Yohana Mlango 8 John

Yohana 8:1 John 8:1

[Walikwenda kila mtu nyumbani kwake; naye Yesu akaenda mpaka mlima wa Mizeituni.

Yohana 8:2 John 8:2

Hata asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; naye akaketi, akawa akiwafundisha.

Yohana 8:3 John 8:3

Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati.

Yohana 8:4 John 8:4

Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini.

Yohana 8:5 John 8:5

Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje?

Yohana 8:6 John 8:6

Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi.

Yohana 8:7 John 8:7

Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe.

Yohana 8:8 John 8:8

Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi.

Yohana 8:9 John 8:9

Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati.

Yohana 8:10 John 8:10

Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Je! Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia?

Yohana 8:11 John 8:11

Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.]

Yohana 8:12 John 8:12

Basi Yesu akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.

Yohana 8:13 John 8:13

Basi Mafarisayo wakamwambia, Wewe unajishuhudia mwenyewe; ushuhuda wako si kweli.

Yohana 8:14 John 8:14

Yesu akajibu, akawaambia, Mimi ningawa ninajishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ndio kweli; kwa sababu najua nilikotoka na niendako; lakini ninyi hamjui nilikotoka wala niendako.

Yohana 8:15 John 8:15

Ninyi mwahukumu kwa kufuata mambo ya mwili; mimi simhukumu mtu.

Yohana 8:16 John 8:16

Nami nijapohukumu, hukumu yangu ni kweli; kwa kuwa mimi si peke yangu, bali ni mimi na yeye aliyenipeleka.

Yohana 8:17 John 8:17

Tena katika torati yenu imeandikwa kwamba, Ushuhuda wa watu wawili ni kweli.

Yohana 8:18 John 8:18

Mimi ndimi ninayejishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenipeleka ananishuhudia.

Yohana 8:19 John 8:19

Basi wakamwambia, Yuko wapi Baba yako? Yesu akajibu, Mimi hamnijui, wala Baba yangu hammjui; kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba yangu.

Yohana 8:20 John 8:20

Maneno hayo aliyasema alipokuwa akifundisha hekaluni, katika chumba cha hazina; wala hakuna mtu aliyemkamata, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado.

Yohana 8:21 John 8:21

Basi akawaambia tena, Mimi naondoka, nanyi mtanitafuta; nanyi mtakufa katika dhambi yenu; mimi niendako ninyi hamwezi kuja.

Yohana 8:22 John 8:22

Basi Wayahudi wakasema, Je! Atajiua! Kwa kuwa asema, Mimi niendako ninyi hamwezi kuja?

Yohana 8:23 John 8:23

Akawaambia, Ninyi ni wa chini, mimi ni wa juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu.

Yohana 8:24 John 8:24

Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu.

Yohana 8:25 John 8:25

Basi wakamwambia, U nani wewe? Yesu akawaambia, Hasa neno lilo hilo ninalowaambia.

Yohana 8:26 John 8:26

Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu; lakini yeye aliyenipeleka ni kweli, nami niliyoyasikia kwake, ndiyo ninenayo katika ulimwengu.

Yohana 8:27 John 8:27

Wala hawakutambua ya kuwa anawatajia Baba.

Yohana 8:28 John 8:28

Basi Yesu akawaambia, Mtakapokuwa mmekwisha kumwinua Mwana wa Adamu, ndipo mtakapofahamu ya kuwa mimi ndiye; na ya kuwa sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila kama Baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo.

Yohana 8:29 John 8:29

Naye aliyenipeleka yu pamoja nami, hakuniacha peke yangu; kwa sababu nafanya sikuzote yale yampendezayo.

Yohana 8:30 John 8:30

Naye alipokuwa akisema hayo, wengi walimwamini.

Yohana 8:31 John 8:31

Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli;

Yohana 8:32 John 8:32

tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.

Yohana 8:33 John 8:33

Wakamjibu, Sisi tu uzao wake Ibrahimu, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wo wote; nawe wasemaje, Mtawekwa huru?

Yohana 8:34 John 8:34

Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.

Yohana 8:35 John 8:35

Wala mtumwa hakai nyumbani sikuzote; mwana hukaa sikuzote.

Yohana 8:36 John 8:36

Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.

Yohana 8:37 John 8:37

Najua ya kuwa ninyi ni uzao wa Ibrahimu lakini mnatafuta kuniua kwa sababu neno langu halimo ndani yenu.

Yohana 8:38 John 8:38

Niliyoyaona kwa Baba ndiyo niyanenayo; nanyi vivyo hivyo mliyoyasikia kwa baba yenu ndiyo myatendayo.

Yohana 8:39 John 8:39

Wakajibu, wakamwambia, Baba yetu ndiye Ibrahimu! Yesu akawaambia, Kama mngekuwa watoto wa Ibrahimu, mngezitenda kazi zake Ibrahimu.

Yohana 8:40 John 8:40

Lakini sasa mnatafuta kuniua mimi, mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli, niliyoisikia kwa Mungu. Ibrahimu hakufanya hivyo.

Yohana 8:41 John 8:41

Ninyi mnazitenda kazi za baba yenu. Ndipo walipomwambia, Sisi hatukuzaliwa kwa zinaa; sisi tunaye Baba mmoja, yaani, Mungu.

Yohana 8:42 John 8:42

Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma.

Yohana 8:43 John 8:43

Mbona hamyafahamu hayo niyasemayo? Ni kwa sababu ninyi hamwezi kulisikia neno langu.

Yohana 8:44 John 8:44

Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.

Yohana 8:45 John 8:45

Nami, kwa sababu nasema iliyo kweli, hamnisadiki.

Yohana 8:46 John 8:46

Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi? Nami nikisema kweli, mbona ninyi hamnisadiki?

Yohana 8:47 John 8:47

Yeye aliye wa Mungu huyasikia maneno ya Mungu; hivyo ninyi hamsikii kwa sababu ninyi si wa Mungu.

Yohana 8:48 John 8:48

Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Je! Sisi hatusemi vema ya kwamba wewe u Msamaria, nawe una pepo?

Yohana 8:49 John 8:49

Yesu akajibu, Mimi sina pepo; lakini mimi namheshimu Baba yangu, na ninyi mwanivunjia heshima yangu.

Yohana 8:50 John 8:50

Wala mimi siutafuti utukufu wangu; yuko mwenye kutafuta na kuhukumu.

Yohana 8:51 John 8:51

Amin, amin, nawaambia, Mtu akilishika neno langu, hataona mauti milele.

Yohana 8:52 John 8:52

Basi Wayahudi wakamwambia, Sasa tumeng'amua ya kuwa una pepo. Ibrahimu amekufa, na manabii wamekufa; nawe wasema, Mtu akilishika neno langu, hataonja mauti milele.

Yohana 8:53 John 8:53

Wewe u mkuu kuliko baba yetu Ibrahimu, ambaye amekufa? Nao manabii wamekufa. Wajifanya u nani?

Yohana 8:54 John 8:54

Yesu akajibu, Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu; anitukuzaye ni Baba yangu, ambaye ninyi mwanena kuwa ni Mungu wenu.

Yohana 8:55 John 8:55

Wala ninyi hamkumjua; lakini mimi namjua. Nikisema ya kwamba simjui, nitakuwa mwongo kama ninyi; lakini namjua, na neno lake nalishika.

Yohana 8:56 John 8:56

Ibrahimu, baba yenu, alishangilia kwa vile atakavyoiona siku yangu; naye akaiona, akafurahi.

Yohana 8:57 John 8:57

Basi Wayahudi wakamwambia, Wewe hujapata bado miaka hamsini, nawe umemwona Ibrahimu?

Yohana 8:58 John 8:58

Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko.

Yohana 8:59 John 8:59

Basi wakaokota mawe ili wamtupie; lakini Yesu akajificha, akatoka hekaluni.