Marko Mlango 4 Mark

Marko 4:1 Mark 4:1

Akaanza kufundisha tena kando ya bahari. Wakamkusanyikia mkutano mkubwa mno, hata yeye akapanda chomboni, akakaa baharini, mkutano wote ulikuwako juu ya nchi kavu kando ya bahari.

Marko 4:2 Mark 4:2

Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, akawaambia katika mafundisho yake,

Marko 4:3 Mark 4:3

Sikilizeni; Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda;

Marko 4:4 Mark 4:4

ikawa alipokuwa akipanda, mbegu nyingine ilianguka kando ya njia, wakaja ndege wakaila.

Marko 4:5 Mark 4:5

Nyingine ikaanguka penye mwamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara ikaota kwa kuwa na udongo haba;

Marko 4:6 Mark 4:6

hata jua lilipozuka iliungua, na kwa kuwa haina mizizi ikanyauka.

Marko 4:7 Mark 4:7

Nyingine ikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea ikaisonga, isizae matunda.

Marko 4:8 Mark 4:8

Nyingine zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia.

Marko 4:9 Mark 4:9

Akasema, Aliye na masikio ya kusikilia, na asikie.

Marko 4:10 Mark 4:10

Naye alipokuwa peke yake, wale watu waliomzunguka, na wale Thenashara, walimwuliza habari za ile mifano.

Marko 4:11 Mark 4:11

Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, bali kwa wale walio nje yote hufanywa kwa mifano,

Marko 4:12 Mark 4:12

ili wakitazama watazame, wasione; Na wakisikia wasikie, wasielewe; Wasije wakaongoka, na kusamehewa.

Marko 4:13 Mark 4:13

Akawaambia, Hamjui mfano huu? Basi mifano yote mtaitambuaje?

Marko 4:14 Mark 4:14

Mpanzi huyo hulipanda neno.

Marko 4:15 Mark 4:15

Hawa ndio walio kando ya njia lipandwapo neno; nao, wakiisha kusikia, mara huja Shetani, akaliondoa lile neno lililopandwa mioyoni mwao.

Marko 4:16 Mark 4:16

Kadhalika na hawa ndio wapandwao penye miamba, ambao kwamba wakiisha kulisikia lile neno, mara hulipokea kwa furaha;

Marko 4:17 Mark 4:17

ila hawana mizizi ndani yao, bali hudumu muda mchache; kisha ikitokea dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara hujikwaa.

Marko 4:18 Mark 4:18

Na hawa ndio wale wapandwao penye miiba; ni watu walisikiao lile neno,

Marko 4:19 Mark 4:19

na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno, likawa halizai.

Marko 4:20 Mark 4:20

Na hawa ndio waliopandwa penye udongo ulio mzuri; ni watu walisikiao lile neno na kulipokea, na kuzaa matunda, mmoja thelathini, mmoja sitini, na mmoja mia.

Marko 4:21 Mark 4:21

Akawaambia, Mwaonaje? Taa huja ili kuwekwa chini ya pishi, au mvunguni? Si kuwekwa juu ya kiango?

Marko 4:22 Mark 4:22

Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila makusudi lije likadhihirika; wala hakuna lililofichwa, ila makusudi lije likatokea wazi.

Marko 4:23 Mark 4:23

Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.

Marko 4:24 Mark 4:24

Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa.

Marko 4:25 Mark 4:25

Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa.

Marko 4:26 Mark 4:26

Akasema, Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi;

Marko 4:27 Mark 4:27

akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye.

Marko 4:28 Mark 4:28

Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke.

Marko 4:29 Mark 4:29

Hata matunda yakiiva, mara atapeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika.

Marko 4:30 Mark 4:30

Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? Au tuutie katika mfano gani?

Marko 4:31 Mark 4:31

Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi,

Marko 4:32 Mark 4:32

lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake.

Marko 4:33 Mark 4:33

Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia;

Marko 4:34 Mark 4:34

wala pasipo mfano hakusema nao; lakini akawaeleza wanafunzi wake mwenyewe mambo yote kwa faragha.

Marko 4:35 Mark 4:35

Siku ile kulipokuwa jioni, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng'ambo.

Marko 4:36 Mark 4:36

Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye.

Marko 4:37 Mark 4:37

Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji.

Marko 4:38 Mark 4:38

Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?

Marko 4:39 Mark 4:39

Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu.

Marko 4:40 Mark 4:40

Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?

Marko 4:41 Mark 4:41

Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?