Marko Mlango 14 Mark

Marko 14:1 Mark 14:1

Baada ya siku mbili ilikuwa sikukuu ya Pasaka, na mikate isiyochachwa; wakuu wa makuhani na waandishi wakatafuta njia ya kumkamata kwa hila na kumwua.

Marko 14:2 Mark 14:2

Kwa maana walisema, Isiwe kwa wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia katika watu.

Marko 14:3 Mark 14:3

Naye alipokuwapo Bethania, nyumbani mwa Simoni mkoma, ameketi chakulani, alikuja mwanamke mwenye kibweta cha marhamu ya nardo safi ya thamani nyingi; akakivunja kibweta akaimimina kichwani pake.

Marko 14:4 Mark 14:4

Palikuwa na watu waliochukizwa katika nafsi zao wakisema, Kwani kupoteza marhamu namna hii?

Marko 14:5 Mark 14:5

Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa dinari mia tatu na kuzidi, wakapewa maskini. Wakamnung'unikia sana yule mwanamke.

Marko 14:6 Mark 14:6

Yesu akasema, Mwacheni; mbona mnamtaabisha? Amenitendea kazi njema;

Marko 14:7 Mark 14:7

maana sikuzote mnao maskini pamoja nanyi, na kila mpendapo mwaweza kuwatendea mema; lakini mimi hamnami sikuzote.

Marko 14:8 Mark 14:8

Ametenda alivyoweza; ametangulia kuupaka mwili wangu marhamu kwa ajili ya maziko.

Marko 14:9 Mark 14:9

Amin, nawaambia, Kila ihubiriwapo Injili katika ulimwengu wote, na hili alilotenda huyu litatajwa kwa kumbukumbu lake.

Marko 14:10 Mark 14:10

Yuda Iskariote, yule mmoja katika wale Thenashara, akaenda zake kwa wakuu wa makuhani, apate kumsaliti kwao.

Marko 14:11 Mark 14:11

Nao waliposikia walifurahi, wakaahidi kumpa fedha. Akatafuta njia ya kumsaliti wakati wa kufaa.

Marko 14:12 Mark 14:12

Hata siku ya kwanza ya mikate isiyochachwa, walipoichinja pasaka, wanafunzi wake wakamwambia, Ni wapi utakapo tuende tukuandalie uile pasaka?

Marko 14:13 Mark 14:13

Akatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni zenu mjini; atakutana nanyi mwanamume amechukua mtungi wa maji; mfuateni;

Marko 14:14 Mark 14:14

na po pote atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba, Mwalimu asema, Ki wapi chumba changu cha wageni, niile pasaka humo, pamoja na wanafunzi wangu?

Marko 14:15 Mark 14:15

Naye mwenyewe atawaonyesha orofa kubwa, imeandikwa tayari; humo tuandalieni.

Marko 14:16 Mark 14:16

Wanafunzi wakatoka, wakaenda mjini, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka.

Marko 14:17 Mark 14:17

Basi ilipokuwa jioni yuaja pamoja na wale Thenashara.

Marko 14:18 Mark 14:18

Nao walipokuwa wameketi chakulani, wakila, Yesu alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu, naye anakula pamoja nami, atanisaliti.

Marko 14:19 Mark 14:19

Wakaanza kuhuzunika, wakamwambia mmoja mmoja, Je! Ni mimi?

Marko 14:20 Mark 14:20

Akawaambia, Ni mmoja wa hao Thenashara, ambaye achovya pamoja nami katika kombe.

Marko 14:21 Mark 14:21

Kwa maana Mwana wa Adamu aenda zake kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu; ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa.

Marko 14:22 Mark 14:22

Nao walipokuwa wakila, alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa, akasema, Twaeni; huu ndio mwili wangu.

Marko 14:23 Mark 14:23

Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote.

Marko 14:24 Mark 14:24

Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi.

Marko 14:25 Mark 14:25

Amin, nawaambia ninyi, Sitakunywa tena kabisa uzao wa mzabibu, hata siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu.

Marko 14:26 Mark 14:26

Nao walipokwisha kuimba walitoka kwenda mlima wa Mizeituni.

Marko 14:27 Mark 14:27

Yesu akawaambia, Mtakunguwazwa ninyi nyote kwa ajili yangu usiku huu; kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo watatawanyika.

Marko 14:28 Mark 14:28

Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.

Marko 14:29 Mark 14:29

Petro akamwambia, Hata wajapokunguwazwa wote, lakini siyo mimi.

Marko 14:30 Mark 14:30

Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, Leo, usiku huu, kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu.

Marko 14:31 Mark 14:31

Naye akazidi sana kusema, Ijaponipasa kufa nawe, hata hivyo sitakukana kamwe. Na wote wakasema vile vile.

Marko 14:32 Mark 14:32

Kisha wakaja mpaka bustani iitwayo Gethsemane; akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa muda niombapo.

Marko 14:33 Mark 14:33

Akamtwaa Petro na Yakobo na Yohana pamoja naye, akaanza kufadhaika sana na kuhangaika.

Marko 14:34 Mark 14:34

Akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa mkeshe.

Marko 14:35 Mark 14:35

Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke.

