Yohana Mlango 4 John

Yohana 4:1 John 4:1

Kwa hiyo Bwana, alipofahamu ya kuwa Mafarisayo wamesikia ya kwamba, Yesu anafanya wanafunzi wengi kuliko Yohana, na kuwabatiza,

Yohana 4:2 John 4:2

(lakini Yesu mwenyewe hakubatiza, bali wanafunzi wake,)

Yohana 4:3 John 4:3

aliacha Uyahudi, akaenda zake tena mpaka Galilaya.

Yohana 4:4 John 4:4

Naye alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria.

Yohana 4:5 John 4:5

Basi akafika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe.

Yohana 4:6 John 4:6

Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita.

Yohana 4:7 John 4:7

Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe.

Yohana 4:8 John 4:8

Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula.

Yohana 4:9 John 4:9

Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.)

Yohana 4:10 John 4:10

Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai.

Yohana 4:11 John 4:11

Yule mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai?

Yohana 4:12 John 4:12

Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake?

Yohana 4:13 John 4:13

Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena;

Yohana 4:14 John 4:14

walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.

Yohana 4:15 John 4:15

Yule mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka.

Yohana 4:16 John 4:16

Yesu akamwambia, Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa.

Yohana 4:17 John 4:17

Yule mwanamke akajibu, akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume;

Yohana 4:18 John 4:18

kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo umesema kweli.

Yohana 4:19 John 4:19

Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii!

Yohana 4:20 John 4:20

Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.

Yohana 4:21 John 4:21

Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu.

Yohana 4:22 John 4:22

Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi.

Yohana 4:23 John 4:23

Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.

Yohana 4:24 John 4:24

Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.

Yohana 4:25 John 4:25

Yule mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masihi, (aitwaye Kristo); naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote.

Yohana 4:26 John 4:26

Yesu akamwambia, Mimi ninayesema nawe, ndiye.

Yohana 4:27 John 4:27

Mara hiyo wakaja wanafunzi wake, wakastaajabu kwa sababu alikuwa akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, Unatafuta nini? Au, Mbona unasema naye?

Yohana 4:28 John 4:28

Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akawaambia watu,

Yohana 4:29 John 4:29

Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?

Yohana 4:30 John 4:30

Basi wakatoka mjini, wakamwendea.

Yohana 4:31 John 4:31

Huko nyuma wanafunzi wakamsihi wakisema, Rabi, ule.

Yohana 4:32 John 4:32

Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi.

Yohana 4:33 John 4:33

Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je! Mtu amemletea chakula?

Yohana 4:34 John 4:34

Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake.

Yohana 4:35 John 4:35

Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yaja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno.

Yohana 4:36 John 4:36

Naye avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja.

Yohana 4:37 John 4:37

Kwa maana hapo neno hilo huwa kweli, Mmoja hupanda akavuna mwingine.

Yohana 4:38 John 4:38

Mimi naliwatuma myavune yale msiyoyataabikia; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao.

Yohana 4:39 John 4:39

Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke, aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda.

Yohana 4:40 John 4:40

Basi wale Wasamaria walipomwendea, walimsihi akae kwao; naye akakaa huko siku mbili.

Yohana 4:41 John 4:41

Watu wengi zaidi wakaamini kwa sababu ya neno lake.

Yohana 4:42 John 4:42

Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu.

Yohana 4:43 John 4:43

Na baada ya siku mbili hizo akaondoka huko, akaenda Galilaya.

Yohana 4:44 John 4:44

Kwa maana Yesu mwenyewe alishuhudia ya kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe.

Yohana 4:45 John 4:45

Basi alipotoka Galilaya, Wagalilaya walimpokea; kwa kuwa wameyaona mambo yote aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu; maana hao nao waliiendea sikukuu.

Yohana 4:46 John 4:46

Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na diwani mmoja ambaye mwanawe hawezi huko Kapernaumu.

Yohana 4:47 John 4:47

Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Uyahudi mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na kumponya mwanawe; kwa maana alikuwa kufani.

Yohana 4:48 John 4:48

Basi Yesu akamwambia, Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa?

Yohana 4:49 John 4:49

Yule diwani akamwambia, Bwana, ushuke asijakufa mtoto wangu.

Yohana 4:50 John 4:50

Yesu akamwambia, Enenda; mwanao yu hai. Mtu yule akalisadiki lile neno aliloambiwa na Yesu, naye akashika njia.

Yohana 4:51 John 4:51

Hata alipokuwa akishuka, watumwa wake walimlaki, wakisema ya kwamba mtoto wake yu hai.

Yohana 4:52 John 4:52

Basi akawauliza habari ya saa alipoanza kuwa hajambo; nao wakamwambia, Jana, saa saba, homa ilimwacha.

Yohana 4:53 John 4:53

Basi babaye akafahamu ya kuwa ni saa ile ile aliyoambiwa na Yesu, Mwanao yu hai. Akaamini yeye na wote wa nyumbani mwake.

Yohana 4:54 John 4:54

Hiyo ni ishara ya pili aliyoifanya Yesu, alipokuwa ametoka Uyahudi kufika Galilaya.