Yohana Mlango 10 John

Yohana 10:1 John 10:1

Yesu aliwaambia, Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang'anyi.

Yohana 10:2 John 10:2

Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo.

Yohana 10:3 John 10:3

Bawabu humfungulia huyo, na kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kwa majina yao, na kuwapeleka nje.

Yohana 10:4 John 10:4

Naye awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake.

Yohana 10:5 John 10:5

Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za wageni.

Yohana 10:6 John 10:6

Mithali hiyo Yesu aliwaambia, lakini wao hawakuelewa na mambo hayo aliyowaambia.

Yohana 10:7 John 10:7

Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo.

Yohana 10:8 John 10:8

Wote walionitangulia ni wevi na wanyang'anyi; lakini kondoo hawakuwasikia.

Yohana 10:9 John 10:9

Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho.

Yohana 10:10 John 10:10

Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.

Yohana 10:11 John 10:11

Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.

Yohana 10:12 John 10:12

Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya.

Yohana 10:13 John 10:13

Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake.

Yohana 10:14 John 10:14

Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi;

Yohana 10:15 John 10:15

kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.

Yohana 10:16 John 10:16

Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.

Yohana 10:17 John 10:17

Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena.

Yohana 10:18 John 10:18

Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu.

Yohana 10:19 John 10:19

Kukaingia tena matengano kati ya Wayahudi, kwa ajili ya maneno hayo.

Yohana 10:20 John 10:20

Wengi wao wakasema, Ana pepo huyu, tena ana wazimu; mbona mnamsikiliza?

Yohana 10:21 John 10:21

Wengine wakasema, Maneno hayo siyo ya mtu mwenye pepo. Je! Pepo aweza kuwafumbua macho vipofu?

Yohana 10:22 John 10:22

Basi huko Yerusalemu ilikuwa Sikukuu ya Kutabaruku; ni wakati wa baridi.

Yohana 10:23 John 10:23

Naye Yesu alikuwa akitembea hekaluni, katika ukumbi wa Sulemani.

Yohana 10:24 John 10:24

Basi Wayahudi walimzunguka, wakamwambia, Hata lini utatuhangaisha nafsi zetu? Kama wewe ndiwe Kristo, utuambie waziwazi.

Yohana 10:25 John 10:25

Yesu akawajibu, Naliwaambia, lakini ninyi hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo zinazonishuhudia.

Yohana 10:26 John 10:26

Lakini ninyi hamsadiki, kwa sababu hammo miongoni mwa kondoo wangu.

Yohana 10:27 John 10:27

Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata.

Yohana 10:28 John 10:28

Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu.

Yohana 10:29 John 10:29

Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu.

Yohana 10:30 John 10:30

Mimi na Baba tu umoja.

Yohana 10:31 John 10:31

Basi Wayahudi wakaokota mawe tena ili wampige.

Yohana 10:32 John 10:32

Yesu akawajibu, Kazi njema nyingi nimewaonyesha, zitokazo kwa Baba; kwa ajili ya kazi ipi katika hizo mnanipiga kwa mawe?

Yohana 10:33 John 10:33

Wayahudi wakamjibu, Kwa ajili ya kazi njema hatukupigi kwa mawe; bali kwa kukufuru, na kwa sababu wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu.

Yohana 10:34 John 10:34

Yesu akawajibu, Je! Haikuandikwa katika torati yenu ya kwamba, Mimi nimesema, Ndinyi miungu?

Yohana 10:35 John 10:35

Ikiwa aliwaita miungu wale waliojiliwa na neno la Mungu; (na maandiko hayawezi kutanguka);

Yohana 10:36 John 10:36

je! Yeye ambaye Baba alimtakasa, akamtuma ulimwenguni, ninyi mnamwambia, Unakufuru; kwa sababu nalisema, Mimi ni Mwana wa Mungu?

Yohana 10:37 John 10:37

Kama sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini;

Yohana 10:38 John 10:38

lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba.

Yohana 10:39 John 10:39

Wakatafuta tena kumkamata; lakini akatoka mikononi mwao.

Yohana 10:40 John 10:40

Akaenda zake tena ng'ambo ya Yordani, mpaka mahali pale alipokuwapo Yohana akibatiza hapo kwanza, akakaa huko.

Yohana 10:41 John 10:41

Na watu wengi wakamwendea, wakasema, Yohana kweli hakufanya ishara yo yote, lakini yote aliyoyasema Yohana katika habari zake huyu yalikuwa kweli.

Yohana 10:42 John 10:42

Nao wengi wakamwamini huko.