Marko Mlango 1 Mark

Marko 1:1 Mark 1:1

Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.

Marko 1:2 Mark 1:2

Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako.

Marko 1:3 Mark 1:3

Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake.

Marko 1:4 Mark 1:4

Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi.

Marko 1:5 Mark 1:5

Wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto wa Yordani, wakiziungama dhambi zao.

Marko 1:6 Mark 1:6

Na Yohana alikuwa amevaa singa za ngamia na mshipi wa ngozi kiunoni mwake, akala nzige na asali ya mwitu.

Marko 1:7 Mark 1:7

Akahubiri akisema, Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake.

Marko 1:8 Mark 1:8

Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.

Marko 1:9 Mark 1:9

Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani.

Marko 1:10 Mark 1:10

Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake;

Marko 1:11 Mark 1:11

na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.

Marko 1:12 Mark 1:12

Mara Roho akamtoa aende nyikani.

Marko 1:13 Mark 1:13

Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia.

Marko 1:14 Mark 1:14

Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu,

Marko 1:15 Mark 1:15

akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.

Marko 1:16 Mark 1:16

Naye alipokuwa akipita kando ya bahari ya Galilaya, akamwona Simoni na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi.

Marko 1:17 Mark 1:17

Yesu akawaambia, Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.

Marko 1:18 Mark 1:18

Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.

Marko 1:19 Mark 1:19

Akaendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, nao pia walikuwa chomboni, wakizitengeneza nyavu zao.

Marko 1:20 Mark 1:20

Mara akawaita, wakamwacha baba yao Zebedayo ndani ya chombo pamoja na watu wa mshahara, wakaenda, wakamfuata.

Marko 1:21 Mark 1:21

Wakashika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha.

Marko 1:22 Mark 1:22

Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi.

Marko 1:23 Mark 1:23

Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti,

Marko 1:24 Mark 1:24

akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza?

Marko 1:25 Mark 1:25

Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke.

Marko 1:26 Mark 1:26

Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka.

Marko 1:27 Mark 1:27

Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii!

Marko 1:28 Mark 1:28

Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando ya Galilaya.

Marko 1:29 Mark 1:29

Na mara walipotoka katika sinagogi, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na Yakobo na Yohana.

Marko 1:30 Mark 1:30

Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia habari zake.

Marko 1:31 Mark 1:31

Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia.

Marko 1:32 Mark 1:32

Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa hawawezi, na wenye pepo.

Marko 1:33 Mark 1:33

Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni.

Marko 1:34 Mark 1:34

Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua.

Marko 1:35 Mark 1:35

Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko.

Marko 1:36 Mark 1:36

Simoni na wenziwe wakamfuata;

Marko 1:37 Mark 1:37

nao walipomwona wakamwambia, Watu wote wanakutafuta.

Marko 1:38 Mark 1:38

Akawaambia, Twendeni mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana kwa hiyo nalitokea.

Marko 1:39 Mark 1:39

Akaenda akihubiri katika masinagogi yao, katika nchi yote ya Galilaya, na kutoa pepo.

Marko 1:40 Mark 1:40

Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa.

Marko 1:41 Mark 1:41

Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika.

Marko 1:42 Mark 1:42

Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika.

Marko 1:43 Mark 1:43

Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara,

Marko 1:44 Mark 1:44

akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao.

Marko 1:45 Mark 1:45

Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi, na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini kwa wazi; bali alikuwako nje mahali pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila mahali.