39:28 Exodus 39:28

na hicho kilemba cha nguo ya kitani nzuri, na zile kofia nzuri za kitani, na hizo suruali za nguo ya kitani nzuri iliyosokotwa,

Kutoka 39:29 Exodus 39:29

na huo mshipi wa nguo nzuri ya kitani iliyosokotwa, na rangi ya samawi, na rangi ya zambarau, na nyekundu, kazi ya fundi mwenye kutia taraza; vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa.

Kutoka 39:30 Exodus 39:30

Nao wakafanya hilo bamba la hiyo taji takatifu la dhahabu safi, na kuandika juu yake andiko, mfano wa kuchorwa kwa muhuri, MTAKATIFU KWA Bwana.

Kutoka 39:31 Exodus 39:31

Nao wakatia ukanda wa rangi ya samawi ili kulifunga katika hicho kilemba upande wa juu; vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa.

Kutoka 39:32 Exodus 39:32

Basi ndivyo ilivyomalizwa kazi yote ya maskani ya hema ya kukutania; na wana wa Israeli walifanya kama yote Bwana aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyofanya.

Kutoka 39:33 Exodus 39:33

Nao wakamletea Musa hiyo maskani; yaani Hema, na vyombo vyake vyote, vifungo vyake, na mbao zake, na mataruma yake, na nguzo zake, na matako yake;

Kutoka 39:34 Exodus 39:34

na kifuniko chake cha ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na kifuniko cha ngozi za pomboo, na pazia la sitara;

Kutoka 39:35 Exodus 39:35

na sanduku la ushuhuda, na miti yake, na kiti cha rehema;

Kutoka 39:36 Exodus 39:36

na meza, na vyombo vyake vyote, na mikate ya wonyesho;

Kutoka 39:37 Exodus 39:37

na kinara cha taa safi, na taa zake, hizo taa za kuwekwa mahali pake, na vyombo vyake vyote, na mafuta ya taa,

Kutoka 39:38 Exodus 39:38

na madhabahu ya dhahabu, na mafuta ya kutiwa, na uvumba mzuri, na pazia kwa mlango wa hema;

Kutoka 39:39 Exodus 39:39

na madhabahu ya shaba, na wavu wake wa shaba, na miti yake, na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake;

Kutoka 39:40 Exodus 39:40

na ukuta wa nguo wa ua, na nguzo zake na matako yake, na pazia la lango la ua, na kamba zake, na vigingi vyake, na vyombo vyote vya kutumiwa katika utumishi wa maskani, kwa hiyo hema ya kukutania,

Kutoka 39:41 Exodus 39:41

na mavazi ya kazi nzuri kwa utumishi katika mahali patakatifu, na mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani.

Kutoka 39:42 Exodus 39:42

Sawasawa na yote Bwana aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyoifanya hiyo kazi yote wana wa Israeli.

Kutoka 39:43 Exodus 39:43

Musa akaiona hiyo kazi yote, na tazama, walikuwa wameimaliza; vile vile kama Bwana alivyoagiza, walikuwa wameifanya vivyo; basi Musa akawaombea heri.