Marko 14:36 Mark 14:36

Akasema, Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.

Marko 14:37 Mark 14:37

Akaja akawakuta wamelala usingizi, akamwambia Petro, Je! Simoni, umelala? Hukuweza kukesha saa moja?

Marko 14:38 Mark 14:38

Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu.

Marko 14:39 Mark 14:39

Akaenda zake tena, akaomba, akisema neno lilo hilo.

Marko 14:40 Mark 14:40

Akaja tena akawakuta wamelala, maana macho yao yamekuwa mazito, wala hawakujua la kumjibu.

Marko 14:41 Mark 14:41

Akaja mara ya tatu, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike; yatosha, saa imekuja; tazama, Mwana wa Adamu anatiwa mikononi mwao wenye dhambi.

Marko 14:42 Mark 14:42

Ondokeni, twendeni zetu; tazama, yule anayenisaliti amekaribia.

Marko 14:43 Mark 14:43

Basi alipokuwa katika kusema, mara Yuda alifika, mmoja wa wale Thenashara, na pamoja naye mkutano, wana panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee.

Marko 14:44 Mark 14:44

Na yule anayemsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni, mkamchukue salama.

Marko 14:45 Mark 14:45

Basi alipokuja, mara akamwendea, akasema, Rabi, akambusu.

Marko 14:46 Mark 14:46

Wakanyosha mikono yao wakamkamata.

Marko 14:47 Mark 14:47

Na mmoja wao waliokuwapo akafuta upanga, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio.

Marko 14:48 Mark 14:48

Yesu akajibu, akawaambia, Je! Ni kama juu ya mnyang'anyi mmetoka wenye panga na marungu, kunitwaa mimi?

Marko 14:49 Mark 14:49

Kila siku nalikuwa mbele yenu hekaluni nikifundisha, msinikamate; lakini haya yamekuwa ili maandiko yapate kutimia.

Marko 14:50 Mark 14:50

Ndipo wakamwacha, wakakimbia wote.

Marko 14:51 Mark 14:51

Na kijana mmoja alimfuata, amejitanda mwili wake nguo ya kitani; wakamkamata;

Marko 14:52 Mark 14:52

naye akaiacha ile nguo ya kitani, akakimbia yu uchi.

Marko 14:53 Mark 14:53

Nao wakamchukua Yesu kwa Kuhani Mkuu; wakamkusanyikia wote, wakuu wa makuhani na wazee na waandishi.

Marko 14:54 Mark 14:54

Naye Petro akamfuata kwa mbali, hata ndani katika behewa ya Kuhani Mkuu; akawa ameketi pamoja na watumishi, anakota moto mwangani.

Marko 14:55 Mark 14:55

Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda juu ya Yesu wapate kumwua; wasione.

Marko 14:56 Mark 14:56

Kwa maana wengi walimshuhudia uongo, walakini ushuhuda wao haukupatana.

Marko 14:57 Mark 14:57

Hata wengine wakasimama, wakamshuhudia uongo, wakisema,

Marko 14:58 Mark 14:58

Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono.

Marko 14:59 Mark 14:59

Wala hata hivi ushuhuda wao haukupatana.

Marko 14:60 Mark 14:60

Kisha Kuhani Mkuu akasimama katikati, akamwuliza Yesu, akisema, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini?

Marko 14:61 Mark 14:61

Lakini akanyamaza, wala hakujibu neno. Kuhani Mkuu akamwuliza tena, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mtukufu?

Marko 14:62 Mark 14:62

Yesu akasema, Mimi ndiye, nanyi mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija na mawingu ya mbinguni.

Marko 14:63 Mark 14:63

Kuhani Mkuu akararua nguo zake, akisema, Tuna haja gani tena ya mashahidi?

Marko 14:64 Mark 14:64

Mmesikia kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wote wakamhukumu kuwa imempasa kuuawa.

Marko 14:65 Mark 14:65

Wengine wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, na kumpiga makonde, na kumwambia, tabiri. Hata watumishi nao wakampiga makofi.

Marko 14:66 Mark 14:66

Na Petro alikuwa chini behewani; akaja mmoja wa vijakazi wa Kuhani Mkuu,

Marko 14:67 Mark 14:67

akamwona Petro akikota moto; akamkazia macho, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na yule Mnazareti, Yesu.

Marko 14:68 Mark 14:68

Akakana, akasema, Sijui wala sisikii unayoyasema wewe. Akatoka nje hata ukumbini; jogoo akawika.

Marko 14:69 Mark 14:69

Na yule kijakazi akamwona tena, akaanza tena kuwaambia waliosimama pale, Huyu ni mmoja wao.

Marko 14:70 Mark 14:70

Akakana tena. Kitambo kidogo tena wale waliosimama pale wakamwambia Petro, Hakika u mmoja wao, kwa sababu u Mgalilaya wewe.

Marko 14:71 Mark 14:71

Akaanza kulaani na kuapiza, Simjui mtu huyu mnayemnena.

Marko 14:72 Mark 14:72

Na mara jogoo akawika mara ya pili. Petro akalikumbuka lile neno aliloambiwa na Yesu, Kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu. Na alipolifikiri, akalia.