Marko Mlango 10 Mark

Marko 10:1 Mark 10:1

Akaondoka huko akafika mipakani mwa Uyahudi, na ng'ambo ya Yordani; makutano mengi wakakutanika tena wakamwendea; akawafundisha tena kama alivyozoea.

Marko 10:2 Mark 10:2

Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamwuliza, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe? Huku wakimjaribu.

Marko 10:3 Mark 10:3

Naye akajibu, akawaambia, Musa aliwaamuru nini?

Marko 10:4 Mark 10:4

Wakasema, Musa alitoa ruhusa kuandika hati ya talaka na kumwacha.

Marko 10:5 Mark 10:5

Yesu akawaambia, Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii.

Marko 10:6 Mark 10:6

Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke.

Marko 10:7 Mark 10:7

Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe;

Marko 10:8 Mark 10:8

na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja.

Marko 10:9 Mark 10:9

Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.

Marko 10:10 Mark 10:10

Hata nyumbani tena wanafunzi wakamwuliza habari ya neno hilo.

Marko 10:11 Mark 10:11

Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake;

Marko 10:12 Mark 10:12

na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini.

Marko 10:13 Mark 10:13

Basi wakamletea watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea.

Marko 10:14 Mark 10:14

Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao.

Marko 10:15 Mark 10:15

Amin, nawaambieni, Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa.

Marko 10:16 Mark 10:16

Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia.

Marko 10:17 Mark 10:17

Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele?

Marko 10:18 Mark 10:18

Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu.

Marko 10:19 Mark 10:19

Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako.

Marko 10:20 Mark 10:20

Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu.

Marko 10:21 Mark 10:21

Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.

Marko 10:22 Mark 10:22

Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

Marko 10:23 Mark 10:23

Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu!

Marko 10:24 Mark 10:24

Wanafunzi wakashangaa kwa maneno yake. Yesu akajibu tena, akawaambia, Watoto, jinsi ilivyo shida wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa Mungu!

Marko 10:25 Mark 10:25

Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.

Marko 10:26 Mark 10:26

Nao wakashangaa mno, wakimwambia, Ni nani, basi, awezaye kuokoka?

Marko 10:27 Mark 10:27

Yesu akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu.

Marko 10:28 Mark 10:28

Petro akaanza kumwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe.

Marko 10:29 Mark 10:29

Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili,

Marko 10:30 Mark 10:30

ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele.

Marko 10:31 Mark 10:31

Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho; na wa mwisho watakuwa wa kwanza.

Marko 10:32 Mark 10:32

Nao walikuwako njiani, huku wakipanda kwenda Yerusalemu; na Yesu alikuwa akiwatangulia, wakashangaa, nao katika kufuata wakaogopa. Akawatwaa tena wale Thenashara, akaanza kuwaambia habari za mambo yatakayompata,

Marko 10:33 Mark 10:33

akisema, Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi, nao watamhukumu afe, watamtia mikononi mwa Mataifa,

Marko 10:34 Mark 10:34

nao watamdhihaki, na kumtemea mate, na kumpiga mijeledi, na kumwua; na baada ya siku tatu atafufuka.

Marko 10:35 Mark 10:35

Na Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, wakamwendea, wakamwambia, Mwalimu, twataka utufanyie lo lote tutakalokuomba.

Marko 10:36 Mark 10:36

Akawaambia, Mwataka niwafanyie nini?

Marko 10:37 Mark 10:37

Wakamwambia, Utujalie sisi tuketi, mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako.

Marko 10:38 Mark 10:38

Yesu akawaambia, Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi?

Marko 10:39 Mark 10:39

Wakamwambia, Twaweza. Yesu akawaambia, Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa;

Marko 10:40 Mark 10:40

lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari.

Marko 10:41 Mark 10:41

Hata wale kumi waliposikia wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohana.

Marko 10:42 Mark 10:42

Yesu akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha.

Marko 10:43 Mark 10:43

Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu,

Marko 10:44 Mark 10:44

na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote.

Marko 10:45 Mark 10:45

Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.

Marko 10:46 Mark 10:46

Wakafika Yeriko; hata alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando ya njia.

Marko 10:47 Mark 10:47

Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu.

Marko 10:48 Mark 10:48

Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, Mwana wa Daudi, unirehemu.

Marko 10:49 Mark 10:49

Yesu akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo; inuka, anakuita.

Marko 10:50 Mark 10:50

Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu.

Marko 10:51 Mark 10:51

Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona.

Marko 10:52 Mark 10:52

Yesu akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani.