Yohana Mlango 18 John

Yohana 18:1 John 18:1

Alipokwisha kusema hayo, Yesu alitoka pamoja na wanafunzi wake kwenda ng'ambo ya kijito Kedroni, palipokuwapo bustani; akaingia yeye na wanafunzi wake.

Yohana 18:2 John 18:2

Naye Yuda, yule aliyetaka kumsaliti, alipajua mahali pale; kwa sababu Yesu alikuwa akienda huko mara nyingi pamoja na wanafunzi wake.

Yohana 18:3 John 18:3

Basi Yuda, akiisha kupokea kikosi cha askari na watumishi waliotoka kwa wakuu wa makuhani na Mafarisayo, akaenda huko na taa na mienge na silaha.

Yohana 18:4 John 18:4

Basi Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawaambia, Ni nani mnayemtafuta?

Yohana 18:5 John 18:5

Wao wakamjibu, Ni Yesu Mnazareti. Yesu akawaambia, Ni mimi. Yuda naye aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao.

Yohana 18:6 John 18:6

Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini.

Yohana 18:7 John 18:7

Basi akawauliza tena, Mnamtafuta nani? Wakasema, Yesu Mnazareti.

Yohana 18:8 John 18:8

Yesu akajibu, Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi; basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.

Yohana 18:9 John 18:9

Ili litimizwe lile neno alilolisema, Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja wao.

Yohana 18:10 John 18:10

Basi Simoni Petro alikuwa na upanga, akaufuta, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. Na yule mtumwa jina lake ni Malko.

Yohana 18:11 John 18:11

Basi Yesu akamwambia Petro, Rudisha upanga alani mwake; je! Kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee?

Yohana 18:12 John 18:12

Basi wale askari na yule jemadari na wale watumishi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga.

Yohana 18:13 John 18:13

Wakamchukua kwa Anasi kwanza; maana alikuwa mkwewe Kayafa, yule aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule.

Yohana 18:14 John 18:14

Naye Kayafa ndiye yule aliyewapa Wayahudi lile shauri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu.

Yohana 18:15 John 18:15

Wakamfuata Yesu, Petro na mwanafunzi mwingine. Na mwanafunzi huyo alikuwa amejulikana na Kuhani Mkuu, akaingia pamoja na Yesu katika behewa ya Kuhani Mkuu.

Yohana 18:16 John 18:16

Lakini Petro akasimama nje mlangoni. Basi yule mwanafunzi mwingine aliyejulikana na Kuhani Mkuu akatoka, akasema na mngoja mlango, akamleta Petro ndani.

Yohana 18:17 John 18:17

Basi yule kijakazi, aliyekuwa mngoja mlango, akamwambia Petro, Wewe nawe, je! Hu mwanafunzi mmojawapo wa mtu huyu? Naye akasema, Si mimi.

Yohana 18:18 John 18:18

Na wale watumwa na watumishi walikuwa wakisimama, wamefanya moto wa makaa; maana ilikuwa baridi; wakawa wakikota moto. Petro naye alikuwapo pamoja nao, anakota moto.

Yohana 18:19 John 18:19

Basi Kuhani Mkuu akamwuliza Yesu habari za wanafunzi wake, na habari za mafundisho yake.

Yohana 18:20 John 18:20

Yesu akamjibu, Mimi nimesema na ulimwengu waziwazi; sikuzote nalifundisha katika sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo Wayahudi wote; wala kwa siri mimi sikusema neno lo lote.

Yohana 18:21 John 18:21

Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena.

Yohana 18:22 John 18:22

Basi aliposema hayo, mtumishi mmojawapo aliyesimama karibu alimpiga Yesu kofi akisema, Wamjibu hivi Kuhani Mkuu?

Yohana 18:23 John 18:23

Yesu akamjibu, Kama nimesema vibaya, ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini?

Yohana 18:24 John 18:24

Basi Anasi akampeleka hali amefungwa kwa Kayafa, Kuhani Mkuu.

Yohana 18:25 John 18:25

Na Simoni Petro alikuwa akisimama huko, anakota moto. Basi wakamwambia, Wewe nawe, je! Hu mwanafunzi wake mmojawapo? Naye akakana, akasema, Si mimi.

Yohana 18:26 John 18:26

Mtumwa mmojawapo wa Kuhani Mkuu, naye ni jamaa yake yule aliyekatwa sikio na Petro, akasema, Je! Mimi sikukuona wewe bustanini pamoja naye?

Yohana 18:27 John 18:27

Basi Petro akakana tena, na mara akawika jimbi.

Yohana 18:28 John 18:28

Kisha wakamchukua Yesu kutoka kwa Kayafa mpaka Praitorio, nayo ikawa alfajiri;lakini wao wenyewe hawakuingia ndani ya ile praitorio,wasije wakanajisika,bali wapate kuila Pasaka.

Yohana 18:29 John 18:29

Basi Pilato akawatokea nje, akasema, Ni mashitaka gani mnayoleta juu ya mtu huyu?

Yohana 18:30 John 18:30

Wakajibu, wakamwambia, Kama huyu asingekuwa mtenda mabaya, tusingemleta kwako.

Yohana 18:31 John 18:31

Basi Pilato akawaambia, Haya! Mtwaeni ninyi, mkamhukumu kwa ile torati yenu! Wayahudi wakamwambia, Sisi hatuna ruhusa ya kuua mtu.

Yohana 18:32 John 18:32

Ili litimie lile neno lake Yesu alilolisema, akionyesha ni mauti gani atakayokufa.

Yohana 18:33 John 18:33

Basi Pilato akaingia tena ndani ya Praitorio, akamwita Yesu, akamwambia, Je! Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?

Yohana 18:34 John 18:34

Yesu akamjibu, Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu?

Yohana 18:35 John 18:35

Pilato akajibu, Ama! Ni Myahudi mimi! Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta kwangu. Umefanya nini?

Yohana 18:36 John 18:36

Yesu akajibu, Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa.

Yohana 18:37 John 18:37

Basi Pilato akamwambia, Wewe u mfalme basi? Yesu akajibu, Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu.

Yohana 18:38 John 18:38

Pilato akamwambia, Kweli ni nini? Naye akiisha kusema neno hilo akawatokea Wayahudi tena, akawaambia, Mimi sioni hatia yo yote kwake.

Yohana 18:39 John 18:39

Lakini kwenu kuna desturi ya mimi kuwafungulia mtu mmoja wakati wa Pasaka; basi, mwapenda niwafungulie Mfalme wa Wayahudi?

Yohana 18:40 John 18:40

Basi wakapiga kelele tena kusema, Si huyu, bali Baraba. Naye yule Baraba alikuwa mnyang'anyi.