Marko Mlango 2 Mark

Marko 2:1 Mark 2:1

Akaingia Kapernaumu tena, baada ya siku kadha wa kadha, ikasikiwa ya kwamba yumo nyumbani.

Marko 2:2 Mark 2:2

Wakakusanyika watu wengi, isibaki nafasi hata mlangoni; akawa akisema nao neno lake.

Marko 2:3 Mark 2:3

Wakaja watu wakimletea mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne.

Marko 2:4 Mark 2:4

Na walipokuwa hawawezi kumkaribia kwa sababu ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo; na wakiisha kuivunja wakalitelemsha godoro alilolilalia yule mwenye kupooza.

Marko 2:5 Mark 2:5

Naye Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.

Marko 2:6 Mark 2:6

Na baadhi ya waandishi walikuwako huko, wameketi, wakifikiri mioyoni mwao,

Marko 2:7 Mark 2:7

Mbona huyu anasema hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu?

Marko 2:8 Mark 2:8

Mara Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri hivi mioyoni mwenu?

Marko 2:9 Mark 2:9

Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende?

Marko 2:10 Mark 2:10

Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza),

Marko 2:11 Mark 2:11

Nakuambia, Ondoka, ujitwike godoro lako uende nyumbani kwako.

Marko 2:12 Mark 2:12

Mara akaondoka, akajitwika godoro lake, akatoka mbele yao wote; hata wakastaajabu wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Namna hii hatujapata kuiona kamwe.

Marko 2:13 Mark 2:13

Akatoka tena, akaenda kando ya bahari, mkutano wote ukamwendea, akawafundisha.

Marko 2:14 Mark 2:14

Hata alipokuwa akipita, akamwona Lawi wa Alfayo, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate. Akaondoka akamfuata.

Marko 2:15 Mark 2:15

Hata alipokuwa ameketi chakulani nyumbani mwake, watoza ushuru wengi na wenye dhambi waliketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake; kwa maana walikuwa wengi wakimfuata.

Marko 2:16 Mark 2:16

Na waandishi na Mafarisayo walipomwona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?

Marko 2:17 Mark 2:17

Yesu aliposikia aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi; sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.

Marko 2:18 Mark 2:18

Nao wanafunzi wake Yohana na Mafarisayo walikuwa wakifunga; basi walikuja, wakamwambia, Kwani wanafunzi wa Yohana na wanafunzi wa Mafarisayo hufunga, bali wanafunzi wako hawafungi?

Marko 2:19 Mark 2:19

Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kufunga maadamu bwana-arusi yupo pamoja nao? Muda wote walipo na bwana-arusi pamoja nao hawawezi kufunga.

Marko 2:20 Mark 2:20

Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana-arusi, ndipo watakapofunga siku ile.

Marko 2:21 Mark 2:21

Hakuna mtu ashonaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; ikiwa ashona, kile kipya kilichotiwa huliharibu lile vazi kuukuu, na pale palipotatuka huzidi.

Marko 2:22 Mark 2:22

Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; ikiwa atia, ile divai mpya itavipasua viriba vile, divai ikamwagika, vile viriba vikaharibika. Bali hutia divai mpya katika viriba vipya.

Marko 2:23 Mark 2:23

Ikawa alipokuwa akipita mashambani siku ya sabato, wanafunzi wake walianza kuendelea njiani wakivunja masuke.

Marko 2:24 Mark 2:24

Mafarisayo wakamwambia, Tazama, mbona wanafanya lisilokuwa halali siku ya sabato?

Marko 2:25 Mark 2:25

Akawaambia, Hamkusoma popote alivyofanya Daudi, alipokuwa ana haja, na kuona njaa, yeye na wenziwe?

Marko 2:26 Mark 2:26

Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, zamani za kuhani mkuu Abiathari, akaila mikate ile ya Wonyesho, ambayo si halali kuliwa ila na makuhani, akawapa na wenziwe?

Marko 2:27 Mark 2:27

Akawaambia, Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato.

Marko 2:28 Mark 2:28

Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia.