Yohana Mlango 16 John

Yohana 16:1 John 16:1

Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa.

Yohana 16:2 John 16:2

Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada.

Yohana 16:3 John 16:3

Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi.

Yohana 16:4 John 16:4

Lakini nimewaambia hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia. Sikuwaambia hayo tangu mwanzo, kwa sababu nalikuwapo pamoja nanyi.

Yohana 16:5 John 16:5

Lakini sasa mimi naenda zangu kwake yeye aliyenipeleka, wala hakuna mmoja wenu aniulizaye, Unakwendapi?

Yohana 16:6 John 16:6

Ila kwa sababu nimewaambia hayo huzuni imejaa mioyoni mwenu.

Yohana 16:7 John 16:7

Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu.

Yohana 16:8 John 16:8

Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.

Yohana 16:9 John 16:9

Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi;

Yohana 16:10 John 16:10

kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena;

Yohana 16:11 John 16:11

kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.

Yohana 16:12 John 16:12

Hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa.

Yohana 16:13 John 16:13

Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.

Yohana 16:14 John 16:14

Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.

Yohana 16:15 John 16:15

Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari.

Yohana 16:16 John 16:16

Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni; na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona.

Yohana 16:17 John 16:17

Basi baadhi ya wanafunzi wake wakasemezana, Neno gani hilo asemalo, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona? Na hilo, Kwa sababu naenda zangu kwa Baba?

Yohana 16:18 John 16:18

Basi walisema, Neno gani hilo asemalo; hilo, Bado kitambo kidogo? Hatujui asemalo.

Yohana 16:19 John 16:19

Yesu alifahamu ya kwamba wanataka kumwuliza, akawaambia, Ndilo hilo mnaloulizana, ya kuwa nalisema, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona?

Yohana 16:20 John 16:20

Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.

Yohana 16:21 John 16:21

Mwanamke azaapo, yuna huzuni kwa kuwa saa yake imefika; lakini akiisha kuzaa mwana, haikumbuki tena ile dhiki, kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtu ulimwenguni.

Yohana 16:22 John 16:22

Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye.

Yohana 16:23 John 16:23

Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu.

Yohana 16:24 John 16:24

Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu.

Yohana 16:25 John 16:25

Hayo nimesema nanyi kwa mithali; saa yaja ambapo sitasema nanyi tena kwa mithali, lakini nitawapa waziwazi habari ya Baba.

Yohana 16:26 John 16:26

Na siku ile mtaomba kwa jina langu, wala siwaambii ya kwamba mimi nitawaombea kwa Baba;

Yohana 16:27 John 16:27

kwa maana Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba.

Yohana 16:28 John 16:28

Nalitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena nauacha ulimwengu; na kwenda kwa Baba.

Yohana 16:29 John 16:29

Basi wanafunzi wake wakasema, Tazama, sasa wasema waziwazi, wala huneni mithali yo yote.

Yohana 16:30 John 16:30

Sasa tumejua ya kuwa wewe wafahamu mambo yote, wala huna haja ya mtu akuulize; kwa hiyo twasadiki ya kwamba ulitoka kwa Mungu.

Yohana 16:31 John 16:31

Yesu akawajibu, Je! Mnasadiki sasa?

Yohana 16:32 John 16:32

Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu; walakini mimi si peke yangu, kwa kuwa Baba yupo pamoja nami.

Yohana 16:33 John 16:33

Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.