Yohana Mlango 9 John

Yohana 9:1 John 9:1

Hata alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa.

Yohana 9:2 John 9:2

Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu?

Yohana 9:3 John 9:3

Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake.

Yohana 9:4 John 9:4

Imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana, usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi.

Yohana 9:5 John 9:5

Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.

Yohana 9:6 John 9:6

Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho,

Yohana 9:7 John 9:7

akamwambia, Nenda kanawe katika birika ya Siloamu, (maana yake, Aliyetumwa). Basi akaenda na kunawa; akarudi anaona.

Yohana 9:8 John 9:8

Basi jirani zake, na wale waliomwona zamani kuwa ni mwombaji, wakasema, Je! Huyu siye yule aliyekuwa akiketi na kuomba?

Yohana 9:9 John 9:9

Wengine wakasema, Ndiye. Wengine wakasema, La, lakini amefanana naye. Yeye mwenyewe alisema, Mimi ndiye.

Yohana 9:10 John 9:10

Basi wakamwambia, Macho yako yalifumbuliwaje?

Yohana 9:11 John 9:11

Yeye akajibu, Mtu yule aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka macho akaniambia, Nenda Siloamu ukanawe; basi nikaenda na kunawa, nikapata kuona.

Yohana 9:12 John 9:12

Wakamwambia, Yuko wapi huyo? Akasema, Mimi sijui.

Yohana 9:13 John 9:13

Basi wakampeleka kwa Mafarisayo yule aliyekuwa kipofu zamani.

Yohana 9:14 John 9:14

Nayo ilikuwa sabato, hapo Yesu alipofanya zile tope na kumfumbua macho.

Yohana 9:15 John 9:15

Basi Mafarisayo nao wakamwuliza tena jinsi gani alivyopata kuona. Akawaambia, Alinitia tope juu ya macho, nami nikanawa, na sasa naona.

Yohana 9:16 John 9:16

Basi baadhi ya Mafarisayo wakasema, Mtu huyo hakutoka kwa Mungu, kwa sababu haishiki sabato. Wengine wakasema, Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya ishara kama hizo? Kukawa matengano kati yao.

Yohana 9:17 John 9:17

Basi wakamwambia yule kipofu mara ya pili, Wewe wasemaje katika habari zake kwa vile alivyokufumbua macho? Akasema, Ni nabii.

Yohana 9:18 John 9:18

Basi Wayahudi hawakusadiki habari zake, ya kuwa alikuwa kipofu, kisha akapata kuona; hata walipowaita wazazi wake yule aliyepata kuona.

Yohana 9:19 John 9:19

Wakawauliza wakisema, Huyu ndiye mwana wenu, ambaye mnasema kwamba alizaliwa kipofu? Amepataje, basi, kuona sasa?

Yohana 9:20 John 9:20

Wazazi wake wakawajibu, wakasema, Tunajua ya kuwa huyu ndiye mwana wetu, tena ya kuwa alizaliwa kipofu;

Yohana 9:21 John 9:21

lakini jinsi aonavyo sasa hatujui; wala hatujui ni nani aliyemfumbua macho. Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima; atajisemea mwenyewe.

Yohana 9:22 John 9:22

Wazazi wake waliyasema hayo kwa sababu waliwaogopa Wayahudi; kwa maana Wayahudi walikuwa wamekwisha kuafikiana kwamba mtu akimkiri kuwa ni Kristo, atatengwa na sinagogi.

Yohana 9:23 John 9:23

Ndiyo sababu wale wazazi wake walisema, Ni mtu mzima, mwulizeni yeye.

Yohana 9:24 John 9:24

Basi mara ya pili wakamwita yule mtu aliyekuwa kipofu, wakamwambia, Mpe Mungu utukufu. Sisi tunajua ya kuwa mtu huyo ni mwenye dhambi.

Yohana 9:25 John 9:25

Basi yule mtu akajibu, Kwamba yeye ni mwenye dhambi sijui. Najua neno moja, kuwa mimi nalikuwa kipofu na sasa naona.

Yohana 9:26 John 9:26

Basi wakamwambia, Alikutendea nini? Alikufumbua macho jinsi gani?

Yohana 9:27 John 9:27

Akawajibu, Nimekwisha kuwaambia, wala hamkusikia; mbona mnataka kusikia tena? Ninyi nanyi mnataka kuwa wanafunzi wake?

Yohana 9:28 John 9:28

Basi wakamshutumu, wakasema, Wewe u mwanafunzi wake yule; sisi tu wanafunzi wa Musa.

Yohana 9:29 John 9:29

Sisi tunajua ya kuwa Mungu alisema na Musa; bali yule hatujui atokako.

Yohana 9:30 John 9:30

Yule mtu akajibu, akawaambia, Hii ni ajabu! Kwamba ninyi hamjui atokako, naye alinifumbua macho!

Yohana 9:31 John 9:31

Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na kuyafanya mapenzi yake, humsikia huyo.

Yohana 9:32 John 9:32

Tokea hapo haijasikiwa ya kuwa mtu ameyafumbua macho ya kipofu, ambaye alizaliwa hali hiyo.

Yohana 9:33 John 9:33

Kama huyo asingalitoka kwa Mungu, asingeweza kutenda neno lo lote.

Yohana 9:34 John 9:34

Wakajibu, wakamwambia, Ama! Wewe ulizaliwa katika dhambi tupu, nawe unatufundisha sisi? Wakamtoa nje.

Yohana 9:35 John 9:35

Yesu akasikia kwamba wamemtoa nje; naye alipomwona alisema, Wewe wamwamini Mwana wa Mungu?

Yohana 9:36 John 9:36

Naye akajibu akasema, Ni nani, Bwana, nipate kumwamini?

Yohana 9:37 John 9:37

Yesu akamwambia, Umemwona, naye anayesema nawe ndiye.

Yohana 9:38 John 9:38

Akasema, Naamini, Bwana. Akamsujudia.

Yohana 9:39 John 9:39

Yesu akasema, Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ili wao wasioona waone, nao wanaoona wawe vipofu.

Yohana 9:40 John 9:40

Baadhi ya Mafarisayo waliokuwapo pamoja naye wakasikia hayo, wakamwambia, Je! Sisi nasi tu vipofu?

Yohana 9:41 John 9:41

Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa.