Kutoka Mlango 3 Exodus

Kutoka 3:1 Exodus 3:1

Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu.

Kutoka 3:2 Exodus 3:2

Malaika wa Bwana akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea.

Kutoka 3:3 Exodus 3:3

Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei.

Kutoka 3:4 Exodus 3:4

Bwana alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa.

Kutoka 3:5 Exodus 3:5

Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu.

Kutoka 3:6 Exodus 3:6

Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu.

Kutoka 3:7 Exodus 3:7

Bwana akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao;

Kutoka 3:8 Exodus 3:8

nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi.

Kutoka 3:9 Exodus 3:9

Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa.

Kutoka 3:10 Exodus 3:10

Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri.

Kutoka 3:11 Exodus 3:11

Musa akamwambia Mungu, Mimi ni nani, hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri?

Kutoka 3:12 Exodus 3:12

Akasema, Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe; na dalili ya kuwa nimekutuma ndiyo hii; utakapokuwa umekwisha kuwatoa hao watu katika Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu.

Kutoka 3:13 Exodus 3:13

Musa akamwambia Mungu, Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza, Jina lake n'nani? Niwaambie nini?

Kutoka 3:14 Exodus 3:14

Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO;akasema,Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli;MIMI NIKO amenituma kwenu.

Kutoka 3:15 Exodus 3:15

Tena Mungu akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli maneno haya, Bwana, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote.

Kutoka 3:16 Exodus 3:16

Enenda, ukawakusanye wazee wa Israeli pamoja, ukawaambie, Bwana, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenitokea, akaniambia, Hakika nimewajilieni, tena nimeyaona mnayotendewa huko Misri;

Kutoka 3:17 Exodus 3:17

Nami nimesema, Nitawapandisha kutoka katika mateso ya Misri na kuwaingiza katika nchi ya Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, nchi ijaayo maziwa na asali.

Kutoka 3:18 Exodus 3:18

Nao watakusikia sauti yako; nawe utakwenda, wewe na wazee wa Israeli kwa mfalme wa Misri, na kumwambia, Bwana Mungu wa Waebrania, amekutana nasi; basi sasa twakuomba, tupe ruhusa twende mwendo siku tatu jangwani, ili tumtolee dhabihu Bwana Mungu wetu.

Kutoka 3:19 Exodus 3:19

Nami najua ya kuwa huyo mfalme wa Misri hatawapa ruhusa mwende zenu, la, hata kwa mkono wa nguvu.

Kutoka 3:20 Exodus 3:20

Nami nitaunyosha mkono wangu, na kuipiga Misri kwa ajabu zangu zote, nitakazofanya kati yake, kisha baadaye atawapa ruhusa kwenda.

Kutoka 3:21 Exodus 3:21

Nami nitawapa watu hao kufadhiliwa mbele ya Wamisri; hata itakuwa, hapo mtakapokwenda zenu hamtakwenda kitupu;

Kutoka 3:22 Exodus 3:22

Lakini kila mwanamke ataomba kwa jirani, na kwa huyo akaaye naye nyumbani, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi; nanyi mtawavika wana wenu na binti zenu; nanyi mtawateka nyara Wamisri.